22.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Jengo la CCM lateketea kwa moto

CCMNA BEATRICE MOSSES, MANYARA OFISI

JENGO la Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara lililopo mjini Babati, limeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Ndeng’asso Ndekubali, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa moja na nusu usiku.

Alisema moto huo ulianza kuwaka ofisi za juu ambako ndiko zilizopo ofisi zote za CCM na kusema kuwa hakuna kitu chochote kilichookolewa.

“Nilikuwa niko safarini kutoka Dodoma kikazi, nilipofika Singida nilipigiwa simu na kuambiwa jengo limeshika moto.

“Niliwasiliana na Kikosi cha Zimamoto, walifika eneo la tukio lakini wakashindwa kuzima moto kwa sababu hawakuwa na vifaa vya kutosha kutokana na moto kuwa ghorofa za juu,” alisema Ndekubali.

Alisema moto huo umesababisha hasara kubwa kwa sababu wakati unatokea hakukuwa na mtu eneo hilo.

“Mafaili yote, nyaraka, kompyuta, mashine za kudurufu, viti, meza, makabati na kila kitu kilichokuwapo pale ofisini kimeteketea… nawashukuru wananchi wote wenye mapenzi mema na Kikosi cha Zimamoto kusaidia kuuzima japo walizidiwa,” alisema Ndekubali.

Miongoni mwa ofisi zilizoungua katika jengo hilo ambalo halina bima, ni ofisi ya Jumuiya ya Wazazi Mkoa, Jumuiya ya Vijana, Jumuiya ya Wanawake, Ofisi ya Mwenyekiti na Katibu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua haraka iwezekavyo kujua chanzo cha moto huo.

“Tumegundua udhaifu, Zimamoto utendaji wao ulikuwa wa kusuasua, kama si wenzetu hawa wanaojenga barabara kufanya kazi ya ziada hali ingekuwa mbaya zaidi.

“Umefika wakati Serikali iimarishe kikosi  hiki, hasa ukizingatia ni makao makuu ya mkoa,” alisema Bendera.

Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Manyara, Heriel Kimaro, alisema kuna umuhimu wa jamii kupata elimu ya majanga.

Alisema hawakupata taarifa mapema, jambo ambalo lilisababisha wachelewe kufika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles