Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Faustina Mfinanga maarufu kama Nandy, ameweka wazi sababu ya kuamua kuvaa vazi ambalo amelifananisha na mtindo wa mavazi anayopendelea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Nandy amesema amevutiwa na uvaaji huo wa Rais Samia kiasi cha kuamua kuiga, akieleza kuwa vazi hilo ni zuri kwa wanawake.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Mwanza kuhusu tamasha lake la Nandy Festival litakalofanyika kesho, msanii huyo alikuwa amevalia ushungi mweusi na suti nyekundu aina ya Kaunda, muonekano uliovutia hisia za waandishi wa habari waliomwuliza kuhusu uvaaji wake wa kipekee.
“Rais amevaa vazi hilo la kipekee ambalo ni zuri, na wanawake kwa sasa wanavaa. Nikaona niwakilishe na mimi. Nitaenda kwenye tamasha la Nandy nikiwa kisamia, huu ni mwanzo tu, mtaona nikivaa zaidi ya hapa,” alisema Nandy kwa furaha.
Nandy ameongeza kuwa anatarajia kutumia muonekano huu kama sehemu ya kuwakilisha heshima na utambulisho wa mwanamke wa Kitanzania kupitia tamasha lake, ambalo litaendelea kuvutia mashabiki wake nchini kote.