24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Marando, Mwalimu watajwa ukatibu Chadema

b16marandoNa Fredrick Katulanda, Mwanza

WAKATI kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajiwa kuanza vikao vyake vya ngazi ya juu mkoani Mwanza leo, majina mawili yanatajwa kurithi nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbrod Slaa.

Dk. Slaa alijiondoa Chadema mwaka jana, baada ya kutofautiana na uongozi wa chama hicho kwa kile alichodai umehongwa fedha na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Dk. Slaa, alitoa kauli hiyo zikiwa zimepita siku 36 tangu aliposusia mkutano wa kumpokea Lowassa aliyegombea urais kupitia Chadema, chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), uliofanyika Julai 28 mwaka jana.

Wakati hali ikiwa hivyo, makada wawili wa chama hicho, Kaimu Katibu Mkuu, Salum Mwalim na Mwenyekiti Chadema Kanda ya Mashariki ambaye pia ni mwanasheria, Mabere Marando wanatajwa kurithi mikoba ya Dk. Slaa.

Mabere Marando na Salimu Mwalimu, yanatajwa kama  ndiyo yanayotarajiwa kupendekezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.

Taarifa za ndani kutoka kwa watu waliokaribu na Mbowe, zinasema ana siri nzito kutokana ya kubeba majina mawili ambayo atayawasilisha Baraza Kuu.

Akizungumza na MTANZANIA jana kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema majina ya Marando na Mwalimu yametawala kwa wajumbe.

“Tuna imani  kikoa cha Baraza Kuu, mwenyekiti  atawasilisha jina la katibu mkuu kwa ajili ya kuthibitishwa… unajua tayari mwenyekiti alishafanya mchakato wa kumpata  mrithi kupitia kikao cha tathimini ya mwaka kilichofanyika mkoani Kilimanjaro ambako wajumbe walipewa nafasi ya kupendekeza jina moja tu kila mmoja kwa ajili ya katibu mkuu,” alisema.

Alisema wakiwa kwenye kikao cha Moshi, Mbowe alitaka kujua mapendekezo ya wajumbe kwa kuomba kila mmoja kuandika jina moja la mtu ambaye wanaona anafaa kumrithi Dk. Slaa.

Alisema katika mapendeko ya wajumbe ambao waliandika majina kwa siri, jina la Marando lilipata kura nyingi.

“Marando ndiye lilikuwa chaguo la wengi, unajua nafasi hii inamtaka mtu mwandilifu, ambaye anakijua chama na anayeweza kujitolea na mwenye sifa.

“Kwa muda mrefu sasa, Marando amekuwa mgonjwa hali mbayo inaweza kumpa nafasi Mwalimu kuteuliwa kwenye nafasi hii,” alisema mjumbe huyo.

Wengine wanaotajwa ni mwanasheria wa chama hicho,Tindu Lisu,Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye na aliyekuwa mgombea mwenza wa Ukawa, Duni Juma Haji.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene, alisema kwa mara ya  kwanza vikao hivyo vinafanyika mkoani Mwanza kwa lengo la kuimarisha ofisi za kanda zilizoanzishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles