* Azushiwa kifo, baadhi ya watu wazimia
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
ALIYEKUWA mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewatoa hofu Wazanzibari kuwa bado yupo hai na afya yake imeimarika.
Ametoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yuko mahututi, huku mingine ikidai amefariki dunia.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, alizidiwa ghafla juzi akiwa kwenye ndege wakati akitoka Zanzibar kwenda Dar es Salaam.
Uvumi huo umekuja zikiwa zimebaki siku 10 kabla ya kufanyika uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar, baada ya ule wa awali kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mwaka jana.
Kuenea kwa uvumi huo kulisababisha vyombo vya habari kutafuta ukweli katika Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kiongozi huyo.
Ilipofika saa 7:00 mchana, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa akiwa na viongozi wengine mbalimbali wa chama hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Maalim Seif ni mzima wa afya.
Dakika 20 baadaye, Maalim Seif alitoka wodini alikokuwa amelazwa kwa kutumia ‘lifti’ akiwa ameambatana na daktari wake na watumishi wengine wa hospitali hiyo na kuanza kuwapungia mkono wananchi waliokuwa wakisubiri matibabu.
“Alhamdulilah, namshukuru Mungu mimi sijambo, ni mzima kabisa,” alisema huku akitembea mwenyewe bila msaada wa mtu akiwafuata wanahabari.
Akisimulia kilichotokea hadi akafikishwa hospitalini hapo na kulazwa, Maalim Seif alisema kuwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Zanzibar kuja Dar es Salaam juzi, ghafla alisikia kizunguzungu.
“Namshukuru Mungu nilikwenda bara Hindi (India) kwa matibabu ambako nilifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo na Ijumaa ya wiki iliyopita nilirudi salama na nikapokewa vizuri Zanzibar.
“Nikapumzika Jumamosi na Jumapili, siku ya Jumatatu nikaja Dar es Salaam, nimeondoka nyumbani mzima kabisa, bahati mbaya kufika ‘airport’ ghafla nikajisikia kizunguzungu, ikabidi wenzangu wanisaidie kupanda kwenye ndege,
“Tulifika Dar es Salaam salama, nikaletwa na kulazwa hapa Hindu Mandal na wenzetu walikuwa wamejiandaa vizuri, wakaanza kunifanyia vipimo,” alisema.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliyomaliza muda wake tangu Oktoba, mwaka jana, alisema madaktari walichukua vipimo na kuvifanyia uchunguzi.
Alisema akiwa anaendelea kupatiwa matibabu, baada ya saa mbili kupita hali yake ilirejea kama kawaida.
“Watanzania wasiwe na wasiwasi, mimi ni mzima, nimelala vizuri, nimeamka salama asubuhi, nimefanya mazoezi na naweza kutembea mwenyewe, hali yangu ni nzuri na hata mtu akitaka tushindane kutembea hadi Kibaha naweza,” alisema na kusababisha kicheko kwa wenzake.
Alisema kuwa anawashukuru wananchi, Wazanzibari, Watanzania wa ndani na nje ya nchi ambao wameonyesha mapenzi makubwa kwake.
“Wengi walikuwa na wasiwasi na wengine waliposikia nimeumwa kiasi hicho walizirai na kupoteza fahamu, yote hiyo ni dalili wananchi wana mahaba na mimi, nami nawapenda sana,” alisema huku akisisitiza kauli aliyoambiwa na madaktari wake kwamba
angeweza kupata ruhusa ya kurejea nyumbani wakati wowote jana.
DAKTARI WAKE
Daktari wa kiongozi huyo, Omary Suleiman, alisema baada ya jopo la madaktari kumfanyia uchunguzi, walibaini tatizo kubwa lililokuwa likimkabili ni uchovu kutokana na safari ndefu.
“Tulikwenda India ambako alifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo, tukarejea salama. Juzi tulikuwa tunakuja Dar es Salaam ambako alitakiwa kuhudhuria kikao Jumatatu jioni.
“Lakini tulipofika uwanja wa ndege kule Zanzibar akajisikia kizunguzungu, hali ile ilitokea kwa sababu safari ya kutoka India hadi kufika huku ilikuwa ndefu, ilikuwa ni takriban saa sita na hakupata muda wa kutosha wa kupumzika,” alisema Dk. Suleiman.
Kwa zaidi ya wiki tatu, Maalim Seif alikuwa nchini India alikokuwa anapatiwa matibabu na baadaye alirudi nchini na kukutana na baadhi ya wanachama wa CUF nyumbani kwake Mbweni, Zanzibar.
ATOKA HOSPITALI
Taarifa tuliozipata wakati tunakwenda mitamboni, zinasema kuwa Maalim Seif ameruhusiwa kurejea nyumbani na kutakiwa kuwa na mapumziko ya muda mrefu, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mawasiliano na watu wengi.
“Ameruhusiwa leo (jana) alasiri na madaktari wamemtaka awe na mapumziko ya muda mrefu, ikiwemo kutokuwa na mawasiliano na watu wengi kwa wakati mmoja na hata maongezi kwa njia ya simu mara kwa mara,” alisema mmoja wa watu wake wa karibu.