24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri aagiza mkataba nyumba 4,000 Dar upitiwe upya

Na Mwandishi Wetu -DODOMA

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, ameagiza kupitiwa upya mkataba wa mauziano ya nyumba 4,000 kati ya Kampuni ya PMM 2001 Ltd na wakazi wa Vingunguti, Dar es Salaam.

Uamuzi huo unafuatia kutozingatiwa kwa masharti ya mkataba ulioingiwa awali, ambao umeonekana kuwa na upungufu wa kisheria na hivyo kusababisha PMM 2001 Ltd kushindwa kuwalipa wamiliki wa nyumba katika eneo la Vingunguti kwa karibu miezi tisa kama walivyokubaliana jambo lililozua taharuki.

Dk. Mabula alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki, baada ya kukutana na pande zote mbili za kamati inayosimamia makubaliano ya uuzaji nyumba 4,000 katika mitaa minne ya Vingunguti ambayo ni Mnyamani, Mtambani, Mtakuja na Faru, Kampuni ya PMM 2001 Ltd na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli katika ofisi za wizara hiyo, jijini hapa.

Alisema baada ya kupitia mkataba wa mauziano ya nyumba katika eneo la Vingunguti, kati ya PMM 2001 Ltd na wamiliki wa nyumba, wamebaini kutofuata taratibu za kisheria na kubainisha kuwa wamiliki ambao hawajalipwa fedha yoyote hawabanwi na mkataba huo na wanaweza kuzifanyia shughuli yoyote nyumba zao.

“Kwa zile nyumba 80 ambazo PMM 2001 Ltd ilizinunua kwa wamiliki katika eneo hilo, wizara itatuma timu maalumu kufuatilia iwapo kampuni hiyo imefuata taratibu zote za mauziano, ikiwamo kutoa kodi ya Serikali,” alisema.

Kuhusu suala la wamiliki wa nyumba 17 ambao kampuni hiyo imewalipa Sh milioni 35 kwa kila mmoja kama fedha za awali, aliagiza hatua za kisheria zifuate kwa kuwa mkataba wa mauziano hauoneshi kiasi kilichobaki.

Dk. Mabula alisema kilichofanywa na PMM 2001 Ltd kwa wamiliki, ni udanganyifu unaoweza kutoa mwanya mkubwa kupoteza haki yao na kusisitiza Serikali  haiko tayari kuona  wananchi  wanapata tabu kufuatilia haki zao. 

Alisema atamwagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Dar es Salaam kuzungumza na wananchi wanaouza nyumba kwa kampuni hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utumishi wa PMM 2001 Ltd, Damian Kanuti, alijitetea kwa kueleza  kampuni yake ilishindwa kutekeleza makubaliano ya ununuzi wa nyumba katika mitaa ya Vingunguti kutokana na kuchelewa kupata mkopo ilioutarajia kutoka Benki ya TIB na kubainisha kuwa pamoja na sakata hilo, walishalipa Sh bilioni 1.7, ikiwa ni malipo ya nyumba 80 na fedha ya awali kwa wamiliki 17.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uuzaji Nyumba 4,000 katika eneo la Vingunguti, Ramadhani Pepo, aliilalamikia kampuni  hiyo kwa kutoonesha ushirikiano kwa kamati wakati wa mauziano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles