28.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

WAWEKEZAJI UTALII WAKAMATWA DODOMA

*Ni baada ya kuitikia wito wa Waziri Mkuu

*Yumo Balozi mdogo wa Cyprus Tanzania

Na Masyaga Matinyi-DAR ES SALAAM


WAWEKEZAJI wawili kwenye Sekta ya Utalii nchini wanashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukamatwa Dodoma juzi  mchana   na kusafirishwa kwenda Arusha jana.

Waliokamatwa ni George Mavroudis (Mtanzania mwenye asili ya Cyprus) ambaye ni Balozi mdogo (Consular) wa Cyprus Tanzania, pia Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni za Nyika Trade and Safaris Limited na George Mavroudis Safaris, zenye ofisi   Arusha.

Mwingine ni raia wa Ureno mwenye hati ya kusafiria namba CA020565, Ricardo Retto, kutoka Kampuni za Tyche Limited na Toya Limited, ambazo zinaendesha kambi za utalii katika maeneo ya Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro zijulikanazo kwa jina la East African Camps.

Pia Mavroudis ni mwekezaji kwenye kisiwa cha utalii cha Rukuba kilichopo Ziwa Victoria (wilayani Musoma Mkoa wa Mara), ambako anamiliki hoteli ndogo ya utalii yenye vyumba 10, hoteli ambayo Retto ameikodi kwa shughuli za biashara ya utalii.

Wawili hao walikwenda Dodoma kuitikia wito wa Waziri Mkuu ambao uliwataka kufika wenyewe na si kutuma wawakilishi kwa ajili ya kikao, Jumamosi, Septemba 15, 2018.

Kabla ya wito huo wa kwenda Dodoma, wawekezaji hao awali walipewa barua iliyoandikwa Septemba 5, 2018, ambayo iliwataka kuripoti kwenye makazi ya Waziri Mkuu  Dar es Salaam, Septemba 10 kuanzia saa 4.00 asubuhi.

Sehemu ya barua hiyo ilisema (tafsiri isiyo rasmi); “Mheshimiwa Kassim M. Kassim (Mbunge), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameitisha kikao kupokea taarifa ya uchunguzi kuhusu ukusanyaji mapato kutoka sekta ya utalii.

“Kikao kinatarajiwa kufanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu yaliyopo Oystebay, Dar es Salaam Jumatatu, Septemba 10 kuanzia saa 4 asubuhi.

“Kwa barua hii, unaarifiwa na kutakiwa kuhudhuria kikao hiki muhimu wewe mwenyewe na si mwakilishi. Tafadhali upe uzito unaostahili wito huu.”

Barua hiyo ilisainiwa na Deograsia J. Mdamu kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, na nakala kwa Ngole Keya, ambaye ni Katibu wa Waziri Mkuu

Taarifa zimedai kuwa  baada ya wawili kufika Dodoma na kusubiri kwa muda kuitwa kwenye kikao, waliarifiwa kuwa kikao kimeahirishwa tena  na kwamba wataambiwa tarehe nyingine ya kikao.

Baada ya kupata taarifa huku wakijiandaa kuondoka Dodoma, walifuatwa na kundi la watu ambao waliwakamata na kuchukua simu zao kabla ya kuwaweka mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma.

Taarifa kutoka vyanzo vya uhakika zimesema   baada ya kulala mahabusu, jana asubuhi walipelekwa Arusha wakiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema bado hana taarifa na kuelekeza suala hilo aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha.

“Mimi hizo taarifa hazijanifikia, lakini nitauliza, tuwasiliane baada ya saa moja.

“… lakini muulizeni Kamanda wa Polisi Arusha, ndiko kwenye mambo ya utalii, si hapa kwangu,” alisema.

Alipopigiwa baada ya saa moja, Kamanda Muroto alisema yupo kwenye kikao, kisha akakata simu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhani Ng’anzi, alisema bado hana taarifa kwa yupo akisimamia usalama kwenye uchaguzi jimboni Monduli.

Lakini aliahidi kulitolea ufafanuzi suala hilo baada ya saa 12.00 jioni.

“Kama wanaletwa kutoka Dodoma, jioni watakuwa wamefika, nitauliza kisha tuwasiliane kwa taarifa zaidi,” alisema.

Alipoulizwa kama ana taarifa za kukamatwa kwa wawekezaji hao, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema mpaka jana mchana alikuwa hana taarifa yoyote.

“Mimi mpaka muda huu sina taarifa yoyote, lakini kama wamekamatwa, basi ni moja kwa moja waliitwa Dodoma ili wakamatwe  na si vinginevyo, ila nitalifuatilia,” alisema Waziri Lugola.

KAULI YA TATO

Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara ya Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo, alisema tayari wana taarifa hizo, ambazo alisema kimsingi zinawachanganya akili.

“Nachofahamu,  hawa mabwana wawili wameshahojiwa na maofisa wa serikali, Mavroudis amehojiwa nadhani mara moja, lakini kuhusu huyu Retto mpaka sasa inasikitisha.

“Ameshahojiwa mara kadhaa na kamati na tume tofauti, wanasema kuhusu masuala ya kodi, lakini inatia shaka, kwa sababu kama ni kodi TRA wanajua taratibu za kufuata, lakini kwa huyu mwanachama wetu amekuwa akihojiwa na watu kutoka idara tofauti tofauti za serikali.

“Mara kadhaa tumefuatilia kujua tatizo ni nini, lakini hakuna mtu aliyewahi kutueleza tatizo au matatizo ya Retto. Ameshawekwa mahabusu mara kadhaa tunamdhamini, pasi yake ya kusafiria inashikiliwa, yaani mambo ni mengi, sasa hatuelewi.

“Siku nyingine alikuwa anatoka Arusha na familia yake kwenda Zanzibar kwa mapumziko, alipofika njia panda ya kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro, akakuta polisi wanamsubiri, wakamkamata mbele ya mke wake na watoto  na kurejea nae Arusha, kisha akawekwa mahabusu, tulipoulizwa tukaambiwa ni masuala ya kodi,” alisema Chambulo.

Alizishauri mamlaka husika ziwe wazi kuhusu mwekezaji huyo na kama hafai hapa nchini, basi utafutwe utaratibu wa sheria aondolewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles