29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI WA MAPAMBANO

*Gari la mbunge Chadema lapigwa risasi

*Wengine wakamatwa na bastola, panga vituoni

*CCM, Chadema wakabana Ukonga, Monduli

Na WAANDISHI WETU-MONDULI/DAR


NI uchaguzi wa vita. Ndivyo unaweza usema baada ya gari la Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Gidarya (Chadema),  kushambuliwa   matairi na watu wasiojulikana wakati akiwa katika Kata ya Majengo wilayani Monduli.

Tukio lilitokea jana asubuhi wakati mbunge huyo alipokuwa  na baadhi ya maofisa wa Chadema   akikagua maendeleo ya uchaguzi kwenye kata hiyo.

Akizungumza   tukio hilo, mbunge huyo alisema   lilitokea wakati akienda kusimamia uchaguzi wa ubunge  kwenye jimbo la Monduli mkoani Arusha jana.

Alisema baada ya tukio hilo alikwenda Kituo cha Polisi Mto wa Mbu ambako aliandika maelezo ya tukio   na anasubiri uchunguzi wa polisi   kubaini wahusika.

MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Ng’anzi ambaye alisema  hakuna risasi iliyopigwa kwenye magurudumu ya gari la mbunge huyo.

Alisema alifika  kituo cha Polisi Mto wa Mbu na kuona gari na maelezo ya mbunge.

“Nimetoka Mto wa Mbu sasa hivi, hakuna risasi kama inavyodaiwa kweye mitandao ya jamii. Kilichotokea ni ugomvi kati ya mbunge Gidirya na baadhi ya watu.

“Katika ugomvi huo kuna mtu mmoja anadaiwa alishuka kwenye gari nyingine na kutoboa magurudumu ya gari la mbunge akitumia kitu chenye ncha kali kama bisibisi au kisu.

“Mbunge amekiri kutambua gari husika na waliokuwamo… tunaendelea kutafuta gari   kujua kama ulikuwa ugomvi wa siasa, kwa sasa haya  ni mambo ya uchunguzi,” alisema Kamnada Ng’anzi.

Alisema  hadi   kukamilika   upigaji wa kura jana jioni na kuanza kuhesabu kura hali ya usalama ilikuwa shwari katika maeneo yote ya wilaya hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye pia ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo, Steven Ulaya alipinga madai ya viongozi wa Chadema kuwa mawakala wao walitolewa nje na kuzuiwa kuingia vyumba vya kupigia kura.

Wakati hayo yakiendelea Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na silaha kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika tukio hilo, mtuhumiwa mmoja anadaiwa kukutwa na bastola   yenye risasi 14 huku mwingine akikutwa na panga.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema watuhumiwa hao waliingia vituoni kama mawakala ingawa alipoulizwa majina yao hakuwa tayari kuwataja alisema  kufanya hivyo kunaweza kuharibu uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema mtuhumiwa aliyekutwa na bastola alikwenda kituoni na barua ambayo haina picha ingawa alipokuwa amekaa alishtukiwa na alipopekuliwa  alikutwa na bastola.

Akizungumzia hali ya uchaguzi wa udiwani katika Kata ya Vingunguti na ule wa ubunge Ukonga,  alisema ni shwari na hakuna vurugu zilijitokeza kuanzia asubuhi hadi saa 10.00 vituo vya kupigia kura vilipofungwa.

MAWAKALA WAZUIWA

Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Ukonga ulimalizika jana huku kukiwa na malalamiko ya kuzuiwa   mawakala wa Chadema  na idadi ndogo ya wapiga kura kujitokeza vituoni.

Jana asubuhi wakati wa upigaji kura ukiendelea,  Chadema kilidai   mawakala wake 26 wa Kata ya  Pugu Jimbo la Ukonga walizuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura wakidaiwa  kutokuwa na fomu namba 14.

Katibu Mwenezi wa Chadema wa Kata hiyo, Kassim Mfinanga, alisema fomu hiyo huwa inatumika kwa ajili ya maoni ya mawakala baada ya kumaliza kuhesabu kura.

“Leo (jana),  saa 12.00 asubuhi mawakala wetu waliingia vituoni kwa kutumia fomu ya hati za viapo lakini mawakala 26 kati ya 50 wa kata hii wamezuiliwa eti hawana fomu namba 14.

“Fomu hiyo si muhimu kwao,  mara nyingi wanakuwa nayo wasimamizi wa uchaguzi,” alisema Mfinanga.

Alivitaja baadhi ya vituo ambavyo mawakala walizuiwa na kuruhusiwa wachache kuwa  ni   Mustafa na Bustani Kinyamwezi.

Vingine ni Kigogo Fresh B ambacho mawakala saba wote walizuiwa na Kigogo Fresh A ambako kati ya 10 walioruhusiwa ni watatu.

Alisema kituo cha Ofisa Mtendaji wa Kata mawakala wapo sita kati ya hao walioruhusiwa ni watatu, Kituo cha Shule ya Msingi Kajiungeni kati ya mawakala sita walioruhusiwa ni wawili huku Kituo cha Kinani wakiruhusiwa wawili kati ya wanne.

NEC YAPINGA

Hata hivyo,  Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Jaji Semistocles Kaijage alikanusha madai yanayotolewa na vyama vya siasa kuwa mawakala wao walizuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi wa ubunge Jimbo la Ukonga na  Monduli.

Jaji Kaijage alisema katika maeneo mengi vituo vilifunguliwa mapema isipokuwa katika baadhi ya vituo ambavyo yalijitokea matatizo ya utaratibu, ambayo yalitatuliwa na baadaye vilifunguliwa.

Alisema uchaguzi huo katika majimbo mawili ya uchaguzi na kata tisa za Tanzania bara ulifanyika vizuri na vituo vyote vilifunguliwa kwa wakati isipokuwa vituo vichache ambavyo vilishindwa kufunguliwa kwa wakati kutokana na sababu za utaratibu lakini   tatizo hilo lilitatuliwa.

Kwenye majimbo mawili hasa Monduli.  katika vituo 256 uchaguzi ulikuwa ukiendelea vizuri jingawa alipata taarifa kuwa ni mawakala wanne wa Chadema walioshindwa kuingia katika vituo kutokana na kukosa sifa.

Alisema tatizo lililojitokeza ni kwamba mawakala walioapishwa ni wengine na waliofika vituoni ni wengine kwa hiyo hawakuruhusiwa kuingia vituoni na  hakuna wakala mwingine aliyezuiwa kuingia kituoni.

“Kwa ujumla katika uchaguzi wa majimbo hayo mawili na kata tisa uchaguzi unaendelea vizuri ingawa inaonekana mwitikio wa wapiga kura siyo mzuri katika baadhi ya vituo tulivyotembelea.

“Lakini labda inawezekana kwa sababu leo ni Jumapili na watu wengi badi wako makanisani na huenda idadi ikaongezeka baadaye,” alisema Jaji Kaijage

MNYIKA

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya kufungwa  vituo vya kupigia kura jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika alilalamikia mwenendo wa uchaguzi huo akidai  kumekuwa na viashairia vingi vya udanganyifu.

Mnyika alimlaumu Jaji Kaijage aliyesema kuwa uchaguzi uliaendelea vizuri wakati kukiwa na taarifa za kuzuiwa mawakala wa upinzani tangu saa 12.00 asubuhi hadi saa 2.00 ndipo walipoanza kuruhusiwa kuingia vituoni.

Alisema hatua hiyo ya Jaji Kaijage ni kudhihirisha kuwa udhaifu wote ulioonekana katika uchaguzi huo ulipata baraka za tume hiyo.

Alisema katika eneo hilo la Shule ya Msingi Juhudi alipozungumzia mwenyekiti huyo wa tume ya uchaguzi aambako kulikuwa na vituo 10, ni mawakala watatu tu wa Chadema walioruhusiwa   huku   mawakala wote wakiwa 10.

“Kwa taarifa tulinazo, ilipofika saa 12.00 asubuhi, muda ambao mawakala wanatakiwa kuwapo vituoni, mawakala wetu walikwenda katika vituo vyote 673, wakiwa na barua za chama lakini walizuiwa kwamba wawe na nakala za viapo,” alisema.

WAPIGA KURA WAJIVUTA

Pamoja na hali hiyo,   mwitikio mdogo wa wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Monduli, umeonekana kuwastua baadhi ya wagombea na wadau wa masuala ya siasa.

Jimbo la Monduli lina wapigakura 82,242 walioandikishwa Daftari la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku kukiwa na vituo vya kupigia kura 256.

Baadhi ya wananchi wilayani humo walijitokeza kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia saa 12.00 asubuhi, lakini   wapiga kura katika baadhi ya vituo  upigaji kura uliendelea   kusuasua hadi    mchana.

MTANZANIA lilitembelea baadhi ya vituo  mjini Monduli   na kukuta kukiwa hakuna foleni za wapiga kura , bali wakifika  mmoja mmoja, kupiga kura na kuondoka.

Akizungumzia mwitikio huo mdogo wa wapiga kura,   Mgombea ubunge wa CCM, Julius Kalanga aliyepiga kura Kituo cha Naja, alisema ilikuwa ni mapema kutoa tathimini ya idadi ya wapiga kura kwenye vituo.

“Mengi yanaweza kuchangia kujitokeza kwa wapiga kura; kwanza kuna wananchi waliopoteza vitambulisho, kuhama makazi. Lakini pia daftari la wapiga kura halijafanyiwa maboresho.

“Kwa ujumla wake hayo yanaweza kuchangia lakini kumbuka leo ni Jumapili, pengine wananchi wakitoka nyumba za Ibada wanaweza kupiga kura na kurejea majumbani mwao wakisubiria matokeo,” alisema Kalanga.

Mgombea ubunge wa Chama cha NRA, Feruz Juma, aliyepiga kura Kituo cha Meserani alitamba kuweka mawakala katika vituo vyote 256.

“Hili la mwitikio mdogo nadhani si jambo jema hasa wananchi wanapomchagua mwakilishi…   wanapaswa kujitokeza,” alisema Juma.

Naye Mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia Makini, Simon Ngilisho alisema hadi   mchana jana uchaguzi ulikuwa unakwenda vizuri katika vituo vyote vya kupigia kura.

Mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo, Willfred Mlay alisema chama chake hakikufanikiwa kuweka mawakala vituo vyote kwa sababu mbalimbali.

Hata hivyo wakati baadhi ya wagombea  wakijulikana walipigia kura maeneo yapi, Mgombea ubunge wa Chadema Laizer, anadaiwa kutojipigia kura kutokana na kutokuwamo kwenye daftari la kupigia kura la wilaya hiyo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema katika baadhi ya vituo vikiwamo vya Shule ya Msingi Orkeswa Kata ya Lashaine wakala wao hawakuapishwa, huku Kata ya Engaruka mawakala wao walizuiwa nje kwa kukosa vitambulisho.

Baadhi ya viongozi waliopiga kura wilayani humo ni  Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyepiga kura katika Kituo cha Shule ya Msingi Ngarash.

WAITARA

Mgombea ubunge wa Ukonga kupitia CCM, Mwita Waitara alisema hali ya uchaguzi ilikuwa  vizuri ingawa kuna watu wa Chadema kutoka Tarime walifika kufanya vurugu lakini anashukuru wamedhibitiwa na polisi.

“Nami nimepiga kura, nashukuru nimepiga kura ya ushindi. Kuna watu kutoka Tarime waliwekwa sehemu kufanya fujo lakini tunashukuru wamedhibitiwa,”alisema Waitara.

Akizungumzia kuhusu tishio la vurugu, Waitara alisema hakuna vurugu kwa sababu wageni waliofika wakati wa kampeni walikuwa walikuwa wamekwisha kuondoka na waliobaki ni wengi.

Naye Mgombea ubunge wa Chadema, Asia Msangi alisema alipiga kura lakini kuna changamoto nyingi zilizojitokea.

“Hali ni mbaya kuna figisufigusi ambazo zimejitokeza, mfano Mkurugezi wa NEC akiagiza A kwa wasimamizi wa uchaguzi wao wanafanya B…lakini sasa tusubiri majumuisho,” alisema Asia.

Mwisho.

 

MGOMBEA CCM ALIA NA MAJINA

Mgombea udiwani Kata ya Kizota   Dodoma, Jamali Ngalya (CCM), alilalamikia hatua ya kukosekana   majina ya baadhi ya wapiga kura kwenye vituo husika.

Akizungumza   wakati akitembelea vituo vya kupigia kura jana, Ngalya alisema alizunguka kwenye vituo vyoye vya kupigia kura lakini changamoto kubwa aliyoiona ni  baadhi ya wapiga kura kukosa majina yao vituoni.

“Kwa mfano, wapiga kura waliokuwapo kwenye Kituo cha Ofisi ya WEO ya zamani wamehamishiwa kwenye ofisi mpya ya WEO.

“Sasa wanapokwenda kupiga kura wanakosa majina yao na ofisi hizo zina umbali, kwa hiyo wengi wanakata tamaa na kuamua kurudi nyumbani bila kupiga kura,” alisema Ngalya.

Alisema pamoja na changamoto hiyo, idadi ya wapiga kura waliojitokeza ni ndogo kulinganisha na mwaka 2015.

Msimamizi wa Kituo hicho, Edwin Mkumbo, alisema upigaji kura ulifanyika kwa amani.

A;isema  alipokea barua za utambulisho za mawakala wa wagombea wa vyama vitatu kati ya vitano vilivyosimamisha wagombea.

 

Habari hii imeandaliwa na ELIYA MBONEA (ARUSHA), ANDREW MSECHU na ELIZABETH HOMBO (DAR)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles