
NA GABRIEL MUSHI, DODOMA
SERIKALI inatarajia kuzindua mpango kuawezesha wauguzi kufahamu jinsi ya kuwakagua watoto wa kike hususani wachanga wanapofikishwa kliniki ili kubaini waliofanywa ukeketaji.
Hatua hiyo pia itawezesha wazazi wao kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni Dodoma jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Fatma Hassa Toufiq (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kufuatilia wa kuwanusuru watoto wachanga wanaokeketwa na wazazi wao kukwepa mkono wa sheria.
Naibu waziri alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inazindua Mpango Kazi wa Taifa wa Kuzuia Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto 2017-2022 wenye lengo la kutokomeza masuala ya ukatili na mila zinazosababisha ukeketaji wa watoto wa kike.
Dk. Kigwangalla alisema serikali inaendelea kuelimisha vikundi mbalimbali kwa kupitia mangariba kwa kuanzisha madawati zaidi ya 417 ya jinsia na watoto katika vituo vya polisi.
Vilevile itaanzisha mtandao wa huduma ya mawasiliano ya kuwasaidia watoto na timu za ulinzi wa mtoto katika kila halmashauri mbalimbali kukabili tatizo la ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Alisema mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa mwezi huu.