Na Willbroad Mathias, DAR ES SALAAM
TRENI ya abiria inayofanya safari zake kati ya Kituo Kikuu cha Reli na maeneo ya Pugu Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ nusura ichomwe moto juzi, baada ya wananchi kudai kuchoshwa na usumbufu wa shirika hilo.
Wananchi hao walitaka warudishiwe nauli zao kwa kile walichodai Shirika la Reli Tanzania (TRL) limeshindwa kuwa na ratiba inayoeleweka.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 3:00 usiku eneo la Majumbasita, baada ya treni hiyo kukaa kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuambiwa kuambiwa chochote.
Hali hiyo iliwafanya abiria kuvamia kituo kidogo cha mawasiliano kilichopo eneo hilo wakitaka warejeshewe nauli zao vinginevyo wangekichoma moto pamoja na mabehewa ya treni hiyo.
MTANZANIA liliwashuhudia abiria wakitaka kuingia ndani ya kituo hicho huku wakiwalazimisha wafanyakazi waliokuwapo wawarudishie fedha zao za nauli.
Purukushani hiyo iliyodumu kwa takribani saa mbili ilimalizika kwa abiria hao kuvunja vioo vya mabahewa ya treni vipatavyo 30.
Wafanyakazi kuona hivyo walijifungia ndani ya kituo hicho huku polisi waliokuwa wakisindikiza treni hiyo wakitimua mbio kunusuru maisha yao.
Baadhi ya abiria walisema tangu Ijumaa iliyopita wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatishiwa tiketi huku treni ikichelewa na wakati mwingine kutoonekana kabisa.
Walisema jambo hilo limekuwa likiwasababishia hasara na kuwalazimu kutafuta usafiri mwingine na kuchelewa kufika kwenye majukumu yao.
Rashid Mpalamo mkazi wa Pugu alisema alipanda treni hiyo saa 2:30 usiku kwenye Kituo cha Reli Stesheni, lakini baada ya kufika Majumbasita waliambiwa wasubiri kwa kile kilichodaiwa kuwa treni ya mizigo ilikuwa imeanguka maeneo ya Pugu.
Meneja wa kituo hicho, Benedict Kassege alisema anashangazwa na kitendo cha abiria hao kuwavamia akidai kuwa wao hawahusiki na ukatishaji tiketi bali wanachokifanya ni mawasiliano ya njia hiyo.