29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa wawili wa ugaidi kortini Dar

Waandishi Wetu, Dar na Tanga
WATU wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakidaiwa kutoa mafunzo ya ugaidi kwa vijana wa Tanzania mkoani Tanga.

Mmoja wao anaelezwa kuwa alikuwa pia akitoa mafunzo ya jeshi kwa kundi la Hizbul al lililotaka kuipindua serikali ya Somalia mwaka 2010.

Washtakiwa hao, Ally Nassoro au Dk. Sule na Juma Zuberi au Kitambi, walifikishwa jana katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Peter Njike akisoma mashtaka ya washtakiwa, alidai kati ya Oktoba Mosi, 2010 na Januari 30, 2001, katika eneo la Doblen Kisimayu, Somalia, Nassoro aliwezesha watu kushiriki mazoezi ya jeshi ya kundi la Hizbul al, lengo likiwa ni kuipindua Serikali ya Somalia.

Nassoro pia anadaiwa kati ya Mei Mosi, 2013 na Agosti 31, mwaka jana, katika Msitu wa Nguu ulioko eneo la Gombe wilayani Muheza, Tanga, aliwapa mafunzo ya matumizi ya silaha watu ambao hawakuwapo mahakamani hapo, lengo likiwa ni kufanya ugaidi nchini.

“Shtaka la tatu linamkabili Zuberi. Anadaiwa kati ya Mei Mosi, 2013 na Agosti 23, mwaka jana katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, Dar es Salaam, alimsaidia Ally Nassoro kutekeleza vitendo vya ugaidi kwa kumpa sehemu ya kukaa na kutekeleza mipango yake.

“Zuberi unadaiwa katika kipindi hicho ukiwa na eneo la biashara katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, ulimruhusu Ally Nassoro kukaa na wenzake kupanga na kujadili mipango ya mafunzo kwenye Msitu wa Nguu kutekeleza vitendo vya ugaidi,” alidai Wakili Njike.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba kesi iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Hakimu Riwa alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 23, mwaka huu itakapotajwa tena na washtakiwa walirudishwa rumande.

Wakati huo huo, mtuhumiwa mwingine wa ugaidi, Jihad Swalehe, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Riwa akikabiliwa na shtaka la kuwezesha kutendeka vitendo vya ugaidi.

Wakili Njike alidai kati ya Machi 21, 2013 na Juni 2, mwaka jana, sehemu mbalimbali Dar es Salaam, alifanya mawasiliano na Nero wa Uturuki na Dacosta wa Ureno, akiomba uwezeshwaji wa malighafi, fedha, elimu na utaalamu ili kufanya vitendo vya ugaidi nchini Kenya.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu lolote na kesi hiyo imepangwa kutajwa Machi 23 mwaka huu.

Ujambazi mapango ya Mleni kortini
Kutoka Tanga inaelezwa kuwa watuhumiwa 10 wa ujambazi katika mapango ya Mleni, Tanga wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi huku ukiwapo ulinzi mkali wa polisi.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano tofauti kuhusiana na tukio la kuwanyang’anya polisi silaha na mauaji ya askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Sajenti Mohamed Rashid Kajembe.
Watuhumiwa hao ni Mbega Seif (25) maarufu kama Abuu Rajab,mfanyabiashara mkazi wa Kiomoni, Rajabu Bakari (19) mwanafunzi mkazi wa Makorora, Ayubu Ramadhani (27) maarufu kama Chiti, fundi umeme na mkazi wa Kona Z Kiomoni.
Wengine ni Hassani Mbogo (20) maarufu kama Mpalestina, mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Mohamed Ramadhani (19) mfanyabiashara na mkazi wa Makorora, Sadiki Mdoe (25) maarufu kama Kizota mkazi wa Magaoni.

Wengine ni Saidi Omari (26)mfanyabiashara na mkazi wa Magaoni Tairi Tatu, Nurdin Mbogo Makorora (27), Ramadhan Mohamed (18) mfanyabiashara na mkazi wa Donge pamoja na Omari Abdala (55) maarufu kama Amy mkazi wa Makorora Dunia Hoteli.
Wakili wa serikali, George Barasa akisaidiana na Maria Clara Mtengule alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Aziza Rutala kuwa shitaka la kwanza hadi la tatu linawahusisha washatakiwa namba moja hadi nane kwa kuhusika kula njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 384 sura ya 16 ya mwaka 2002.

“Katika maeneo tofauti ya Tanga kati ya Septemba mosi 2014 hadi Januari 26 mwaka huu, washtakiwa wote wanane kwa pamoja walitenda kosa la kula njama na kufanya kosa la unyang’anyi wa silaha,” alidai Barasa.

Katika shitaka la pili, Barasa alidai kwamba Januari 26 mwaka huu katika mgahawa wa Jamali uliopo kati ya barabara ya Nne na ya Tano jijini Tanga washitakiwa wote wanane waliiba bunduki ya SMG namba 14303545 mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.

Alidai muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walitumia visu kumchoma askari H 501 Mwalimu ili kupata silaha hiyo.

Katika shitaka la tatu ambalo ni la unyang’anyi wa kutumia silaha, washtakiwa wote wanane katika mgahawa wa Jamali uliopo kati ya barabara ya Nne na ya Tano, waliiba SMG nyingine namba 14301230 SMG, mali ya Jeshi la polisi Tanzania.

Alidai muda mfupi kabla ya kutenda kosa hilo walimtishia kwa kutumia nguvu kumnyang’anya silaha askari H Mansoor.

Katika shitaka la nne ambalo limemuhusisha mshatakiwa namba tisa, Nurdin Mbogo, wakili Barasa alidai katika sehemu isiyofahamika jijini Tanga, mshtakiwa Hassan Mboko (mshatakiwa namba nne) alitenda kosa Septemba mosi 2014 na Januari 26 mwaka huu kwa kumwezesha kukwepa kushtakiwa.

Wakili wa serikali, Mtengule alisoma shitaka la tano lililowahusisha mshtakiwa wa pili na wa 10 la kuhusika kumuua askari wa JWTZ Sajenti Mohamed Rashid Kajembe Februari 13 mwaka huu katika Mapango ya Amboni Jijini Tanga.

Hata hivyo washitakiwa wote namba moja hadi 10 walikana mashitaka dhidi yao. Mshitakiwa namba tisa, Nurdin Mbogo alishindwa kutimiza masharti ya dhamana baada ya kutakiwa kutoa Sh milioni moja na mdhamini mmoja mwenye mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh milioni moja.

Washtakiwa wote walirudishwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Machi 23 mwaka huu.

Februari 13 mwaka huu katika eneo la Amboni Jijini Tanga palizuka mapigano baina ya polisi wakishirikiana na askari wa JWTZ dhidi ya watu waliodaiwa kuwa ni majambazi,waliokuwa wamejificha katika mapango ya Majimoto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles