28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo TCAA aingia mtandao wa Escrow

Pg 4Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BARAZA ya Maadili jana lilimuhoji Mkurugenzi Mdhibiti Uchumi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Dk. James Diu, kwa tuhuma za kuomba, kudai fadhila za uchumi.
Kigogo huyo anadaiwa kupokea Sh milioni 80.8 kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira .
Mahojiano hayo ni muendelezo wa utetezi wa watumishi na viongozi wa umma wanaodaiwa kupata mgao kutoka katika kampuni hiyo kupitia akaunti ya Tegeta Escrow.
Dk. Diu alikana mashitaka hayo akidai kuwa fedha alizopewa hazikutoka kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited badala yake alipewa na Rugemalira binafsi kwa kuwa ni rafiki yake na alimpa kama mchango wa matibabu ya mke wake.
“Sijaomba wala sijadai maslahi ya uchumi kutoka kwa Rugemalira alinipa akiwa kama rafiki yangu wa karibu, rafiki wa familia… pia nilisoma naye shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1982-85 .
“Alikuja katika Hospitali ya TMJ na Sanitaris Mikocheni ambako mke wangu alikuwa amelazwa kwa bahati mbaya alifariki dunia mwaka jana.
“Lengo lilikuwa kuja kumuangalia lakini aliahidi kumuhudumia kwa kumpeleka India kwa matibabu… sijapokea zawadi nilichopokea ni mchango kama msaada wa matibabu ya marehemu mke wangu, nasisitiza haikuwa zawadi,”alisema Dk.Diu.
Alisema endapo angepokea zawadi angeiwasilisha kwa ofisa masuhuli na kwa kuwa ile haikuwa na mlengwa wa zawadi hakuona haja ya kuiwasilisha.
Alisema katika fomu ya rasilimali na madeni ambayo aliiwasilisha Desemba 30 mwaka jana alichelewa kumuarifu ofisa masuhuli kuhusu huduma za matibabu za mke wake kwa kuwa alijua halitawezekana ikizingatiwa waliwahi kushutumiwa kwa mkurugenzi aliyepita.
Alisema katika fomu hizo pia aliambatanisha nakala za kwenda na kurudi India alipokwenda kwa matibabu ya mke wake pamoja na gharama za Agosti 17 mwaka jana. Alizikwa Agosti 21.
“Katika shutuma hizo hapakuwapo mgongano wa maslahi,tuhuma hizo si za kweli kwa kuwa sina uhusiano wowote wa biashara na uchumi na Rugemalira wala kampuni zake,”alisema Dk.Diu.
Baada ya utetezi huo, Wakili wa baraza hilo, Getrude Cyriacus alisimama na kumuuliza maswali kama ifuatavyo:
Wakili: Ni kweli ulipokea fedha kutoka Kampuni ya VIP Engineering anda Marketing?
Dk.Diu:Sijapokea kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering nilipokea kutoka kwa Rugemalira. VIP haijawai kuhusika na mimi wala familia yangu.
Wakili:Lakini fedha zinaonekana zimetoka katika akaunti ya Mabibo Bear unawezaje kusema haujachukua fedha kutoka katika kampuni.
Dk.Diu:Mimi ameniwekea fedha hazikuambatanishwa na jina lolote la kampuni.
Wakili:Februari 8 mwaka jana ulitoa Sh milioni 40,Februari 10 ukatoa Sh milioni 35 na Februari 15 ulitoa Sh milioni 1.5,mpaka Desemba 13 ulitoa karibia Sh milioni 75 na zaidi ni kweli?
Dk.Diu: Kweli.
Wakili:Ulileta taarifa mbili za miamala ya benki moja ya kigeni nyingine za Tanzania
Dk.Diu:Kweli
Wakili:Uliingiziwa Dola 25000 kutoka Mabibo Bear kwa mujibu wa benki statement(taarifa ya benki),kweli?
Dk.Diu:Fedha niliahidiwa na Rugemalira lakini sijui zimetoka wapi.
Wakili:Unakubaliana na sisi kuwa tamko lako uliloliwasilisha katika baraza Sh milioni 80 na Bwana Godison kwamba uliuziwa nyumba isiyokamilika.
Dk.Diu:Sikumbuki.
Wakili:Unaweza kuturuhusu upitie tamko lako ujikumbushe ulichoandika.
Aliangalia na kujibu
Dk.Diu:Ni kweli ila haihusiani.
Wakili:Tamko lako la mwaka 2014 ulisema una upungufu wa madeni, deni la Sh milioni 80 limelipwa kwa nyumba ya Mbezi Kawe na hizo fedha zilitoka kwa Rugemalira, kweli?
Dk.Diu:Hizi ni tofauti na zilizotajwa.
Wakili:Kwa hiyo ulipewa Sh milioni 160 na Rugemalira.
Dk.Diu: Hapana.
Wakili:Dola 25000 (Sh milioni 45) kutoka kwa Rugemalira ulipokea Agosti 4 lakini matibabu ulisema yameanza Desemba 2013.
Wakili:Ulikuwa meneja wa udhibiti uchumi Ewura unaweza kutuambia inajishughulisha na nini.
Dk:Sikumbuki, mimi nilishatoka huko.
Wakili:Kiongozi, taasisi uliyoifanyia kazi inajishughulisha na nini?.
Dk.Diu:Kazi ya udhibiti wa nishati ikiwamo umeme.
Wakili:IPTL inahusika na umeme.
Dk.Diu:Sijui.

Wakili:Kama hujui basi nikueleze tu IPTL inahusika na umeme, wadau wenu walikuwa ni kampuni ya mafuta si ndiyo?
Dk.Diu:Sikumbuki.
Wakili:Uliingiziwa fedha na Kampuni ya Prime Fuel Tanzania Limited Novemba 4 mwaka jana, Dola 10,100 (sawa na Sh milioni 18) ni kweli?
Dk.Diu: Sikumbuki
Wakili: Kama hukumbuki vitu ambavyo vipo katika taarifa yako ya benki ngoja nikukumbushe; Desemba, Aprili 14 Dola za Marekani 3000, nakukumbusha tu miamala yako uweze kukumbuka ingawa akaunti ni ya kwako.
Dk.Diu:Akaunti ni yangu lakini miamala inaweza ikawa siyo sahihi kuna miamala mingine siitambui, naomba baraza lijiridhishe kwanza na akaunti kuangalia kama hazijakosewa.
Wakili:Kwa hiyo haya maelezo uliyoyaleta mbele ya baraza ukajiridhisha na kusaini yalikuwa ya uongo?
Dk.Diu:Nilikuta nimeandikiwa maelezo nikaambiwa nitie saini.
Wakili:Kwa hiyo hata ulichozungumza hukikumbuki?
Dk.Diu:Mpaka nione hiyo statement (maelezo), nakumbuka nilitoa Sh milioni 80 nilienda kulipa deni la nyumba, nilikopa sehemu nyingi ikiwamo DCB benki.
Wakili:Kwa hiyo na fedha za Rugemalira ni mkopo.
Dk.Diu:Siyo mkopo wa masharti nilipokea soft loan (mkopo wa masharti nafuu)
Wakili:Soft loan ni nini?
Dk.Diu:Kawaulize wanaohusika na madeni.
Wakili:Ulishawahi kukopa benki mara nyingi, ulishawahi kutumia utaratibu huu wa Rugemalira kupewa fedha bila maandishi?
Dk.Diu:Utaratibu wa benki tofauti na mtu binafsi.
Baada ya mahojiano hayo Wakili Getrude alisema mtuhumiwa ameshindwa kujitetea kwa kutoa kauli ambazo zinakinzana na matamko ya rasilimali na madeni pamoja na taarifa alizohojiwa na baraza hilo.
Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi aliahirisha shauri hilo na kuahidi kulipitia ili kutoa mapendekezo na kuyawasilisha katika mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria ya Maadili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles