24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kinana arusha kombora Ikulu

kinanaNA ELIYA MBONEA, DODOMA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amemshauri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, awachukulie hatua watumishi wote wa Serikali wanaohusishwa na mgawo wa fedha za Escrow.
Akihutubia wakazi wa mji wa Dodoma jana katika viwanja vya Barafu, Kinana alisema haiingii akilini kuona mtuhumiwa wa ufisadi akitokea ofisini kwenda kuhojiwa kuhusu jinsi alivyopewa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa viongozi wa umma kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika kutumikia nafasi zao badala ya kuzigeuza kuwa sehemu za kujitajirisha.
“CCM tumewapa adhabu wanachama wetu wanaotuhumiwa kwenye sakata la Escrow. Hivyo basi, namshauri Katibu Mkuu Kiongozi naye achukue hatua kwa watumishi wa Serikali wanaohusishwa na Escrow kwa kuwaweka kando.
“Haiwezekani watu wanatuhumiwa kwenye sakata la Escrow halafu bado wapo ofisini, ni vema wakakaa kando hadi hapo kitakapoeleweka,” alisema Kinana.
Pamoja na hayo, alisema amelazimika kuyasema hayo jukwaani kwa kuwa hana mamlaka ya kumwagiza Balozi Sefue awachukulie hatua watuhumiwa hao.
“Wanaotuhumiwa katika sakata hili wanapaswa kuwajibishwa kwani hii nchi ni ya Watanzania wote, si ya kikundi cha watu waliopo kwenye madaraka.
“Siku hizi kuna tabia ya watu kuiba halafu wanakusanya kikundi cha watu nyumbani au jimboni kwao ili wawashangilie na kuwatetea.
“Ni vema zaidi suala la uadilifu likapewa kipaumbele na CCM lazima isimame imara katika kusimamia maadili ya uongozi.
“Hakuna jambo baya kama inapofika wakati wananchi wakawa na shaka na uadilifu wa viongozi waliopo madarakani na kwa misingi hiyo, CCM lazima ijikite katika kuhakikisha suala la maadili linapewa kipaumbele na wale watakaokwenda kinyume, wachukuliwe hatua.
“Kunapokuwa na watu wamekosea halafu hakuna hatua zozote dhidi yao, wananchi wanajumuisha watu wote kuwa ni walewale ingawa wanachama wa CCM hawana tatizo bali viongozi walio wengi ndio wenye matatizo ya kimaadili.
“Kwahiyo, umefika wakati wa kuacha tabia ya kulindana, kama kiongozi ni rafiki yako, lakini ni mwizi au mlarushwa, ni vema akawekwa kando na urafiki wenu ukaendelea kuliko kumtetea na kumwacha kwenye nafasi aliyonayo,” alionya Kinana.
Ingawa hakutaja jina la kiongozi anayehojiwa kuhusu fedha za Escrow akitokea katika ofisi ya umma, Kinana alionekana kumgusa Msimamizi Mkuu wa Makazi ya Rais, Mnikulu Shabani Gurumo, aliyehojiwa na Baraza la Maadili la Watumishi wa Umma wiki iliyopita, akidaiwa kupokea Sh milioni 80 kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Akizungumzia matumizi ya Serikali, Kinana alisema ni muhimu ikaanza kupunguza matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.
Mbali na hilo, alisisitiza kwa viongozi mbalimbali kufanya kazi kwa kutanguliza utumishi uliotukuka badala ya utukufu.
“Tumefikia mahali kila mtu ni mheshimiwa, katibu kata ni mheshimiwa, katibu wa tawi ni mheshimiwa, mtendaji wa kijiji ni mheshimiwa. Haya ni matokeo ya watu kupenda utukufu badala ya utumishi,” alisema Kinana.
Aliongeza: “Viongozi wanapaswa kutambua kwamba wananchi si mali ya Serikali bali Serikali ni mali ya wananchi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles