23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 22, 2023

Contact us: [email protected]

Watuhumiwa 50 wa utakatishaji wapanda kisutu kwa mpigo

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MCHAKATO wa watuhumiwa takribani 50 waliotolewa magereza na kupelekwa katika Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kukiri makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, umekwama baada ya washtakiwa kudai hawajajiandaa kufanya hivyo kwa jana.

Kati ya watuhumiwa hao, 40 walitolewa katika Gereza la Segerea na 10 Gereza la Keko ambapo walifikishwa asubuhi mahakamani kwa hati ya wito.

Kwa nyakati tofauti watuhumiwa hao waliingia kwa mahakimu na kudai hawakuwa wamejiandaa hivyo kesi zao ziahirishwe hadi Oktoba 7.

Miongoni mwa watuhumiwa hao ni Michael Wambura anayetuhumiwa kutakatisha zaidi ya Sh milioni 100.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina kwamba mshtakiwa aliletwa kwa hati ya wito (remove order) kwa ajili ya kukiri makosa yake lakini kasema hayuko tayari hadi Jumatatu.

“Tunaifahamisha mahakama tutafaili makubaliano tuliyofikia kati ya mshtakiwa na DPP, mshtakiwa aliomba kukiri na atatekeleza Jumatatu,”alidai Wankyo.

Hata hivyo Wambura amedai uwezo wake kulipa ni Sh milioni 85 na si zaidi ya hapo.

Mchina

Raia wa China, Cheng Guo anayeshtakiwa kwa kusafirisha nyara za Serikali amechafua hali ya hewa mahakamani baada ya kukana kuandika barua ya kuomba msamaha na kukiri makosa ya kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh 267,407,400.

Mshtakiwa huyo anayedaiwa kusafirisha meno ya tembo na kucha za Simba, alikuwa miongoni mwa washtakiwa wengi waliotolewa gerezani kuletwa mahakamani kwa ajili ya kukiri makosa kutokana na barua walizoandika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon aliiwakilisha Jamhuri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi akidai mshtakiwa aliandika barua ya msamaha. “Uliandika barua ya kukiri makosa? alihoji Hakimu Shaidi.

Mshtakiwa alijibu hapana, hakuandika barua ya kukiri makosa, yeye aliandika barua ya kulalamika upelelezi unachelewa na kuomba msamaha. “Sijaandika barua ya kukiri makosa, sina hela za kulipa,”alidai.

Wakati huohuo, Raia wa Victam Bui Thi Yen Nhi, amehukumiwa kulipa faini ya sh milioni 22 baada ya kutiwa hatiani katika shtaka la kujihusisha na nyara za Serikali bila kibali.

Mshtakiwa huyo alipewa adhabu hiyo jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Wanjaa Hamza baada ya kukiri shtaka linalomkabili.

Akitoa adhabu hiyo, hakimu alimueleza kuwa, kwakuwa amekiri shitaka, mahakama inampa adhabu ya kulipa faini ya Sh milioni 22.1 au kwenda jela miaka miaka 15.

 Pia mahakama imeamuru nyara za Serikali alizokamatwa nazo mshtakiwa zitaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Mshtakiwa huyo kupitia wakili wake Eliya Mwingira, aliieleza mahakama kuwa watalipa faini.

Katika kesi hiyo, mshitakiwa huyo anadaiwa Machi 3 mwaka 2018, katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam alikutwa na nyara za Serikali ambazo ni kucha 98, meno 21, vipande vya mifupa 12 vyote vya Simba vya thamani ya dola 4,900  (sh milioni 11).

Polisi, mwanajeshi wakiri kuiba mafuta ya ndege

 Askari Polisi watano na mwanajeshi mmoja  waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi yenye mashtaka matatu likiwamo la wizi wa mafuta ya ndege yenye thamani zaidi ya Sh milioni nne na kutakatisha fedha hizo wamekiri makosa.

Wamekiri mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Mwaikambo. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Koplo Shwahiba(38), MT. 74164 SGT Ally Chibwana (47), wa jeshi la wananchi Tanzania, PC Elidaima Paranjo (38), PC Simon (28), PC Dickson  na PC Hamza.

Mahakama iliwatia hatiani na kuwapa adhabu ya kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh 500,000 na kulipa fidia ya mafuta Sh milioni 4.6 na mafuta yanataifishwa.

Katika shtaka la kwanza  inadaiwa, Julai 30,2019 katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere uliopo katika Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, watuhumiwa hao(askari), waliiba lita 2180 za mafuta ya ndege( Jet A-1/Ik yenye thamani ya Sh 4,647,760 mali ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Katika shtaka la pili imedaiwa, siku na mahali hapo washtakiwa hao walifanya uwizi wa mafuta hayo yenye thamani ya Sh Milioni 4.6.

NIDA

Kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA), Dickson Maimu na wenzake itakuja kwa mara nyingine Jumatatu Oktoba 7, Hakimu anayesikiliza hakuwepo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,690FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles