28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Mhasibu Takukuru agoma kukiri kwa DPP, mwenzake akiri alipa milioni 100 /-

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mhasibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai, amegoma kuomba msamaha na kukiri makosa 19 ya kutakatisha fedha na 19 ya kughushi mikataba ya kuuziana nyumba na viwanja.

Mshtakiwa wa pili na watatu wamegoma pia na wamekana kughushi na kutakatisha fedha huku mshtakiwa wa nne, Yasin Katera ameomba msamaha na kukiri kutakatisha fedha, kuficha ukweli wa nyumba ya Nyegezi Mwanza akijifanya yake wakati ya rafiki yake Gugai, hivyo aliamuriwa kulipa Sh milioni 100.

Washtakiwa hao walikana na mmoja kukiri makosa yake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali Mkuu, Pendo Makondo alidai kesi hiyo iliyofikia kusikilizwa ushahidi wa shahidi wa 28 na kwamba sasa wanaomba kubadili hati ya mashtaka kwa kuondoa mashtaka matatu ambapo mawili ya kughushi na moja la kutakatisha fedha.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Gugai, George Makaranga, Leonard Aloys na Yasini Katera.

Katika shtaka la kwanza mshtakiwa Gugai anadaiwa kati ya Januari 2005 na Desemba 2015 akiwa ofisa wa umma, aliyeajiriwa na Takukuru alikutwa anamiliki mali yenye thamani ya Sh 3,634,961,105.02 ambayo haiendani na kipato chake.

Gugai anakabiliwa na mashataka mengine ya kughushi 19 na kutakatisha 20 wakati mshtakiwa Makaranga anashtakiwa kwa kosa moja la kutakatisha na mshtakiwa Leonard anakabiliwa na mashtaka manne ya kughushi na manne ya kutakatisha fedha.

Mshtakiwa Yasini alikiri kosa la 40 la kutakatisha fedha ambapo anadaiwa kati ya Januari 2016 na Juni 2016 Dar es Salaam, alificha umiliki halali wa nyumba iliyopo katika viwanja namba 438 na 439 iliyopo Nyegezi Mwanza akijifanya ni mmiliki halali wakati ni mali ya Gugai ambaye ni rafiki yake.

Wakili wa Serikali Mkuu, Awamu Mbagwa alidai mshtakiwa alifanya hivyo ili kumsaidia rafiki yake kukwepa mkono wa sheria na alitumia mali hiyo kutakatisha fedha.

Baada kukiri, mahakama ilimtia hatiani Yasini na kumuhukumu kulipa faini ya Sh milioni 100 na imeamuru nyumba itaifishwe na kuwa mali ya Serikali.

Wakili Awamu aliomba mshtakiwa asipewe adhabu kali sababu alikiri makosa, huku wakili wake Shunde Mrutu aliomba mteja wake asipewe adhabu kubwa sababu afya yake sio nzuri, familia inamtegemea na amekaa ndani miaka miwili. Mahakama ilizingatia maombi hayo ikampa adhabu iliyotoa.

Mashtaka yaliyobakia:

Alidai shtaka la pili mpaka la sita, Gugai anadaiwa kughushi mikataba ya mauziano ya nyumba akionyesha kauza kwa watu mbalimali wakiwemo washtakiwa wenzake hivyo walionunua ndio wamiliki halali wakati si kweli.

Anadaiwa kuonyesha Agosti,2007 alimuuzia Zenna Mgallah plot namba 225 block 6, iliyopo Mbweni JKT, Julai 2011 alionyesha kauza nyumba namba 621,622 na 623 zilizopo block A Gomba Arumeru kwa Salehe Saa wakati si kweli.

Gugai anadaiwa Oktoba 20, 2013 kwa kughushi alionyesha kamuuzia Arif Premji nyumba namba 64 iliyopo Ununio,  Desemba 20,2014 alionyesha kamuuzia nyumba namba 737 block C Edith Mbatia iliyopo Mwarongo Tanga na shtaka la sita anadaiwa alidanganya kuonyesha kamuuzia Mbatia nyumba namba 1,2,3 block J iliyopo Mwarongo.

Shtaka la saba linamkabili mshtakiwa wa kwanza ambapo inadaiwa Novemba 20,2011 alighushi mkataba kuonyesha Gugai kamuuzia Makaranga nyumba namba 150 block 8 iliyopo Bunju akionyesha ndiye mmiliki wa nyumba hiyo.

Shtaka la 8 mpaka la 11 la kughushi pia linamkabili mshtakiwa wa kwanza na wa tatu Aloys ambapo inadaiwa Novemba 19,2009 Gugai alionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 275,277,296 na 297 zilizopo block 2  Nyamhongolo Mwanza.

Shtaka la tisa Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia Aloys nyumba namba 90block 5 Bugarika Mwanza,  shtaka la kumi kamuuzia Aloys nyumba namba 713 block B Kiseke Mwanza na Oktoba 20,2015 alionyesha kamuuzia nyumba nyingine namba 230 block B Nyegezi Mwanza.

Shtaka la 12 mpaka 20 linamkabili mshtakiwa wa kwanza Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Manwal Masalakulangwa Bunju, Bagamoyo na Buyuni Temeke.

Anadaiwa kughushi mkataba wa mauzo akionyesha kamuuzia nyumba Rose Abdallah Nyumba mbili Dodoma, Mwongozo Temeke,Chidachi North na Itege Dodoma.

Gugai anadaiwa kughushi akionyesha kamuuzia nyumba Patrick Magesa nyumba mbili zilizopo mkoani Tanga huku akionyesha mnunuzi huyo ndiye mmiliki.

 Shtaka la 23,24,25, 31 mpaka 39  yanamkabili Gugai anadaiwa kuficha umiliki wa mali huku akijua ni mazalia ya mali zisizo na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

Shtaka la 26 la kutakatisha fedha linamkabili Gugai na Makaranga  wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuficha umiliki wa nyuma aliyouza Gugai kwa Makaranga.

Shtaka la 27 mpaka mpaka 30 la kutakatisha linamkabili Aloys na Gugai wanadaiwa kutakatisha fedha akionesha kuuza nyumba nne kwa Aloys huku akijua ni zao la mali zisizokuwa na maelezo ambalo ni kosa tangulizi la utakatishaji fedha.

Shtaka la 31 mpaka la 39 linamkabili Gugai ambapo anadaiwa kutakatisha fedha kwa kumuuzia nyumba tatu Masalakulangwa,  nyumba nne za Rose na nyumba mbili Patrick huku akijua ni zao la rushwa ambalo ni kosa tangulizi la kutakatisha fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles