Watu 11 nyuma ya urais wa Mkapa

0
1295

Mwandishi wetu –dar es salaam

RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amewaanika watu 11 ambao walikuwa nyuma ya urais wake kuanzia kumshauri kuwania nafasi hiyo hadi kutengeneza timu na mbinu za kuwania kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hayo yapo katika kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu), ambacho kilizinduliwa na Rais Dk. John Magufuli juma lililopita.

Katika kitabu hicho, Mkapa anasema baada ya kushauriwa na marafiki zao hao, waliamua kumweleza Mwalimu Julius Nyerere juu ya uamuzi huo.

Kitabu hicho ambacho ni cha kwanza cha aina yake kuandikwa na kiongozi mstaafu wa Tanzania, pia kimeeleza jinsi alivyoandika kimemo kwenda kwa Mwalimu Nyerere kumweleza nia yake ya kuwania urais.

Katika kitabu hicho Mkapa anasema wiki chache kabla ya kufanya mazungumzo na Mwalimu Nyerere kuhusu nia yake ya kutaka kugombea urais, alijadiliana na rafiki zake.

Aliwataja marafiki hao kuwa ni Ferdinand Ruhinda na Kabenga Nsa Kaisi aliokuwa akifanya nao kazi chumba cha habari, marehemu Patrick Qorro aliyekuwa mbunge wa zamani, Jared Gachocha na Edgar      Maokola-Majogo waliokuwa wabunge, mabalozi Saleh Tambwe na Adam Marwa, na marehemu Suleiman Hemed.

Aliwataja wengine ni makada wa chama, Harrison Mwakyembe na Walter Bgoya na mfanyabiashara Yusuph Mushi.

“Balozi Suleiman Hemed yeye anastahili shukrani maalumu kwa sababu alikuwa na mimi kwenye mikutano mingi ya kampeni akitoa ushauri na akifanya tathimini ya waliokuwa wakihudhuria kampeni zile,” anasema Mkapa.

 Anasema Qorro na Gachocha waliongoza katika kuhakikisha anateuliwa na kuiweka pamoja timu ya kampeni.

“Walikuwa wanajitoa sana katika hili, wakati mwingine walilipa baadhi ya gharama za awali kutoka mifukoni mwao. Hawa watu wema walinisadia kufikia uamuzi wa kukutana na Mwalimu kumweleza nia yangu,” anasema Mkapa.

Katika kitabu chake hicho, anaeleza pia jinsi alivyomshirikisha Nyerere na kuibuka jina la Dk. Salim Ahmed Salim.

Anasema baada ya utumishi wa umma uliotukuka kati ya mwaka 1962 na 1995, alidhani ulikuwa wakati mwafaka kustaafu shughuli nyingine.

Lakini wakati huo huo, hali ya kisiasa ilivyokuwa nchini ilimfanya akose amani nafsini mwake kutokana na masuala kadhaa kutokwenda vizuri.

Miongoni mwa masuala ambayo yalikuwa yakimsumbua ni hali ya mishahara ya watumishi wa umma, makusanyo ya kodi yalikuwa chini, kulikuwa na sintofahamu kwenye mashirikisho ya wafanyakazi, hasa walimu na washirika wa maendeleo hawakuwa wakifurahia mambo yalivyokuwa yakifanyika nchini.

Mkapa anasema baada ya mashauriano na rafiki zake na mke wake, aliona anaweza kusaidia kuweka mambo sawa.

“Hatua yangu ya pili ilikuwa kumtaarifu Mwalimu. Nikaandika ujumbe kwenda nyumbani kwake Butiama alipokuwa nikisema; Ndugu Rais, natumaini ni mzima, nimeamua kutafuta kuteuliwa, na nakutumia ujumbe huu kwa sababu sitaki usikie kwa mtu mwingine asije akapotosha juu ya sababu za uamuzi wangu.”

Mkapa anasema alimpa ujumbe huo Joseph Warioba ambaye ni mwenyeji wa mji wa Bunda, ambao ni jirani na Butiama, ingawaje hakumwambia lolote kuhusu kilichomo kwenye ujumbe, na Mwalimu hakujadili lolote na Warioba kuhusu ujumbe huo.

Anasema kuwa alikuja kukutana na Mwalimu Nyerere Dodoma, ambako alikwenda kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya chama, na alitumia fursa hiyo kumweleza sababu za kutaka kuteuliwa.

Baada ya kumaliza kumweleza Mwalimu nia yake, alimshukuru kwa kumsikiliza, na kwamba alikuwa msikivu kwa kiwango cha juu, na alimsikiliza bila kutamka neno.

Mkapa anasema baada ya kumaliza, Mwalimu alimwangalia machoni na kumwambia; “Ahsante sana kwa kuwa mkweli na muwazi kwangu. Nami nitakuwa mkweli kwako.

“Sikuwahi kudhani siku moja utatafuta urais, wazo hilo halijawahi kuja mawazoni mwangu, na si tu kwamba sikutegemea utataka urais, lakini nilikuwa nikifikiria mtu mwingine ambaye angekuwa rais bora.

“Lakini juhudi zangu kumshawishi hazikufanikiwa, anasita, anadhani anaweza pata uteuzi kwenye sahani, hiyo si siasa, ni lazima upambane. Nilituma mjumbe kwake, lakini hakuonekana kuwa tayari.

“Ben nachoweza kukwambia, sitokuzuia, sitakupinga. Kama umeamua, endelea kama dhamira yako inavyokutuma.”

BARAZA LA MAWAZIRI

Mkapa anasema baada ya kuteuliwa na kushinda urais, aliwasiliana na Nyerere ambaye alimpongeza kwa ushindi na alimwomba amsaidie kujua ni nani anastahili kuwepo na kwenye Baraza la Mawaziri.

Anasema Nyerere alimwambia; “Ben, hili ni baraza lako, siyo langu. Ni Serikali yako, siyo yangu. Kwa hiyo kaa uunde baraza. Ushauri pekee ninaokupa ni kwamba kwanza, tuna makabila mengi, hilo hutakiwi kulipuuza hilo.

 “Jitahidi kuweka usawa, na pili tuna dini nyingi, ila tuna dini kubwa mbili, hili pia hutakiwi kulipuuza. Zaidi ya hapo, hii ni Serikali yako, ni baraza lako, nenda kaliunde.”

Anasema katika uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri, aliamua kuwa wazi na alidhamiria kuwaacha waliowahi kuwa mawaziri wakuu, Cleopa Msuya na John Malecela, uamuzi mgumu uliowashangaza wengi.

“Nilikuja kusikia kuwa Mwalimu aliposikia taarifa hizo kuwa wawili waliowahi kuwa mawaziri wakuu si miongoni mwa mawaziri niliowateua, alisema hakuwahi kujua kuwa nina maamuzi magumu namna hiyo,” anasema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here