29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Mbowe alazwa Aga Khan, kina Mdee waenda Segerea

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amelazwa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

Mbowe ni miongoni mwa viongozi tisa wa Chadema wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi ambayo iliendelea jana kwa hatua ya utetezi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alitakiwa kuendelea kujitetea jana, lakini mdhamini wake, Greyson Selestine aliieleza mahakama hiyo kuwa anaumwa na amelazwa katika hospitali hiyo.

“Mbowe amelazwa tangu Novemba 17 mwaka huu katika Hospitali ya Aga Khan,” alisema Selestine bila kueleza anaumwa nini.

Alipoulizwa na MTANZANIA kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu hali ya afya ya Mbowe, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema ni kweli amelazwa katika hospitali hiyo na anaendelea na matibabu.

Kuhusu kesi hiyo, washtakiwa John Heche (Mbunge wa Tarime Vijijini), Ester Bulaya (Bunda), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini) na Halima Mdee (Kawe) walitakiwa kujitetea kwanini wasifutiwe dhamana.

Ijumaa iliyopita, mahakama hiyo ilitoa amri ya kukamatwa kwa washtakiwa hao kutokana na kukiuka masharti ya dhamana baada ya kutofika mahakamani kusikiliza kesi hiyo.

Siku hiyo wenzao watano ambao ni Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Vincent Mashinji, naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) na Esther Matiko (Tarime Mjini) walifika mahakamani hapo.

Amri ya kukamatwa kwa wabunge hao wanne ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya kutokuwepo mahakamani bila taarifa yoyote wala wadhamini wao.

Kutokana na hilo, wabunge hao wanne ambao walikuwa mahabusu Oysterbay jana, wamelala Gereza la Segerea wakisubiri leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa uamuzi wa kuwafutia ama kutowafutia dhamana kwa kukiuka masharti.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisikiliza hoja za pande zote mbili na maelezo ya washtakiwa ya kwanini wasifutiwe dhamana jana kwa saa nne na kuahidi kutoa uamuzi leo.

Kabla ya kufikia hatua hiyo, washtakiwa walipewa nafasi ya kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana ambapo Msigwa alianza kwa kuomba radhi kwamba haikuwa nia yake kuidharau mahakama, tangu kesi ianze hajawahi kuchelewa, hajawahi kukaidi amri ya mahakama na kwamba anaheshimu kiti cha hakimu.

Anadai alitokea Dodoma akidhani kesi ni saa nne na nusu kama kawaida akiwa na Heche, lakini walipofika walikuta kesi imeisha na juhudi za kumuona hakimu kumaliza tatizo hilo zilishindikana.

Mdee pia aliomba radhi, alionyesha jinsi anavyoiheshimu mahakama na kwamba alichelewa kwa kuwa alipitia kupima presha zahanati na alipofika kesi ikawa imeisha na amri imeshatolewa.

Anadai amekuwa na kesi mbili tofauti mbele ya Hakimu Simba, lakini hajawahi kukosa kufika mahakamani kwani hata pale ambapo Jamhuri wamekuwa hawana shahidi alikuwa anafika, kesi inaahirishwa.

Martha Mtiko ambaye ni mdhamini wa Mdee, alidai aliwahi mahakamani lakini kesi ilipoitwa alikuwa chooni na alipotoka alikutana na wenzake wanashuka, kesi imeahirishwa.

Anadai alifanya juhudi na wadhamini wenzake kuhakikisha tatizo hilo linaisha, lakini hawakufanikiwa na alipomfuata Hakimu Simba alijibu kuwa tayari alishatoa uamuzi.

Heche anadai aliomba asifutiwe dhamana, ambapo alidai anaiheshimu mahakama, hajawahi kuidharau, siku ya kesi alikuwa Dar es Salaam, lakini alijua kama kawaida kesi yao inasikilizwa saa nne na nusu hivyo alipofika alikuta imeahirishwa.

Akijitetea, Bulaya alidai Novemba 14, alienda msibani Singida kumzika mama yake mdogo, lakini aliwapa taarifa wadhamini wake ambao siku ya kesi Novemba 15, mwaka huu walikuwepo katika eneo la mahakama.

Wadhamini wanaomba mahakama isimfutie Bulaya dhamana kwani wanaendelea kumdhamini na wana imani naye.

Mshtakiwa Heche wadhamini wake hawakuwepo, Mchungaji Msigwa wadhamini pia hawakuwepo, lakini alidai mdhamini mmoja kahama chama hivyo hana mawasiliano naye.

Wakili wa Serikali, Salim Msemo alidai upande wa Jamhuri unasisitiza mahakama iwafutie dhamana washtakiwa hao kwani muda ambao shauri limeitwa mahakamani hawakuwepo.

Alidai hoja ya kutofika mahakamani haiwezi kuondolewa na hoja kwamba walifika baada ya mahakama kumalizika.

Akiwatetea, Wakili Peter Kibatala alidai hakuna sababu za kimazingira wala kisheria za kuwafutia dhamana washtakiwa.

Alidai uamuzi wa kuwapa dhamana washtakiwa ni mwepesi kuliko uamuzi wa kuwafutia dhamana na kwamba hakuna ubishi kuwa washtakiwa wana rekodi nzuri ya kuhudhuria mahakamani.

Alidai washtakiwa wote walifika mahakamani siku hiyo kwa kuchelewa isipokuwa Bulaya, hivyo aliomba wasifutiwe dhamana.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja zote iliamuru kutoa uamuzi leo. Washtakiwa wote walikuwepo isipokuwa Mbowe.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles