25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WATIBET HUZIKA WAPENDWA WAO TUMBONI MWA TAI

KWA mara nyingine katika safu yako hii uipendayo tunakuja na moja ya tamaduni nyingine za kushangaza, ambazo bado zingalipo duniani.

Safari hii tunasafiri hadi katika eneo la Tibet, lililopo katika vilima vya Tibet kwa upande wa kaskazini wa safu za milima Himalaya, nchini China.

Eneo hilo limepewa jina la utani kama ‘Paa la Dunia’ kutokana na vilele vyake virefu vya milima visivyo na mpinzani duniani.

Ni eneo linaloshea Mlima Everest na taifa la Nepal na ni eneo maarufu kwa watawa wa Kibuddha, akiwamo kiongozi wake wa kiroho na mwanaharakati maarufu duniani wa haki za kiraia, Dalai Lama.

Sasa jamii hiyo katika eneo hilo lisilofikika kirahisi, wana mila ya kugeuza matumbo ya tai, hasa wale walao mizoga maarufu kama tumbusi kuwa makaburi ya wapendwa wao
Mila yao hii ya ajabu ya mazishi ya wapendwa wao hujulikana kama ‘mazishi ya angani’ na hufanyika zaidi katika jimbo la Tibet la Qinghai pamoja na Mongolia.

Kabla ya kuzika miili ya wapendwa wao katika makaburi ya matumbo ya tai, mwili wa marehemu hukatwa katwa vipande na kuwekwa juu ya mlima.

Mlimani hapo mwili huo huachwa uliwe na tumbusi, yaani vulture kwa lugha za wenzetu.

Jamii hizo za majimboni humo huamini kwamba haina maana kuuhifadhi mwili au kutumia ardhi vibaya kwa kuzika kasha tupu, wakiamini kufanya hivyo ni kuharibu mazingira pamoja na uchoyo wa kuwanyima wanyama wengine mlo mahsusi.

Ilin kuepuka na ukosefu huo wa ‘haki’ kwa wanyama wengine pamoja na kulinda mazingira, suluhu huwa kuweka mwili katika eneo la wazi ambapo wanyama au hawa tumbusi watajipatie msosi.


Picha hizi za kushtusha zinatoa utambuzi wa nadra juu ya ibada ya mazishi ya siri ya jamii za Tibeti zilizopo karibu na bonde la Larung lililopo mita 4,000 juu ya usawa wa bahari.

Sehemu kubwa ya Watibetans na Wamongolia ni waumini wakubwa wa utamaduni wa madhehebu ya Kibudhha ya Vajrayana, ambayo hufundisha mhamo wa roho kuingia katika roho ya mtu mwingine wakati anapofariki.

Hilo linaanisha kwamba hawaoni hitaji la kuuhifadhi mwili katika kasha tupu, na hivyo huuzika kupitia mazishi ya angani, ikiwa ni aina ya kujitoa kafara. 

Kwa Watibet, tumbusi ni Dakinis kwa lugha yao, yaani malaika au wachungaji wa roho angani, ambao huichukua roho na kuipeleka mbinguni ambako watasubiri ufufuo kuelekea maisha mapya.

Utoaji huo kafara wa mwili wa binadamu unahesabika kama kitendo cha haki kwa sababu kinaokoa maisha ya wanyama wengine wadogo, ambao tumbusi ili wasife njaa wangewawinda kwa ajili ya chakula chao. 

Ikimaanisha wanajitoa kafara kwa gharama ya wanyama wengine wadogo wanaopaswa kuendelea kuishi badala ya kuliwa na tumbusi.

 

Wakati wa ibada, watazamaji hukusanyika kilimani karibu na bonde maarufu la Larung lililopo karibu na Taasisi ya  Buddha ya Wuming kushuhudia mazishi hayo.

Katika siku kuelekea sherehe za watawa wa Kibuddha zijulikanazo kama lamas – wanaweza kushuhudiwa wakipaza sauti kuzunguka mwili na kuchoma viungo vya kuchochea harufu nzuri. 

Baada ya kupaza sauti, mwili unakatwa katwa vipande na watu wajulikanao kama rogyapas, yaani ‘wavunjaji wa miili, ambao hutumia mapanga na mashoka kuukata kata haraka.

Wakati wavunja vunja mwili wanapoanza kazi hiyo haramu, tumbusi huzunguka juu angani katika eneo la tukio wakisubiri karamu, yaani ‘sadaka’hiyo maalumu kwa ajili yao. 

Inadhaniwa kuwa mwili mzima unatolewa kwa tumbusi ili kuruhusu roho kuhamia katika ulimwengu mpya.

Kugundua kikamilifu mchakato huo wa mazishi si kazi rahisi kwa vile Watibetans hupinga vikali kutembelewa na watalii wakati wa ibada, na hivyo picha kutojulikana kikamilifu kwa wengine duniani. 

Wakati wa kitendo hicho watawa wa Tibet wa madhehebu hayo ya Buddha hujikinga na harufu mbaya inayotokana na miili iliyooza karibu na bonde hilo la Larung.

Wananchi wa Tibet huhimizwa kushuhudia ibada hiyo, kukikabili kifo na mhamo wa maisha, ambao kwa mujibu wa Buddha maisha ya hapa duniani ni ya muda, bali hutakiwa kuyawekeza katika dunia nyingine nzuri zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles