25.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 29, 2022

Contact us: [email protected]

Watetezi haki za binadamu msijihusishe siasa – THRDC

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC) umewataka watetezi wa haki za binadamu kutojihusisha na shughuli za kisiasa ili kuondoa dhana ya kutambulika kama wanasiasa na kutengeneza mgawanyiko kwa wananchi wenye itikadi tofauti.

Vilevile katika kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba, mashirika wanachama wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu wametakiwa  kuboresha mahusiano na Serikali kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta tija kwa maendeleo katika  jamii.

Hayo yalielezwa  jana jijini hapa na Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Olengurumwa alitoa wito kwa watetezi wa haki za binadamu kutojihusisha na shughuli za kisiasa ili kuondoa dhana ya kutambulika kama wanasiasa na kutengeneza mgawanyiko kwa wananchi wenye itikadi tofauti.

“Tupo kwenye kipindi cha uchaguzi, hivyo nitoe rai kwa wanaharakati wote wa haki za binadamu wanapaswa kuchagua siasa au kuendelea kuwa watetezi wa haki za binadamu, mambo haya hayapaswi kwenda pamoja ili kuepusha migogoro katika jamii,” alisema Olengurumwa.

Alisema mashirika hayo yakifanya kazi na Serikali yatafanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutatua baadhi ya changamoto kwa haraka na kuwasilisha agenda muhimu za makundi mbalimbali ya haki za binadamu.

Olengurumwa  alisema kuna baadhi ya taasisi zinazojihusisha na masuala ya utetezi wa haki za binadamu zimekuwa zikikiuka taratibu na misingi ya mlengo wa uanzishwaji wa taasisi hizo na kuzua taharuki kwenye jamii jambo ambalo linapaswa kupingwa.

Alisema ikiwa watetezi wa haki za binadamu watafanya kazi kwa ukaribu na serikali itawasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima na itawarahisishia kufanya kazi kwa uhuru na kufanikiwa kutimiza malengo yao kwa wakati.

Akieleza hali ya utetezi wa haki za binadamu kanda ya kati, Olengurumwa alieleza kuwa mashirika ya haki za binadamu yamekuwa chachu na hamasa ya wanawake  na watoto kujitambua hasa katika kutoa taarifa pindi wanapokutana na matukio ya ukatili wa kijinsia.

“Kupitia klabu na masunduku ya maoni yaliyoanzishwa sehemu mbalimbali yamesaidia kwa kaisi kikubwa wanawake na watoto kutoa taarifa za ukatili pindi zinapovunjwa, hatua hii imesaidia kupunguza changamoto za ukeketaji na ndoa za utotoni,” alisema Olengurumwa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dodoma, William Mtwazi, alisema  Tanzania ikiwa inajiandaa kuelekea uchaguzi mkuu, watetezi wa haki za binadamu wanapaswa kujenga utaratibu wa kushirikiana katika kuhakikisha matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanatokomezwa.

Mtwazi alisema baadhi ya kazi za watetezi wa haki za binadamu hazijulikani kutokana na baadhi yao kuhusishwa na masuala ya kisiasa na kupata vitisho vya kiusalama wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao hali ambayo imepelekea kukosekana kwa umoja kwa baadhi ya wanachama wa mtandao kuhofia usalama wao na familia zao.

Naye mwanasheria wa LHRC kituo cha Dodoma, Joyce Eliezer alisema licha ya mtandao wa watetezi wa haki za binadamu kuwa na jukumu la kutetea haki za raia bado mtandao huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mashirika wanachama kutokuwa na rasilimali fedha za kuendeshea shughuli za kutoa elimu ya uchaguzi licha ya kuwa wamepata vibali vya uchaguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,444FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles