27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

Takukuru yataka viongozi kutochaguliwa kwa misingi ya rushwa

Na YOHANA PAUL-MWANZA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza imewatahadharisha wananchi mkoani hapa kutokuchagua viongozi kwa misingi ya rushwa badala yake wachague viongozi wazalendo, waadilifu na wachapakazi ili kuchagiza maendeleo ya kijamii katika maeneo yao.

Tahadhari hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa vyombo vya habari katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Stenga alisema rushwa ya kiwango chochote itakayotolewa na mgombea inaweza kuwagharimu wananchi kwa kukosa maendeleo na kutokuwa na utatuzi wa changamoto zinazowakabili na hiyo ni kwa sababu mgombea akichaguliwa kwa kutoa rushwa atajikita zaidi katika kurejesha fedha alizotumia kutoa hongo.

“Nawakumbusha wananchi wa Mkoa wa Mwanza, kwamba kipindi kipindi cha mchakato wa uchaguzi siyo kipindi cha mavuno, ambacho wananchi wanaweza kukitumia kujipatia chochote kwa njia rushwa badala yake ni kipindi cha wao kutafakari kuhusu changamoto walizonazo na viongozi sahihi wa kuzitatua,” alisema Stenga.

Alisema kwa kipindi hiki cha uchaguzi wa kura za maoni tayari Takukuru Mwanza imeshafungua majalada sita ya watuhumiwa 13 ambao wapo kwenye uchunguzi ambapo kati yao, watuhumiwa sita  ni watia nia na wagombea ubunge na wengine watano ni wagombea wa udiwani.

Aidha Stenga alisema wamefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh 53,086,720 kwa kipindi cha miezi mitatu ikiwemo Sh 20,384, 000 zilizokuwa zimefanyiwa ubadhirifu kwenye mradi wa Moram wa Mtaa wa Bapumula Nyamhongoro, Manispaa ya Ilemela.

Kwamba Mwenyekiti wa mtaa huo, Marco Ncheye anadaiwa alifanya ubadhirifu kwa kuziweka kwenye akaunti yake kwa matumizi binafsi.

Stenga alisema uchunguzi ulibaini fedha hizo zilitokana na malipo ya Moram yayolifanywa na kampuni ya Steco Ltd na tayari mhusika amekiri kosa na kurejesha kiasi chote cha fedha hizo, nyingine ni Sh 24,377,300 zilizorejeshwa kwenye vyama vya ushirika na Sh 8,325,420 zilizorejeshwa kwenye akaunti maalumu ya Serikali iliyopo Benki Kuu.

Alisisitiza kuwa kwa kipindi hiki cha Julai hadi Septemba mwaka huu taasisi hiyo itajikita zaidi kuelimisha wananchi kuhusu makatazo ya rushwa kwenye uchaguzi na kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa atakamatwa na atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles