MSANII kutoka kundi la Weusi, Nickson Saimon (Niki wa Pili), mwanasiasa Chikulupi Kasaka, mjasiriamali Modesta Mahinga na Mbunge Steven Masele wameshiriki katika mdahalo wa vijana uliojadili mambo mbalimbali wanayotaka yafanyike katika uchaguzi mkuu wa Tanzania Oktoba, mwaka huu.
Mdahalo huo umeandaliwa na taasisi ya Tanzania Bora Initiative, ikiwa na lengo la kuweka msimamo kwa vijana katika uchaguzi utakaoweza kusaidia kushiriki kikamilifu katika hatua zote za uchaguzi na kufuatilia utekelezaji wa yaliyokusudiwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa TBI, Abella Bateyunga, alisema hatua hiyo itawezesha vijana wanaolenga kugombea nafasi mbalimbali waelewe nia na matarajio yao watakapopata nafasi ya kuongoza.
Mdahalo huo uliambatana na uzinduzi wa kampeni ya njia ya mitandao ya habari ijulikanayo kama ‘Uchaguzi Tanzania 2015 kura yetu’, iliyozinduliwa na balozi wa zamani wa Marekani, Mark Green, ambaye alisema vijana wana uwezo mkubwa wa kuongoza na kuelimisha jamii.