24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WASANII WA KIKE MCHANGO WENU KWENYE JAMII UMEONEKANA

wasanii-wa-kike

NA CHRISTOPHER MSEKENA

IMEKUWA tofauti na mawazo ya watu wengi waliokuwa wamekatishwa tamaa na mwenendo wa wasanii wa kike kwenye tasnia ya filamu. Mwenendo wa tabia chafu zisizofaa kuigwa na jamii ilhali wao ni kioo chao.

Chama cha Wanawake wa Tasnia ya Filamu Tanzania kimeanza vizuri kuibadili taswira hiyo mbaya ya wasanii mbele ya jamii. Kuanzia kwenye masuala ya kuingia kwenye mapenzi ya ndoa mpaka katika yale mambo yanayogusa afya zetu.

Tunaona chama hiki kilivyokuwa na umoja katika matukio ya misiba na yale ya furaha. Kwenye ndoa ya Shamsa Ford ilidhihirika kuwa umoja huo una nguvu na umekuja kwa ajili ya kurudisha heshima ya msanii wa kike.

Hivi sasa wasanii hao wa kike wameingia mpaka kwenye maisha ya mashabiki wao, wanagusa mambo muhimu ya kutetea uhai wa jamii. Nilifurahi kusikia wasanii hao wakihamasisha watu kuchangia damu.

Wiki hii walifanya hivyo kwenye Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam na nguvu yao iliwavuta watu wengine wengi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania wengi wanaopoteza uhai kwa kupungukiwa damu.

Linaweza kuonekana ni tukio dogo, lakini kwa watu waliokumbwa na majanga yanayohitaji damu watakuwa wameelewa ukubwa wa jambo la wasanii hawa wa kike kuchangia damu.

Wasanii hao pia hawakuishia hapo, ndani ya wiki hii walitembelea kituo cha kulea watoto yatima kilichopo Bunju B, jijini. Walitokwa na machozi baada ya kushuhudia mazingira hatarishi wanayokaa wale watoto.

Walitoa msaada wenye thamani ya Sh milioni 2 kwa mlezi wa kituo hicho, Sifa John. Huu ndio utu, huku ndiko kushukuru kwenyewe ambako kila binadamu inatakiwa afanye mara kwa mara.

Mashabiki wenye uwezo mkubwa wapo, ila hawafanyi hivyo. Nadhani baada ya wasanii hawa wa kike kufanya matukio haya mawili makubwa wanaweza kuwa wameihamasisha sehemu kubwa ya jamii kusaidia watu wenye uhitaji.

Ningefurahi makundi mengine ya wasanii yafuate nyayo za Chama cha Wanawake wa Tasnia ya Filamu Tanzania.

Hiki ni kipindi cha kurudisha fadhila kwa mashabiki. Wasanii wa kiume wa filamu msilipuuze suala hili, hali kadhalika wasanii wa muziki ambao mwaka huu umekuwa na mafanikio makubwa kwao,  gawaneni faida na mashabiki wenu wanaoishi kwenye mazingira magumu na wenye uhitaji kama huo wa damu nk.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles