KIPINDUPINDU CHATUA MAKAO MAKUU YA NCHI

0
729

kipindupindu

Na RAMADHAN HASSAN- DODOMA

WATU wawili wamefariki dunia kwa kuumwa ugonjwa wa kipindupindu huku watu wanane wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Dodoma kutokana na kuugua ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Christina Mndeme, alisema watu hao walifariki wiki iliyopita.

“Tunatakiwa tuzingatie kanuni za usafi kwani wilaya yetu imekumbwa na tatizo la ugonjwa wa kipindupindu mpaka sasa wameshafariki watu wawili huku wengine wanane wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakiugua ugonjwa huo,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alisema ameanzisha kampeni maalumu iliyopewa jina la ondoa kipindupindu lengo likiwa ni kuutokomeza ugonjwa huo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi jinsi ya kujikinga.

“Niwaombe wananchi wahakikishe chakula tunachokula kinakuwa safi, kuacha kutupa taka ovyo, mji unakuwa safi na watu wote wanaouza chakula wahakikishe wanakiuza katika mazingira ambayo ni safi pamoja na kunawa mikono kabla ya kula na wakati wa kuandaa chakula,” alisema.

Mndeme aliwataka maofisa afya wa kata kutoa elimu kwa wananchi kuzingatia kanuni za usafi ili kujiepusha kuupata ugonjwa huo.

Pia aliwataka kutoa taarifa sehemu husika pale wanapoona kuna mgonjwa ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa na kuliweka eneo husika katika mazingira ambayo hayatakuwa rahisi kuwaambukiza wengine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here