27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaofanya miamala ya simu, benki kubanwa

Na Mwandishi wetu

-Dar es Salaam

KANUNI mpya za kudhibiti utakatishaji fedha, zinatarajiwa kubana zaidi wanaofanya miamala kwa njia za kielektroniki ikiwamo benki na simu za mkononi.

Kwa mujibu wa kanuni hizo zilizosainiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Mei 7, mwaka huu na kuchapishwa kwa umma Mei 24, zinataka taarifa za mtu anayefanya muamala wa fedha zenye thamani ya Dola za Marekani 10,000 (zaidi ya Sh mil. 20) au zaidi, kutoa taarifa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU).

Kanuni hizo pia zinabana wanaochezesha michezo ya kubahatisha kwa njia mbalimbali ambao nao wanatakiwa kutoa taarifa zao FIU.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, kiasi hicho kinachotakiwa kutolewa taarifa ni kile kilichofika thamani hiyo ya fedha kwa muamala uliofanyika kwa wakati mmoja.

Katika kanuni hizo, uhamishaji fedha umetafsiriwa kuwa unajumuisha “shughuli yoyote ya fedha inayohusisha amana, utoaji, kubadilisha, malipo au kupokea fedha kwa shilingi za Tanzania au sarafu yoyote ya kigeni.”

Kanuni ya tano inasema, “mtu anayepaswa kutoa taarifa, atapaswa kutoa taarifa zifuatazo katika Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) (a) ubadilishaji wa fedha zinazohusisha shilingi za Tanzania au sarafu yoyote ya kigeni ambayo thamani yake ni sawa na dola 10,000 za Marekani au zaidi kwa mara moja.  

 “(b) Kuhamisha fedha kwa mtandao, unaohusisha shilingi za Tanzania au sarafu yoyote ya kigeni sawa na Dola 1,000 za Marekani au zaidi kwa mkupuo.

“(4) Katika kutambua thamani ya fedha za kigeni sawa na Dola za Marekani 10,000 kwa madhumuni ya taarifa ya fedha au dola 1,000 kwa lengo la kutoa taarifa za uhamisho wa fedha za kwa njia ya kielektroniki, muhusika anatakiwa kutumia viwango vilivyowekwa na Benki Kuu ya Tanzania vinavyotumika kwa wakati huo.”

Akizungumzia kanuni hizo, Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ben Mwaipaja, alisema; “kanuni zinasema mtu yeyote anayefanya muhamala wa fedha kwa njia ya mtandao ama anayesafirisha fedha kwa njia ya mtandao, atoe taarifa kwamba ‘nataka kusafirisha kiasi fulani kwa sababu fulani’.

“Kama unatuma fedha Japan kwa ajili ya kununua gari ama umepokea fedha kutoka nje, au unataka kumtumia mtu fedha zinazofika kiasi kilichotajwa kwenye kanuni, lazima utoe taarifa, hii ni kwa benki ama simu kwa sababu zote hizo ni njia za kielektroniki.

“Utaona dhumuni hapa ni kupambana na fedha haramu ama ndiyo maana ukienda kwenye mambo ya ‘cash’ kuna sheria inabana ipo kwenye viwanja vya ndege na mipaka, kwamba mtu anaweza kusafirisha kiasi gani cha fedha na azitolee taarifa. 

“Kwa hiyo inahusu watu wote kama ni nje ama ndani ndiyo maana inasema ndani au nje ya nchi,” alisema.

Alisema kanuni hizo zinabana hata wale wanaochezesha michezo ya kubahatisha ambao kama wanataka kutoa fedha kama zawadi ambazo zinafika kiwango kilichotajwa na kanuni wanatakiwa kutoa taarifa hizo.

“Kwa hiyo hizi kanuni zinakubana kama unataka kutumia njia za kielektroniki kutuma fedha ama kuchukua fedha huko,” alisema. 

Kanuni ya 11 inasema miamala miwili au zaidi ikifanywa ndani ya saa 24 na kufikia dola 10,000 za Marekani au zaidi, itachukuliwa kuwa ni muamala mmoja na hivyo itatakiwa kutolewa taarifa.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, ripoti za uhamisho wa fedha  kielektroniki au ripoti zote za fedha zitapelekwa FIU kabla ya kumalizika kwa siku tano za kazi baada ya siku ya uhamishaji.

“Zitapelekwa kwa njia ya kielektroniki au vinginevyo inavyohitajika na FIU, kila operesheni ya shughuli za michezo ya kubahatisha atahitajika kutoa ripoti ya fedha kwa fedha zilizopatikana kutoka kwa mteja,” inasema sehemu ya kanuni hizo.

Kanuni hizo pia zimeweka adhabu mbalimbali kwa watakaoshindwa kufuata matakwa yake ikiwa ni pamoja na faini na kifungo.

Zinasema FIU au mdhibiti akiridhika kwamba mtoa ripoti ameshindwa kutoa ripoti ya fedha au uhamisho wa fedha zilizohamishwa kielektroniki au kimataifa, kitengo hicho kinaweza kutoa onyo au tahadhari ya kurudia mwenendo uliosababisha kutotii.

Mtu atakayefanya kosa hilo pia anaweza kusimamishwa kufanya shughuli yake ama biashara, kutozwa faini isiyozidi Sh milioni tano na isiyopungua Sh milioni moja kwa siku ambayo kasoro ilijitokeza.

Adhabu nyingine ni kusimamisha leseni ya biashara au kusimamishwa au kuondolewa kutoka ofisi ya mfanyakazi ambaye alisababisha kasoro hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles