23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Majaliwa ahadi wakulima wa korosho kulipwa kabla ya Juni 30

Na MWANDISHI WETU

-LINDI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameahidi wakulima wa korosho mkoani hapa kuwa Serikali itawalipa fedha zao kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Mwaka huu wa fedha utaisha Juni 30 ambapo bajeti mpya ya Serikali kwa mwaka 2019/20 itaanza.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Lindi, kilichofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa.

Alisema wakulima ambao hawajalipwa au kumaliziwa malipo yao, baada ya Serikali kumaliza uhakiki majina yao yatapelekwa Benki ya Maendeleo Tanzania (TADB) kwa ajili ya malipo.

 “Wakulima wote wanaodai malipo yao ya korosho watalipwa katika mwaka huu wa fedha kwa kuwa ni haki yao na Serikali haitodhulumu haki ya mkulima yeyote,” alisema.

Kadhalika, alisisitiza suala la uboreshwaji wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma zikiwemo barabara ili ziweze kupitika kwa urahisi wakati wote.

Alisema uboreshwaji wa mbiundombinu pamoja na huduma nyingine za jamii ni jukumu la watendaji, hivyo wahakikishe wananchi wote wanahudumiwa bila ya kubaguliwa.

 “Kila aliyepewa jukumu ahakikishe analitekeleza ipasavyo. Watendaji hakikisheni mnawatumikia Watanzania wote vizuri, kusiwe na ubaguzi wa kisiasa, kidini na kikabila,” alisema.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema zoezi la malipo ya fedha za korosho zilizohakikiwa linaendelea.

Zambi alisema hadi Mei 31 kilo 51,990,999.97 zenye thamani ya Sh bilioni 171.570 ambazo ni sawa na asilimia 87.6 zimeshalipwa kwa wakulima husika.

Alisema kiasi cha Sh bilioni 23.404 bado hazijalipwa kwa wakulima wa korosho wa Mkoa wa Lindi. Korosho hizo zilihakikiwa kituo cha Mtwara.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wabunge wa mkoa wa Lindi, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na manispaa pamoja na wakuu wa idara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles