24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Vijana waishi kwa kutegemea fedha za Tasaf walizopewa wazazi wao

Na HARRIETH MANDARI

-GEITA

MBUNGE wa Bukombe mkoani Geita, Dotto Biteko, amesikitishwa na kitendo cha vijana kuishi kwa kutegemea fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambazo lengo lake ni kuwakwamua wazazi wao kwenye lindi la umasikini.

Kutokana na hali hiyo, Biteko ambaye pia ni Waziri wa Madini, aliwataka wazazi katika jimbo hilo kuhakikisha wanawapeleka watoto shule ili waweze kujenga misingi ya maisha yao. 

Biteko alisema hayo wakati akifuturisha waumini wa dini ya Kiislamu na wakazi wa jimbo lake.

“Hakuna kitu kinaniumiza kama ninapoona baadhi ya vijana wakiishi kwa kutegemea fedha za Tasaf ambazo wazazi wao  ambao wana umasikini uliokithiri wanasaidiwa na Serikali ili waweze kujikimu, jambo hili ni baya, ni lazima tubadilike na kuanza kuwaandaa watoto wetu sasa,” alisema.

Alisema ili Wilaya ya Bukombe iweze kuendelea miaka ijayo, ni lazima watoto waanze kuandaliwa ili wawe viongozi na raia wema na wenye weledi katika majukumu yao.

 “Bukombe ya sasa inaongozwa na sisi, lakini ya miaka ijayo ni lazima ije kuongozwa na watoto wetu ambao tunatakiwa kuwapika katika maadili mema sasa,” alisema.

Alisema ndoto na kiu yake ni kuona Wilaya ya Bukombe katika miaka ijayo inaongozwa na viongozi vijana kutoka wilayani hapo hapo.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kapeke, ambaye alikuwa mmoja wa waalikwa katika futari hiyo, aliwasisitiza Waislamu mkoani hapa kudumisha amani.

Alisema dini ya Kiislamu inasisitiza amani na inapotokea kiongozi yeyote wa Kiislamu akasababisha uvunjifu wa amani ni jambo lisilofaa.

 “Ningependa kuwakumbusha ndugu zangu kuwa tupendane wote bila kujali dini, Mwenyezi Mungu katika vitabu vitakatifu ametusisitiza kuishi kwa kupendana na amani,” alisema.

Aidha alimpongeza Biteko kwa utendaji wake mahiri chini ya Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli, hasa kwa upande wa uanzishwaji wa masoko ya dhahabu ambayo yamekuwa yakililiwa na wachimbaji nchini kwa miaka mingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles