24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Wananchi wa Chandama walilia maji

pg-3
Mhariri Msanifu wa Gazeti hili, Khamis Mkotya, akiangalia kisima kilichochimbwa katika Kijiji cha Chandama mwaka 2011 chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), kikiwa kimepigwa kufuli. Katikati ni mkazi wa kijiji hicho, Igwana Maulid na Yusuph Kijuu

 

Na Mwandishi Wetu, Chemba

WANANCHI wa Kijiji cha Chandama, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo, kutokana na kukabiliwa na tatizo la maji kwa miaka mingi.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi kwa nyakati tofauti na baadhi ya wakazi hao walipokuwa wakizungumza na MTANZANIA.

Walisema, wanashangaa kuona wanapata shida ya maji, wakati kuna visima viwili vilivyochimbwa kijijini hapo na vyenye maji mengi, lakini hawafaidiki navyo kutokana na ukosefu wa miundombinu.

Kutokana na shida hiyo, wananchi hao wamemwomba Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, afike kijijini hapo ili aweze kutatua kero hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Iddy Ijui, alisema kijiji hicho kinakabiliwa na shida kubwa ya maji, ambapo hivi sasa wanalazimika kununua pipa moja la maji kwa Sh 5,000.

“Kitendo cha kukosa maji kinatufanya tushindwe kufanya shughuli za maendeleo, kwani tunapoteza muda mwingi kutafuta maji.

“Hapa kijijini kuna visima viwili na vyote vina maji mengi, lakini vimefunikwa na magunia na kingine kimepigwa kufuli tangu 2011, sasa hatuelewi lengo lao lilikuwa ni kutuachia mashimo au kutoondolea kero ya maji,” alihoji.

Naye Igwana Maulidi, alisema katika kujitafutia huduma hiyo wananchi wa kijiji hicho wamechimba visima virefu vya kienyeji vinavyotumia kamba, kiasi cha kuhatarisha usalama wao.

“Visima viwili vimechimbwa lakini havitumiki, hatuwezi kupata maji kwa sababu havijafungwa mashine. Kibaya zaidi hakuna kiongozi anayezungumzia hatima ya hivi visima na jitihada za kumaliza hii kero, ndiyo maana tunaomba waziri wa maji aje hapa kijijini,” alisema.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mustafa Kidunka maarufu kwa jina la Munguji, alisema wananchi wa kijiji hicho ni kama yatima, kwani hakuna kiongozi anayehangaika kutatua kero zao.

“Watu wanashida ya maji hakuna anayejali, kilichimbwa kisima hapa na wajapani, kimepigwa kufuli hadi leo hakijafunguliwa. Mwaka jana tena halmashauri ilichimba kisima kingine na chenyewe kimefunikwa tu, kama ni hasara ya viongozi tumeipata,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Said Mwaliko (Chadema), maarufu kwa jina la Machapati, alikiri kuwapo kwa kero hiyo na kusema uongozi wa juu ndiyo kikwazo cha kumaliza kero hiyo.

“Shida ya maji ni kubwa, watu wanaugua matumbo, mimi nafuatilia ngazi ya juu nimekuwa nikimpigia simu mbunge, ananiambia linashughulikiwa lakini sioni chochote na mimi hapa kijijini nasumbuliwa sana kuhusu tatizo la maji.

“Tukikaa kwenye vikao vya WDC (kamati ya maendeleo ya kata) diwani anasema suala hili linashughulikiwa mara anasema hela zimetengwa lakini ni muda mrefu sasa hatuoni chochote na wananchi wanaendelea kupata shida,” alisema

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chandama, Titus Sindamwaka (CCM), alipotafutwa kuzungumzia kero hiyo aliwataka wananchi hao kuwa na subira, kwani kuanzia mwezi ujao tatizo hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi.

“Tumechimba visima viwili kimoja kipo Chandama na kingine kipo Mapango, tunasubiri bajeti ya Novemba 4, mwaka huu Baraza la Madiwani litakapokutana tuone tunakiasi gani tuanze kufunga miundombinu,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu kisima kimoja kupigwa kufuli kwa muda mrefu, Sindamwaka alikiri kisima hicho kuchimbwa 2011 na kueleza kuwa hakiwezi kufunguliwa, kwani hakijakabidhiwa rasmi katika Serikali ya Kijiji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles