
Na Amon Mtega, Songea
IDADI ya wakazi wa Kijiji cha Litapwasi Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma waliolazwa hospitalini wakidaiwa kunywa togwa yenye sumu imeongezeka kutoka 246 kufikia 325.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela, alisema jana wanakijiji hao wamelazwa katika Hospitali ya Peramiho na zahanati ya Lyangweni iliyopo kijijini hapo.
Alisema kutokana na tukio hilo jeshi la polisi linawashikilia watuhumiwa kadhaa huku baadhi ya wagonjwa wakiruhusiwa kurudi makwao baada ya afya zao kuimarika.
Kamanda alisema tukio hilo lilitokea Septemba 28 mchana katika sherehe ya Kipaimara ya mtoto Dickson Nungu (14) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Litapwasi.
Alisema polisi wanaendelea kufuatilia tukio hilo na wamekwisha kuchukua sampuli ya mabaki ya vyakula na togwa ambavyo vimepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali Dar es Salaam kwa uchunguzi.
Kamanda Msikhela alisema jeshi lake linawashikilia watu watano kwa mahojiano akiwamo mwandaaji wa sherehe hiyo.
Aliwataja watu wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Enesi Nungu (47) mkazi wa kijiji hicho ambaye ndiye mwandaaji wa sherehe hiyo.
Wengine ni Benidict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki Masoud (65) na John Kaulangudidi Mapunda, wote wakazi wa kijiji hicho.
Baadhi ya majeruhi waliolazwa katika Hospital ya Misheni ya Peramiho walisema walipatwa na masahibu hayo baada ya kunywa togwa iliyoandaliwa katika sherehe ya kipaimara ya mtoto wa mwanakijiji mwenzao.