28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Kwa hesabu hizi, Katiba Mpya shakani

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NA MWANDISHI WETU, DODOMA

RASIMU ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba ipo shakani kuweza kupitishwa bungeni, MTANZANIA limebaini.

Kutokana na sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, ili Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa, inahitajika kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka kila upande wa Muungano.

Idadi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ni 629 ambapo kati ya hao wanaotoka Tanzania Bara ni 419 na Zanzibar 210.

Hali inaonyesha kuwa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa itakwama kupitishwa kutokana na kukosekana theluthi mbili ya upande wa Zanzibar ambayo ni sawa na wajumbe 140 watakaopiga kura za ndiyo.

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Ukawa, Ismail Jussa, akizungumza na MTANZANIA alisema ili kuikwamisha rasimu hiyo kwa kukosekana theluthi mbili ya Zanzibar zinatakiwa kura 71 za hapana.

“Miongoni mwa wajumbe 210 wa Bunge la Katiba wanaotoka upande wa Zanzibar, wawakilishi wa CUF ni 33, wabunge 25, wabunge wa Chadema 4 na wana Ukawa 5 kutoka Zanzibar, miongoni mwa wajumbe 67 wa umoja huo waliotoka nje ya Bunge hilo.

“Mbali na hilo pia kuna 7 waliopiga kura za wazi za hapana jana, kuna wajumbe wawili ambao kwa hakika huenda wasipige kura ambao ni Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman Masoud na mjumbe Abdallah Abbas ambao kwa ujumla wao wanafikia 76,” alisema Jussa kupitia taarifa yake.

Kwa kuwa kukosekana theluthi mbili Zanzibar inatakiwa zaidi ya wajumbe 70 kati ya 210 kupiga kura ya hapana, hivyo kama hesabu hizo zitabaki kama zilivyo, kwa lugha rahisi ni kwamba Rasimu ya Katiba inayopendekezwa haitopita.

Mbali na takwimu hizo, kuna kura 28 zilizopigwa kwa siri ambazo huenda kati yake kuna baadhi ya wajumbe walipiga kura za hapana.

Pia wapo baadhi ya wajumbe waliotajwa kwamba wameorodheshwa watapiga kura wakiwa nje ya Bunge Maalumu ambapo hata ikichukulia zote zitakuwa za ndiyo, bado haziwezi kubadilisha msimamo huo wa kitakwimu uliopo wa kukosekana kwa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar.

SITTA NA MATUMAINI

Hofu hiyo ilimfanya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta, jana kuwaeleza wajumbe kuwa kura za kupata rasimu ya Katiba iliyopendekezwa zitapatikana.

“Inshallah, mambo yanakwenda vizuri, dua la kuku halimpati mwewe,” alisema.

MAPOKEZI YA KISHUJAA

Wakati hayo yakiendelea taarifa kutoka Zanzibar zinaeleza kuwa wajumbe wa Bunge hilo waliopiga kura za hapana wanatajiwa kupokewa kishujaa kwa mapokezi maalumu.

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa kamati inayoratibu mapokezi hayo inaundwa na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano pamoja na baadhi ya vyama vya siasa visiwani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles