32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mchuano mkali theluthi mbili Katiba Mpya

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar, Ali Juma Khatib, akipiga kura ya ya siri kwa sura 10 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka Zanzibar, Ali Juma Khatib, akipiga kura ya ya siri kwa sura 10 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

MCHUANO mkali umeibuka bungeni jana wakati wa upigaji kura wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, ambapo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba  kutoka Zanzibar walipiga kura ya HAPANA

Upigaji kura ulianza jana saa 9 alasiri kwa wajumbe kupiga kura katika sura 10 na ibara 157 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Hatua hiyo ilitawaliwa na wajumbe wengi kutoka Zanzibar kupiga kura ya Hapana huku wengine wakipiga kura ya siri.

Pia wapo waliopiga kura ya Ndiyo kwa baadhi ya ibara zilizopendekezwa.

Aliyekuwa wa kwanza kupiga kura kwa kuitwa jina na kusema anapiga kura ya wazi ni Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliyefuatiwa na Makamu Mwenyekiti wake Samia Suluhu Hassan ambao wote walipiga kura ya Ndiyo.

Baada ya viongozi hao wa Bunge waliofuatia kupiga kura ni wajumbe kutoka upande wa Tanzania Bara wakiongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda huku wengi wao wakipiga kura ya Ndiyo.

Hata hivyo, hali ya upepo ilibadilika hasa wakati wa upigaji kwa wajumbe kutoka Zanzibar ambapo hadi tunakwenda mtamboni, saba walipiga kura ya hapana, kura za siri 30 na ndiyo 75.

Wajumbe wote kutoka Zanzibar ni 210, na hadi kura zinapigwa waliokuwapo bungeni walikuwa 142. Hili kuunga mkono Rasimu ya Katiba inayopendekezwa inahitajika kupata theluthi mbili ya kura ya ndiyo kwa wajumbe 140.

Wakati wajumbe wengi kutoka Zanzibar wakipiga kura za siri, hali ilikuwa tofauti kwa wajumbe wa Bara ambapo wengi walipiga kura za ndiyo na watano wakipiga kura za siri.

Kabla ya kuanza upigaji kura, Sitta alitangaza idadi ya wajumbe ambapo alisema waliokuwa ukumbini ni 142 kutoka Zanzibar na 295 kutoka Bara.

Kutokana na hali hiyo, alisema ili kupata theluthi mbili kwa upande wa Bara ilikuwa inahitaji wajumbe 280 na Zanzibar wajumbe 140 kuweza kupitisha sura 10 na ibara 157 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Idadi ya wajumbe wote wa Bunge hilo ni 629, kati ya hao kutokana Bara ni 419 na Wazanzibari ni 210. Idadi iliyopo ni 295 kwa Tanzania Bara na 142 kwa Zanzibar.

Kazi ya upigaji kura iliendelea hadi tunakwenda mtamboni ambapo

Sitta na nyaraka za kanisa

Awali Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Sitta, alisema baadhi ya nyaraka zinazotolewa makanisani hazina utukufu wowote.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi wasisikilize matamko hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na anavyotaka Mungu.

Sitta alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwatambulisha wageni waliotembelea Bunge wakiwamo viongozi wa dini.

“Kuweni makini sana kwa sababu siku hizi kuna nyaraka zinatolewa makanisani, lakini hazina utukufu wowote wa Mungu,” alisema Sitta bila kufafanua.

Wakati huo huo, Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Donald Mtetemela, alisema yuko bungeni kihalali kwa kuwa jina lake lilipendekezwa na kanisa lake.

Askofu Mtetemela alisema hayo jana alipokuwa akizungumzia kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyetoa ufafanuzi wa namna ya kuitambua Mahakama ya Kadhi.

“Uwapo wangu hapa siyo wa kuhongwa, mimi hapa sikuhongwa na mtu, nimekuja hapa baada ya kanisa langu kupendekeza jina langu kwa rais.

“Kwahiyo, hao wanaosema hawaridhwishi na uteuzi wangu, siyo CCT ninaowafahamu,” alisema Askofu Mtetemela.

Katika hatua nyingine, Bunge hilo limependekeza katika rasimu kwamba idadi ya wabunge wa Bunge la muungano wasizidi 390.

Taarifa hiyo ilitolewa na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uandishi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa akitoa ufafanuzi wa mapendekezo ya wajumbe wa Bunge hilo.

“Rasimu ya Warioba ilipendekeza wabunge 75 katika Bunge la Muungano. Idadi hii ni ndogo ukiiona kwa haraka, lakini ni kubwa kwa sababu pamoja na uwapo wa Bunge hilo, Tanzania Bara ingekuwa na Bunge lake na Zanzibar ingekuwa na Bunge lake.

“Katika rasimu yetu mwanzoni tulipendekeza ukomo wa wabunge wawe ni 360, lakini baada ya kuangalia mabunge ya nchi nyingine, tumeona kuna haja ya kuwa na wabunge wasiozidi 390 na kama kuna rais atakuja na kutaka wabunge zaidi ya hapo, atalazimika kuwauliza wananchi.

“Tumependekeza idadi hii baada ya kuangalia ukubwa wa nchi, idadi ya Watanzania waliopo, kasi ya ongezeko la watu, gharama za kuendesha Bunge na mabadiliko ya teknolojia,” alisema Dk. Mwakyembe.

Habari hii imeandaliwa na Maregesi Paul (Dodoma), Shabani Matutu, Maneno Selanyika, Nora Damian na Jonas Mushi (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles