26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Waliofutiwa mitihani kurudia leo

LEONARD MANG’OHA (DAR ES SALAAM) Na RAMADHAN HASSAN(DODOMA)

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk. Charles Msonde, amesema maandalizi ya mtihani wa marudio katika shule zote za msingi za Halmashauri ya Chemba, mkoani Dodoma pamoja na halmashauri nyingine sita unaotarajiwa kufanyika leo, yamekamilika.

Shule nyingine zinazotarajiwa kurudia mtihani huo leo ni pamoja na Hazina na New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za jijini Dar es Salam.

Nyingine ni Alliance, New Alliance, Kisiwani za jijini Mwanza na Kondoa Integrity iliyopo Kondoa, Mkoa wa Dodoma.

Marudio ya mtihani huo yanatokana na uamuzi wa Necta kuzifutia matokeo ya mitihani iliyofanyika Septemba 5 na 6 mwaka huu baada ya kubainika kuwa zilifanya udanganyifu katika mitihani hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Msonde alisema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na mitihani kufika katika kamati za mitihani za mikoa na halmashauri za wilaya.

“Maandalizi ya mtihani wa marudio yameshakamilika, hapa tunapoongea, mtihani uko kwenye maeneo husika, kwenye kamati zetu za mitihani za mikoa na halmashauri.

“Watahiniwa wameshaandaliwa, vituo na wasimamizi wameshaandaliwa pia. Kwa hiyo ni matumaini ya baraza mtihani utafanyika kama ulivyopangwa.

“Kamati zetu za mitihani za mikoa na halmashauri zimeandaliwa na zimejipanga vizuri kama zilivyoweza kubaini matatizo haya, maana ndizo zilizobaini nadhani zimejipanga vizuri zaidi ili kuhakikisha mitihani inafanyika vizuri.

“Yeyote atakayekwenda kinyume cha kanuni za mtihani kwa namna yoyote ile, nadhani kamati zitamshughulikia hata kabla suala hilo halijaja kwangu,” alisema Dk. Msonde.

Aliwataka wanafunzi wanaorudia mtihani kutokuwa na hofu kwa sababu mtihani watakaofanya ni wa kawaida unaohitaji kutumia maarifa na stadi walizofundishwa na walimu wao.

“Kwa kifupi, waende wakiwa na amani, wafanye vizuri na mimi kama baraza nawatakia kila la kheri katika mitihani yao ili waifanye vizuri na Mungu atawasimamia wafaulu vizuri,” alisema Dk. Msonde.

Akitangaza kufuta mitihani kwa shule hizo Ocktoba 3, mwaka huu, Dk. Msonde alisema ilifutwa baada ya kubainika kuwa baadhi ya wasimamizi walivujisha mtihani huo wakishirikiana na waratibu wa elimu wa maeneo husika.

Katika Halmashauri ya Chemba, alisema uongozi wa idara ya elimu ulipanga kwa makusudi kufanya udanganyifu kupitia kwa waratibu elimu kata, walimu wakuu na wasimamizi ili kuhakikisha wanainua ufaulu wa halmashauri hiyo.

“Uongozi wa elimu Chemba uliunda kundi la whatsApp lililojulikana kwa jina la Elimu Chemba,  yakiwajumuisha waratibu wa elimu kata na baadhi ya walimu wakuu, kwa lengo la kurahisisha mawasiliano baina yao.

“Katika kutekeleza azma yao, mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifunguliwa kabla ya wakati na kusambazwa kupitia makundi ya WhatsApp waliyokuwa wameyaunda.

“Uongozi wa idara ya elimu wa Halmashauri ya Chemba, ulishiriki kutoa maelekezo yaliyohakikisha maswali yanafanywa na majibu yanawafikia watahiniwa kwa wakati na waratibu wa elimu kata, walitekeleza kazi ya usambazaji wa majibu kwa walimu wakuu na watahiniwa,” alisema Dk. Msonde alipokuwa akitangaza uamuzi huo.

Aliongeza kuwa, baraza hilo linaendelea kuchunguza uwepo wa udanganyifu katika vituo mbalimbali vya mitihani na halitasita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kujihusisha na udanganyifu wakati mitihani ilipokuwa ikifanyika.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, alisema maandalizi ya mtihani huo wilayani humo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kuongeza ulinzi katika vituo vya kufanyia mtihani ili kuhakikisha hakuna udanganyifu utakaojitokeza.

Alisema kwamba, juzi walifanya semina kwa walimu wote watakaosimamia mtihani huo na kuwaeleza namna bora ya kusimamia ili kuepuka udanganyifu wa aina yoyote.

“Maandalizi yamekamilika jana (juzi) tulikuwa na vikao na kamati ya mitihani ya wilaya na mkoa  na pia tulikuwa na semina kwa walimu tumeweka kila kitu sawa yale yaliyotokea mwanzo hatua zilichukuliwa na sasa tunachukua hatua kuhakikisha ulinzi unakuwa wa kutosha.

“Pia, kulikuwa na gari linazunguka kila kijiji kutangaza marudio ya mtihani, ni imani yangu wanafunzi wote wanaotakiwa kurudia mtihani watakwenda kufanya mtihani,”alisema.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chemba, Dk. Semistatus Mashimba, aliithibitishia MTANZANIA kukamilika kwa maandalizi hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles