22.4 C
Dar es Salaam
Friday, May 17, 2024

Contact us: [email protected]

OCD Kyerwa matatani kwa kusindikiza kahawa ya magendo

Na MWANDISHI WETU-KAGERA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi awachukulie hatua askari polisi wote wa wilaya ya Kyerwa wanaotuhumiwa kusindikiza kahawa ya magendo inayouzwa nchi jirani akiwemo Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Justin Joseph.

Alitoa agizo hilo jana baada ya kukagua kiwanda cha kukoboa kahawa cha Nkwenda wilayani Kyerwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi mkoani Kagera. Katika ziara hiyo Waziri Mkuu ameandamana na Mkewe, Mama Mary Majaliwa.

“Askari polisi wa wilaya ya Kyerwa pamoja na OCD wao wanatuhumiwa kusindikiza kahawa inayosafirishwa kwa njia ya magendo kwenda nchi jirani kupitia njia mbalimbali zisizo rasmi zikiwemo za Kumisongo, Kashaijo na Omukatoma,”alisema.

Waziri Mkuu alisema ni jambo la hatari kama askari Polisi wanasindikiza kahawa inayouzwa kwa magendo, hivyo akaagiza jambo hilo lidhibitiwe haraka.

Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu alisema kuanzia msimu ujao wa kahawa, minada yote ya kahawa inayozalishwa mkoani Kagera itafanyika ndani ya mkoa huo badala ya kufanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Alisema minada yote ya kahawa ikifanyika mkoani Kagera itawawezesha wakulima kulipwa fedha zao kwa muda mfupi na pia itapunguza makato  yasiyokuwa ya lazima ambayo ni kero kwa wakulima.

“Wanunuzi watafuata kahawa ilipo, utaratibu huu utawawezesha wakulima kulipwa fedha zake kwa wakati. Mnada ukifanyika katika maeneo ya uzalishaji utamuwezesha mkulima kujua bei, tofauti na unavyofanyika Moshi kwani ni rahisi mkulima kuibiwa,”alisema.

Aidha, kiongozi huyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Serikali yao ambayo imedhamiria kuwaletea maendeleo na kwamba itahakikisha kila mmoja anapata haki yake wakiwemo wakulima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles