25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

Auawa kwa risasi katika vurugu na polisi

Na IBRAHIM YASSIN-ILEJE

MWANAMKE aliyejulikana kwa jina la Mtineghe Naswila anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45, mkazi wa Kijiji cha Isheta, amepigwa risasi kifuani na kupoteza uhai.

Mwanamke huyo alidaiwa kuungana na wananchi wengine kufanya vurugu zilizosababishwa na kikundi cha waganga wa kienyeji (lambalamba) kinachopiga ramli chonganishi.

Akizungumza baada ya tukio hilo, mkazi wa kijiji hicho ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema baadhi ya watu waliwaita waganga hao ili wapige ramli ya kuwabaini wachawi waliopigwa marufuku na Serikali.

Alisema baada ya Serikali kukataza vitendo hivyo licha ya watu kukaidi na kuendelea kuwaita waganga hao, jana ilitokea vurugu wakiwapiga mawe askari polisi na kusababisha mmoja kuuawa kwa risasi ya moto kifuani.

Alisema katika wilaya hiyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiamini ushirikina ambapo wanalazimika kuwaita waganga wa kienyeji ili kueleza shida zao wakidhani wanaweza kupatiwa ufumbuzi wa matatizo yao hali ambayo imezua tafrani.

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Mathias Nyange, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza sababu ya polisi kutumia risasi ya moto.

“Hali hiyo ilijitokeza baada ya wananchi kuwafanyia vurugu polisi kuwarushia mawe na kushambulia gari la polisi, baada ya mabomu ya machozi kuisha wakatumia njia mbadala,” alisema.

Alisema wakati vurugu zikiendelea mwanamke huyo alimvuta askari mmoja na kutaka kumvutia kwa wananchi ili asulubiwe ndipo akapatwa na kadhia hiyo ya kupatwa na risasi kifuani na kufariki papo hapo.

Alisema zaidi ya vijana 60 walikamatwa kwa kuendesha vitendo hivyo vya uganga wakipiga ramli chonganishi na kwamba wanapopelekwa mahakamani wanapewa hukumu ndogo ya mwezi mmoja ambapo wakitoka wamekuwa wakiendelea tena kufanya shughuli hizo.

Aliwataka wananchi kuheshimu maagizo ya serikali kwa kuwa kuendesha vitendo hivyo ni kinyume na taratibu.

Ikumbukwe kuwa wiki iliyopita mwanamke mmoja aliuawa kwa kuchinjwa shingo na wauaji wakaondoka na kichwa hali ya kuwa mwili ulizikwa bila kichwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles