Na WALTER MGULUCHUMA -KATAVI
MKAZI wa Kijiji cha Kasokola katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Nassor Omary, ameshambuliwa na Kiboko katika sehemu ya tumbo na mgongoni hadi utumbo wake kutoka nje.
Mwenyekiti wa Kijiji Hicho, Domic Fungameza alisema tukio hilo la kushambuliwa mtu huyo lilitokea juzi saa saba mchana katika eneo la Chuo cha VETA Mpanda .
Alieleza kuwa kabla ya tukio hilo mnyama huyo alijichanganya kwenye kundi la ng’ombe waliokuwa machungajini.
“Ndipo mchungaji aliyekuwa na mifugo hiyo alipokwenda kutoa taarifa kijijini hapo juu ya kiboko huyo kujichanganya na mifugo ambayo alikuwa akiichunga.
“Baada ya taarifa hizo kuwa zimefika kijijini hapo kundi kubwa la wanakijiji lilijikusanya na kwenda kwenye eneo hilo huku wakiwa na silaha za jadi huku wengi wao wakiwa na nia ya kwenda kumuua kiboko huyo ili wapate kitoweo,”alisema .
Mwenyekiti huyo alisema baada ya kufika kwenye eneo hilo walimkuta kiboko huyo akiwa bado kwenye kundi la ng’ombe ndipo walipoanza kumshambulia kwa kumpiga na mawe.
Alisema pamoja na mnyama huyo kukimbilia kichakani wanakijiji waliendelea kumrushia mawe na fimbo huku dhumuni lao kubwa likiwa ni kutaka kumuua ili wapate kitoweo.
Alisema baada ya kuona anazidi kushambuliwa mnyama huyo alitoka mbio kwenye kichaka kwa lengo la kuwashambulia wanakijiji hao waliokuwa na silaha za jadi hatua iliyowafanya wanakijiji hao wakimbie.
Wakati wakiwa wanakimbia mnyama huyo alimshambulia Omary sehemu za tumboni na pia alimjeruhi sehemu za mgongoni.
Pamoja na Omary kupiga mayowe ya kuomba msaada kwa wanakijiji wenzake hakuna aliweza kumpa msaada na badala yake waliendelea kukimbia hadi mnyama huyo alipoamua kutokomea kusikojulikana.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya muda kupita wanakijiji hao walirudi kwenye eneo hilo na kumkuta mwenzao akiwa amejeruhiwa vibaya hali iliyowalazimu kumkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Katavi kwa ajili ya matibabu ambapo amelazwa huku hali yake ikiwa mbaya.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Kulwa Sanane alisema kiboko huyo alikuwa hana nia ya kumshambulia mtu lakini alipata hasira baada ya kuona anazidi kushambuliwa .
Askari wa maliasili walifika eneo hilo huku wakiwa na silaha na walianza kumsaka kiboko huyo na walifanikiwa kumwona na kumpiga risasi hadi kufa.
Baada ya askari hao wa maliasili kumwua mnyama huyo, wananchi walifurika katika eneo hilo wakigombania kukata nyama ya kiboko huyo kwa ajili ya kitoweo.