DC awashukia wazazi kupotea kwa watoto

0
920

Na FERDINANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amewatupia lawama baadhi ya wazazi nchini kuwa ndio chanzo cha watoto wao kupotea na kumomonyoka kimaadili.

Akizungumza juzi wakati wa mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Tusiime, alisema baadhi ya wazazi wamekuwa hawawajibiki ipasavyo katika malezi ya watoto wao na kusababisha wengine kupotea.

Aliwataka wazazi kuwa waangalifu na watoto waliomaliza darasa la saba katika kipindi hiki ambacho wanasubiri kujiunga na kidato cha kwanza ili wasije kujiingiza katika makundi mabaya.

“Tumeisikia matukio ya kupotea kwa watoto yaliyotokea hivi karibuni kama wazazi tujiulize je, tunatimiza wajibu wetu ipasavyo? Je, tunatenga muda kuzungumza na watoto wetu?

“Na watoto wengine huamua tu kuondoka nyumbani baada ya kutokea ugomvi kati ya wazazi na walezi hivyo, tuwe makini kufuatilia malezi ya watoto wetu ili kuwajengea msingi mzuri kimaisha,” alisema Mjema.

Mkuu huyo wa wilaya pia aliwataka wazazi na walezi kuacha kutumia tamaduni za kizungu katika malezi ya watoto wao kwani zimesababisha vijana wengi kushindwa kujitambua.

“Kuna walezi wengine wameshajifanya wao wazungu, wanaacha watoto peke yao nyumbani halafu wao wanakwenda kulala hotelini, matokeo yake wengine wanabakwa na kulawitiwa halafu hawasemi.

“Wengine wameuacha uhusika wao na kujikuta wakiwa watumwa kwa watoto wao, jamani hauwi mshamba kwa kulinda utamaduni wako, sisi ni wabantu vitu vya kuiga vinatuharibia watoto wetu,” alisema.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tusiime, Philbert Simon, aliwataka wazazi kutenga muda wa kutosha wa kukaa na kuzungumza na watoto wao ili kujenga misingi ya urafiki na kuwawezesha kuwa wazi, kujiamini na uaminifu.

“Kwa bahati mbaya wazazi wengi tumekuwa tukiwategemea wasaidizi wa nyumbani kufanya kazi ya malezi ya watoto wetu.

“Tabia hii inasababisha kukosekana kwa misingi imara ya malezi na makuzi kwa watoto wetu, tukumbuke taifa bora na imara hujengwa kuanzia kwenye ngazi ya familia,” alisema Mwalimu Simon.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here