23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Walimu wachangishana kuwanunulia wanafunzi wenye ulemavu taulo za kike

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Baadhi ya walimu katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wanalazimika kuchangishana fedha kwa ajili ya kuwanunulia taulo za kike wanafunzi wenye ulemavu.

Hali hiyo inatokana na baadhi ya wanafunzi kushindwa kumudu kuzipata taulo hizo kwa kuwa wengine wanatoka kwenye familia duni.

Mosi Rashidi mwenye ulemavu wa macho akiandika kwa kutumia mashine ya kuchapa maandishi ya nukta nundu. Wanafunzi wenye ulemavu wa macho na uziwi katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko huishi hosteli na baadhi yao wana changamoto ya kushindwa kupata taulo za kike.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko, Sezaria Kiwango, amesema kuna uhitaji mkubwa wa taulo za kike na kuomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia wanafunzi hao.

“Kuna uhitaji mkubwa wa taulo za kike kwa sababu wanafunzi wengi wenye ulemavu wanatoka familia za kipato cha chini na wengine wanaishi hosteli, wakati mwingine inabidi kuchukua fedha zetu mfukoni kuwasaidia. Tunaomba kama kuna wadau watusaidie ili mabinti zetu wasikose masomo kwa sababu ya hedhi,” amesema Mwalimu Kiwango.

Kutokana na hali hiyo Jumuiya ya Maendeleo ya Wasioona Tanzania (TAB) imeishauri Serikali kutenga ruzuku ya taulo za kike ili kuwawezesha wasichana kusoma bila vikwazo na kutimiza ndoto zao.

Mwenyekiti wa TAB, Omary Itambu, amesema wanafunzi wengi wa kike wamekuwa wakikosa masomo kwa siku tatu hadi tano kila mwezi kutokana na kushinda kumudu kununua taulo za kike pindi wanapokuwa kwenye hedhi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Wasioona Tanzania (TAB), Omary Itambu.

“Tunapotembelea shule mbalimbali hasa zenye wanafunzi wenye ulemavu tumekuwa tukikutana na changamoto hii na kwa kuwa shule inapewa ruzuku ingeongezea kipengele cha kusaidia watoto wa kike waliofikia umri wa hedhi ili kuepuka kukatisha masomo yao. Wengi wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini hawawezi kumudu kuwanunulia watoto wao.

“Bila hedhi salama unaweza kuja kumsababishia binti baadaye akawa na matatizo mengine ya kiafya kwahiyo tuiombe Serikali kwa upekee ilione hili iongeze ruzuku shuleni ili taulo zipatikane kwa shule zote zenye watoto wenye ulemavu,” amesema Itambu.

Mmoja wa wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo na mwenye ulemavu wa macho, Ushindi Lwiva, ameomba wadau mbalimbali kujitokeza kuwasaidia mahitaji muhimu zikiwemo taulo za kike ili waweze kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles