Na Malima Lubasha-Musoma
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Musoma, imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu watatu kwa kosa la kumuua Tabu Makanya (58) kwa kumchinja na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Musiba Maregeba, Abeid Casimil na Ndaro Sumuni wote wakazi Kijiji cha Kwibara Kata ya Mugango Wilaya ya Musoma vijijini mkoani Mara, huku Wandwi Mugulu diwani wa Kata ya Mugango, akiachiwa huru.
Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Girson Mdeme wa hiyo baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa Jamuhuri.
Jaji Mdeme, alisema ametoa adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa kwa washtakiwa baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi saba pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani na upande wa mashtaka.
Awali washtakiwa hao walihukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza katika kesi namba 189/2013 ambayo hukumu yake ilitolewa Julai 14,2015.
Jaji Mdeme alisema, wakati washtakiwa wakisubiri kunyongwa baada ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, walikata rufaa ambayo ilisikilizwa na na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Agosti 16.
Washtakiwa hao walikuwa wakituhumiwa kumuua Tabu Makanya (58) mkazi wa Kijiji cha Kwibara Kata Mugango, ambapo Februali 21 mwaka 2013 majira ya saa 5.00 usiku walivamia nyumba ya mwanamke huyo kwa kubomoa mlango kwa jiwe kubwa marufu fatuma.
Ilidaiwa wakiwa na mapanga na tochi, baada ya kuingia ndani walitoa onyo kwa watoto wa Tabu na kuwata kukaa kimya bila kupiga kelele.
Baada ya kuwatisha watoto, walimvamia mwanamke huyo kisha kumchinja na kutenganisha kichwa na kiwiliwili na kukiweka ndani ya mfuko wa sandarusi na kuondoka nacho.
Ilidaiwa wakati watuhumiwa hao wakiwa katika harakati za kutoka eneo la tukio, wananchi walifanikiwa kumkamata mtuhuniwa mmoja akiwa na kichwa hicho.
Kuhusu diwani aliyekuwa amejumuishwa kwenye kesi hiyo, inadaiwa alikamata baada ya uchunguzi wa awali kuonesha kwamba yeye ndiye aliwatuma watu hao kumtafutia kichwa cha binadamu kwa makubaliano ya kuwapatia fedha.
Ilidaiwa kuwa, diwani huyo alitaka kichwa hicho ili kukitumia kishirikina kwenye masuala ya uvuvi wa samaki lakini baada ya jalada lake kupelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali, aliondolewa kwenye kesi hiyo.