23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyefukuzwa kazi kwa kufoji cheti, afoji barua na kufanya kazi kwa miaka nane

Na Mwandishi wetu-Sengerema

KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro, ameagiza kusakwa kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Boniventura Bwire, akidai alifukuzwa kazi mwaka 2012 baada ya kubainika ana cheti cha kufoji kisha akafoji barua ya Katibu Mkuu Tamisemi na kufanya kazi kwa miaka nane kwenye halmashauri tatu tofauti.

Dk Ndumbaro alitoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Boniface Magesa, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo chenye lengo la kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili na kuzitatua.

Alisema Bwire alikuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mpaka mwaka 2011 kabla ya kufukuzwa kazi mwaka 2012 na mwajiri wake baada ya kugundulika kuwa na Stashahada ya Juu ya Uhasibu ya kughushi.

Alisema mtumishi huyo alighushi barua za Katibu Mkuu Tamisemi na kufanikiwa kuhamia katika Halmashauri za Wilaya ya Ukerewe, Bariadi na hatimaye Sengerema.

“Kwa miaka nane Bwire amekuwa akifanya kazi serikalini akiwa sio mtumishi wa umma halali baada ya kufukuzwa kazi na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara na katika halmashauri zote alizohamia amekuwa akijitambulisha kama Ofisa Mapato na kufanya kazi hiyo na hatimaye kujilipa, hivyo kujipatia fedha kwa udanganyifu,”alisema  Dk Ndumbaro.

Alisema baada ya mtumishi huyo kuhamia Sengerema, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kutokana na umakini wake aliweza kubaini kuwa, mtumishi huyo anatumia cheti cha kidato cha nne ambacho si chake hivyo akamfukuza kazi.

Alisema mtumishi huyo baada ya kufukuzwa kazi aliwasilisha rufaa yake kimakosa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) badala ya Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndio mamlaka yake ya rufaa.

Alisema mambo yote aliyoyafanya Bwire tangia mwaka 2011 hadi sasa ni batili kwani si mtumishi wa umma halali baada ya kufukuzwa kazi, na hakuwahi kukata rufaa kwenye mamlaka stahiki.

Alisema kutokana na makosa yake kuwa ni ya jinai, suala lake liwasilishwe Polisi na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa uchunguzi na kulifikisha mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles