Wabongo Ukimwi hawauogopi, hata corona?

0
1313

Na MICHAEL MAURUS

DUNIA kwa sasa ipo katika kipindi kigumu mno kutokana na janga la virus vya corona, uliopiga hodi katika mataifa mbalimbali, yakiwamo yaliyoendelea kama Marekani, China, Italia na mengineyo.

Ugonjwa huo ambao kwa kitaalam unaitwa Covid-19, tayari umeshasababisha vifu lukuki duniani, huku kukiwamo na waathirika wengi katika mataifa mbalimbali.

Japo unasadikika kuanzia nchini China, lakini ndani ya miezi michache, tayari umeshasambaa katika mataifa lukuki, ikiwamo Tanzania.

Hadi kufikia Ijumaa, Tanzania ilikuwa na waathirika 147 wa virus vya ugonjwa huo, huku kukiwa na vifo vitano.

Kutokana na kubaini ukubwa wa janga hilo, Machi 18, mwaka huu, Serikali ilitangaza kusitisha shughuli zote za mikusanyiko ili kuepusha kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo unaosababisha vifo kwa haraka mno.

Katazo hilo lilikwenda sambamba na kufunga shule zote kuanzia za awali hadi za sekondari, lakini pia vyuo vyote nchini.

Hadi sasa, hakuna dalili ya serikali kutengua katazo hilo kwani inaonyesha hali si shwari kutokana na kasi ya maambukizi ya virus hivyo.

Sambamba na kuzuia mikusanyiko, serikali imekuwa ikihimiza Watanzania kujiweka mbali na hatari zinazoweza kuwasababishia maambukizi ya virus hivyo, ikiwamo kupeana mikono, kunawa maji yanayotiririka kwa kutumia sabuni mara kwa mara.

Pia, jamii imetakiwa kusafisha mikono kwa kutumia kitakasa mikono ‘sanitizer’, kufunika midomo na pua kwa kutumia barakoa (mask), kutosimama karibu na mtu unayeongea naye kuepusha kurushiwa mate yanayoweza kuambatana na virus vya corona.

Wataalam wa afya pia wamekuwa wakishauri jamii kutoshika shika vitu ovyo, kuepuka mikusanyiko, kutojenga mazoea ya kugusa usoni kabla ya kunawa, kuepuka safari zisizo za lazima na kutulia majumbani.

Wazazi wametakiwa kuwalinda watoto wao kwa kuwaelimisha juu ya ugonjwa huo, huku viongozi wa dini nao wakishauriwa kufanya hivyo kwa waumini wao.

Lakini pamoja na tishio la ugonjwa huo na kasi ya kuenea kwa maambukizi ya virus vyake hapa nchini, bado jamii ya Watanzania imeonekana kutoelewa somo.

Katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, watu wameendelea kukusanyika na kutopeana ‘distance’ (umbali) wanapoongea, kushika vitu ovyo, watoto zaidi ya watano kucheza pamoja iwe ni chandimu, rede, kupika pika na michezo mingineyo ya watoto.

Watu wanapokwenda madukani, bado wanashika madirisha ama mbao za meza bila kuwa na hofu yoyote, abiria katika daladala wanapopanda, wanagusa ovyo milango au madirisha na viti bila hofu yoyote.

Makondakta nao wanaongea ovyo tu mbele ya abiria huku midomo yao ikiwa wazi bila kujali kama kuna hatari ya virus vya corona.

Binafsi najiuliza ina maana Watanzania hatujaelewa tu ukubwa wa hili janga la corona? Kama tumeshindwa kuogopa Virusi vya Ukimwi, hata hivi vya corona vinavyoyatesa hata mataifa makubwa kama Marekani na Italia?

Hivi sisi Wabongo tumerogwa na nani kiasi cha kutoelewa ukubwa wa janga hili la corona? Hatumuoni Rais wetu Dk. John Magufuli anavyozungumza kwa hisia kuwataka wananchi kujikinga na ugonjwa huo? 

Hebu tubadilike, kila mmoja awe makini na hili suala la corona, hakuna cha urafiki wala undugu katika janga hili, tukifanya mchezo, tutapukutika kama kuku waliokumbwa na ugonjwa wa kideri (Newcastle Disease) na kuweka rekodi duniani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here