24.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 17, 2021

Tumia mbinu hii kumbaini mchumba anayeigiza tabia

Na CHRISTIAN BWAYA

UNAPOANZISHA uhusiano na mtu usiogope kuwa wewe. Mapenzi yasikufanye ukasahau wewe ni nani. Unajua kila mtu ana namna alivyo. Kuna vile unapenda kuwa. Kuna vile unavyoyatazama maisha. Sina neno sahihi lakini nazungumzia jumla ya mitazamo, imani, misimamo na mtindo wako wa maisha. Hapa nazungumzia misimamo yako ya kidini, vitu unavyovichukulia kuwa muhimu zaidi katika maisha vinavyoumba matamanio yako ya maisha. Lakini pia, ni pamoja na namna yako ya kuvaa, kuzungumza, aina ya marafiki uwapendao, burudani uzipendazo na mambo mengine kama hayo. Wakati mwingine misimamo yako inaonekana kwenye vile vitu usivyopenda kuvifanya. Kuna vitu huhitaji kuambiwa na mtu lakini unaamini sio sahihi. Ukiona mtu anavifanya kuna namna unakereka. Unajisikia vibaya. Mara nyingi vitu kama hivi ndivyo vinavyoamua nini cha kufanya, nini cha kuacha, nini cha kufanya unajisikia kujutia, aina ya watu usiotaka kuwa nao karibu, aina ya watu unaowachukulia kama adui, aina ya watu wanaokuvutia na vitu vinavyoamua uamuzi wako ya kila siku. Jumla ya haya yote ndio yanayotengeneza mfumo wako wa maisha. 

Katika makosa unayoweza kuyafanya unapoingia kwenye uhusiano na mtu ni kupuuza tofauti zenu za kimitazamo, kiimani na misimamo mingine ya kimaisha. Kihunzi cha kwanza kukivuka kama kijana ni kuweza kusimamia mfumo wa maisha yako unapoingia kwenye uhusiano na mtu. Najua nguvu ya mapenzi. Ukishapenda kuna uwezekano hisia za mapenzi ulizonanzo zikakupofusha usiuone ukweli. Unaamua kuvaa sura fulani kwa ajili ya kumfurahisha huyo uliyempenda. Unaikana imani yako, unaachana na misimamo yako, unabadili mfumo mzima wa maisha yako kwa sababu unaogopa ukisimamia kile unachokiamini utakataliwa. Woga wa kumkatisha tamaa mwenzako unakufanya uone bora kuigiza sura fulani kwa muda. Nikukumbushe tu kwamba mara nyingi badiliko hilo la muda lina gharama yake. Mambo unayoyaamini, mifumo ya maisha ni vitu vyenye mizizi mirefu kwenye maisha. Huwezi kuachana nayo kirahisi. Ukilazimisha kuyaacha kwa muda, kwa lengo la kumfurahisha mtu, yanaweza kukuletea matatizo mbele ya safari. Pamoja na uwezekano wa tabia yako kubadilika, kuna vitu katika maisha yetu havibadiliki. Unaweza kuvikana, unaweza usivipende, ukatamani kuvibadilisha, lakini haviondoki. Kuvibadilisha, wakati mwingine, ni sawa na kujaribu kujirefusha kimo chako, kubadili rangi ya ngozi yako, vitu ambavyo tunajua haviwezekani. 

Nafahamu vijana wengi wanaotumia nguvu nyingi kujaribu kuwa watu wengine. Kundi la kwanza, hujipandisha hadhi kufikia viwango vya wale wanaotamani kuwa nao. Hawa hulazimika kuigiza maisha yasiyo yao, ili kuwavutia wale wanaoamini wana hadhi kuliko wao. Hasara, kwa kawaida, huwa ni suala la muda. Huwezi kuigiza maisha ukiwa karibu na mwenzako. Lakini kundi la pili, ni wale wenye wasiwasi kuwa misimamo yao ya maisha itawafukuza wapenzi wao. Kwa hawa, suluhu ni ‘kujitelekeza’ kwa maana ya kupuuza misimamo na imani yao, kubadili mifumo yao ya maisha ili kuendana na misimamo ya wapenzi wao. Unapoona unalazimika kubadilika, kwa hakika, hiyo ni ishara kuwa unaingilia uhusiano usiokufaa. Tumia hicho kama kipimo cha uhusiano unaokufaa.

Kufikia hapa, swali tunalohitaji kulijibu, ni tunawezaje kumjua mtu anayeigiza tabia? Kwanza, ni muhimu kuzingatia kwamba mwanadamu kwa asili yake ni mtu wa maigizo. Tunaanza kuigiza mapema katika umri mdogo. Mgeni akija nyumbani tunajitahidi kuwa na sura inayomfaa mgeni. Hatulii, hatulalamiki, hatugombani. Maigizo haya yanayoendelea hata tunapokuwa watu wazima, yanatokana na ukweli kwamba kwa hulka yetu hatupendi kuhukumiwa. Tunaogopa kueleweka vibaya na kujenga picha itakayotufanya tudharaulike, tupoteze heshima na hata kukataliwa. Ukitaka kumwelewa mwanadamu, mwondolee hofu hiyo. Mahali pa kuanzia ni kujipa muda. Huna sababu ya kuharakisha mambo. Haraka haraka, wahenga walisema, haina baraka. Muda utakupa fursa ya kuwa karibu na mwenzako. Kadri unavyoweka karibu ndivyo unavyomwekea mazingira ya kukuamini afunguke bila yeye mwenyewe kujistukia. Siri hapa ni kutokumhukumu, kutokumshutumu na kutokumshambulia anapoonesha tofauti yoyote ya kimtazamo, kiimani au hata kitabia. Jenga ukaribu na mtu ukimpa uhuru wa kufikiri, kutenda na kuenenda vile anavyopenda. Unapofanya hivyo unamfanya ajisikie salama kufikiri na kutenda vile anavyotaka. Mara nyingi tunakosa fursa ya kuwafahamu watu kwa sababu tunaonesha mapema dalili za kutafuta ukamilifu ambao wakati mwingine sisi wenyewe hatunao. Tunakuwa wepesi kuhukumu, kuhamaki, kushangaa tunapobaini tabia fulani fulani tusizozipenda. Matokeo yake mtu anaficha makucha yake kwa hofu ya kushambuliwa, kuhukumiwa na kuachwa. 

Lakini pili na muhimu, epuka kuwa mtu anayetabirika katika hatua za mwanzo za uhusiano. Ingia kwenye uhusiano kama shushushu asiyejulikana anatafuta nini wakati huo huo ukiepuka misimamo yako kueleweka kirahisi. Kwa mfano, ikiwa unatafuta mwenzi mshika dini, huna sababu ya kuliweka hilo wazi mwanzoni mwa uhusiano wenu kupunguza uwezekano wa mwenzako kushawishika kupambana anaonekane ni mshika dini. Katika mazingira ambayo dini siku hizi zimeingiliwa na ‘wahuni’ wanaochukulia nyumba za ibada kama maeneo ya kuwapata washika dini, unaweza kumtafuta mshika dini, bila kuonesha waziwazi njaa yako ya kupata mshika dini. Hutakuwa na kazi kubwa ya kumbaini.

CHRISTIAN BWAYA – Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

12,054FansLike
2,941FollowersFollow
18,400SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Latest Articles