29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tuweke siasa pembeni, vyama vishirikiane kuikabili corona

Na FARAJA MASINDE

DUNIA bado iko kwenye kipindi kigumu cha kukabiliana na janga la virusi vya corona vilivyolipuka mwishoni mwa mwaka jana nchini China.

Jambo la kushtua zaidi ni kwamba hadi sasa karibu kila nchi zinakabiliwa na janga hili la virusi vya corona, pia maelfu ya raia wameendelea kupoteza maisha kutokana na virusi hivi hatari.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia juzi Ijumaa, idadi ya watu waliokuwa wameambikizwa duniani kote ilikuwa ni zaidi ya milioni mbili huku vifo vikifikia 135,163 huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwa wahanga wa janga hili baya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Hadi sasa, Tanzania imepoteza jumla ya raia wake watano kutokana na virusi hivyo huku idadi ya maambukizi ikifika 147.

Jambo la kupongezwa kwa serikali ikiongozwa na Rais Dk. John Magufuli, ni kwamba imeendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha janga hili linakabiliwa kikamilifu.

Tumeshuhudia kwa nyakati tofauti Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na hata Rais Dk. Magufuli wakitumia nafasi zao katika kuhakikisha kuwa janga hili linadhibitiwa kikamilifu.

Katika hilo, tayari Rais Dk. Magufuli mapema Alhamisi kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, alichapisha ujumbe akiwahimiza Watanzania kuliombea taifa kwa siku tatu ambazo zinafikia ukomo leo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa janga hili linaondoka.

Hakuna shaka kwamba Watanzania wengi wametekeleza mwongozi huu wa Rais ikiwa ni njia ya kulikabidhi taifa letu mikononi mwa Mwenyezi Mungu.

Katika ujumbe huo, Rais Magufuli aliandika: “Ndugu zangu Watanzania, kutokana na ugonjwa wa corona, nawaomba tutumie siku tatu za kuanzia tarehe 16-18 Aprili, 2020 (Ijumaa, Jumamosi na Jumapili) kumuomba Mwenyezi Mungu aliyemuweza wa yote atuepushe na janga la ugonjwa huu. Tusali kwa kila mmoja kwa imani yake, atatusikia.”

Ni bayana kwamba maombi pamoja na kutegemea Mwenyezi Mungu ni nguzo mumhimu inayoweza kuliponya taifa na janga hili hatari, hii inamaana kwamba ni jambo la kupongezwa kwa kiongozi wa nchi kuona umuhimu wa kumtanguliza Mungu mbele kama ambavyo imekuwa kauli mbiu yake mara kwa mara akiwaasa Watanzania kumtumainia Mungu.

Lakini wakati Serikali ikiwa kwenye mtihani huo mzito wa wa kuhakikisha kuwa taifa linavuka kwenye janga hili, kumekuwapo na baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini ambavyo wakati mwingine pamoja na kuwa na mawazo mazuri lakini vimekuwa vikisalia kuishi na fikra za upinzani wakati wote, jambo ambalo binafasi sioni kama lina afya kwa Tanzania yetu.

Kwa nyakati tofauti tumeshuhudia namna ambavyo vyama kama Chadema ambacho ni Chama Kikuu cha Upinzani nchini, Chama cha ACT Wazalendo, kupitia kwa viongozi wao wa ngazi mbalimbali wakitoa mawazo yao juu ya virusi hivi. 

Kila upande ukisema serikali ingefanya hivi, huku upande mwingine ukisema kwamba serikali ingefanya vile ili kuikabili corona na mawazo mengine kama hayo yakiwamo yale ya kuondoa ushuru kwenye bidhaa zinazotumika kutengeneza vitakasa mikono na sabuni.

Mfano Machi 31, mwaka huu, Chadema Kanda ya Pwani, iliitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye huduma za afya kwa wakati huu ikiwa ni pamoja kurahisisha upatikanaji wa vitakasa mikono (sanitizer).

Kauli hiyo ya Chadema, ilitolewa jana na Ofisa Habari wa Kanda hiyo, Grevas Lyenda, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Lyenda anasema Serikali inapaswa kutilia mkazo kuhusu ugonjwa huo.

“Kama taifa lazima tuwe ‘siriasi’ na huu ugonjwa kwani watu wanapoteza maisha kila siku na tumeshuhudia namna ambavyo majirani zetu mfano, Uganda na Kenya wanavyochukua hatua thabithi kuhakikisha kuwa watu hawatoki.

“Lakini hapa kwetu bado ni changamoto, kwani watu wanajaa kila mahala, ikiwamo kwenye vyombo vya usafiri na sokoni.

“Tunaiomba Serikali iipe uzito kweli kweli suala la corona, tunaona namna ambavyo idadi ya wagonjwa wanavyozidi kuongezeka.

“Tungependa mgonjwa huyu awe wa mwisho, tunaona Kenya wenzetu wanagawa vitakasa mikono bure na hata upatikanaji wake ni rahisi, lakini kwetu hapa huduma hii inazidi kuwa ghali kila kukicha,” anafafanua Lyenda.

Anaongeza: “Wito wetu ni kwamba hakuna kipindi Serikali inatakiwa kuwekeza kwenye masuala ya afya kama sasa. Kenya wameweza, wanagawa bure, sisi tunashindwa nini? Walau hata kuondoa tozo kwenye bidhaa zinazotumika kutengeneza vitakasa mikono.

“Hivyo, ni bora Serikali ikaona umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na kusaidia wazalishaji kupata vifungashio vya bei nafuu au hata bure ili kitakasa kinachouzwa Sh 10,000 kiuzwe hata Sh 1,000 na kile cha Sh 7,000 kiuzwe Sh 500 au hata kugawiwa bure kwa wananchi ili iweze kusaidia kupunguza maambukizi, hapo tutaonekana tuko ‘siriasi’.”

Ukija upande wa ACT Wazalendo, kupitia kwa Kiongozi Mkuu, Zitto Kabwe, kilieleza kuwa Serikali kupitia Waziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango, kupeleka bungeni taarifa ya utafiti wa madhara ya mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona nchini ili ijadiliwe na kutoa mapendekezo ya kibajeti kuhami uchumi wa nchi.

“Waziri wa Fedha na Uchumi apeleke bungeni  taarifa ya utafiti wa madhara ya mlipuko wa corona kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla na bunge lijadili kwa maslahi ya taifa,”  imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Zitto.

Hivyo basi, hayo ni baadhi tu ya mawazo ya viongozi wa vyama vya siasa hapa nchi ambayo mengine yanaweza kuwa na tija au yasiwe na tija, lakini changamoto inabaki ni moja tu kwamaba ni kwa namna gani yanaifikia serikali?

Vyama vya siasa lazima vitambue kuwa  licha ya kuwa upinzani, lakini mwishowe sisi sote ni watoto wa taifa moja hivyo, ni busara kama mawazo haya yenye sura ya kipinzani yangewasilishwa kwa mamlaka husika kama sehemu ya jitihada za kusaidia kutokomeza janga hili kuliko kusalia kuwa wapinzani kila siku.

Sababu iwapo vyama vya siasa licha ya kuwa upinzani vitaamua kuweka siasa hizi kando na kutoa mawazo ambayo yanamchango kwa serikali, basi vitakuwa vimelisaidia taifa na manufaa yatakuwa ni kwa Watanzania wote kuliko utaratibu huu wa sasa ambao kila mmoja anapaza sauti yake kwa upande wake bila kujali kuwa hili ni janga ambalo limetesa sehemu kubwa ya dunia.

Ni vyema mawazo haya mazuri yakawasilishwa kwenye mamlaka husika kwa njia za busara zaidi ili kuweza kuangalia ni kwa namna gani tutapata mwarobaini huu wa kuondokana na janga hili la corona.

Hivyo, katika kipindi hiki ambacho bado kun unafuu wa hali ya maambukizi hapa nchini ndicho kilikuwa muda sahihi kwa vyama vyote vyenye mawazo ambayo vinaamini ni sahihi kuipelekea serikali ili tujiepushe na yale yaliyowakuta wenzetu.

Tumeshuhudia mataifa mengine jirani kama Kenya, Uganda na hata Afrika Kusini ambako imesababisha mamlaka za nchi hizo kutumia nguvu kuhakikisha kuwa raia wake wanasalia majumbani ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

Uamuzi huo ulitazamwa kama tatizo ndani ya tatizo, hatua ambayo inaweza kuongeza hatari zaidi ya mlipuko wa virusi hivi.

Kwa nguvu kubwa ambayo inachukuliwa na mamlaka husika, kuwatawanya kwa kuwapiga baadhi ya wale wanaokaidi agizo hilo la serikali ni sawa na kuzalisha chuki nyingine miongoni mwa raia hao na serikali.

Hivyo, badala ya raia kuanza kupambana na virusi vya corona katika kuhakikisha kuwa wanajikinga, badala yake wataanza kupambana na serikali hatua ambayo inaweza ikaibua hatari kubwa kwani mapambano yataelekezwa serikalini na kusahau kuchukua hatua muhimu ya kujikinga na virusi vyenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles