Vyama vya upinzani vilipaswa kuwa mfano

0
442

TUNAPOJADILI maendeleo yeyote katika nchi yetu, huwezi kuviacha vyama vya siasa na viongozi wake waliotokana na vyama hivyo.

Tunasema hivyo kwa sababu, kwanza kwa mfumo uliopo wawakilishi wa wananchi wanatokana na vyama vya siasa hivyo kupitia viongozi hao waliotokana na vyama vya siasa  wananchi hupata fursa ya kuwakilishwa  kuanzia kwenye mitaa, vitongoji, vijiji, bungeni na hata katika baadhi ya nafasi  serikalini.

Kwa mantiki hiyo, unaweza kuona jukumu zito ambalo vyama vya siasa vimebeba, lakini pamoja na jukumu hilo zito kwa vyama vya siasa, tunachelea kusema iwapo vinatambua wananchi ndio ‘mabosi’ zao.

Hakuna asiyefahamu kwamba bosi mara zote furaha yake ni kuona kazi aliyokutuma umeifanikisha sawasawa na imeleta faida, na pale inapokuwa tofauti njia ni moja tu kumtafuta mwingine ambaye atatimiza  lengo lake.

Ndivyo ilivyo kwa upande wa vyama vya siasa, wananchi ambao wanaona mahitaji na matamanio yao hayatimizwi na chama ‘A’ basi huamia chama ‘B’ au ‘C’.

Hapa nchini kwa muda mrefu kumekuwa na chama kimoja kinachotawala na baadhi kwa sababu zao baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, waligeukia vyama vya upinzani.

Waliogeukia vyama vya upinzani wengi wao ukiwauliza watakwambia matumaini yao ni kupata yale ambayo walikuwa hawayapati ndani ya chama tawala hususani katika eneo la haki, demokrasia, rushwa, ufisadi na mambo mengine kadha kadha yanayokwaza maendeleo ya wananchi.

Kwa bahati mbaya sana, vyama vya upinzani ambavyo vilipaswa kuwa mfano kwa yale wanayoyakosoa chama tawala, kadiri siku zinavyozidi kwenda baadhi ya viongozi wake na wanachama wao wamekuwa wakitenda ama kuamua mambo ambayo yanazua maswali.

Kwa mfano ndani ya chama kikuu cha upinzani cha Chadema pamoja na mara kadhaa kuonekana kuandamwa kukwamishwa na washindani wake, lakini yapo matukio yanayotekelezwa na chama hicho ambayo yanaweza kuonekana kuwa ni madogo na yasiyo na athari.

Miongoni mwa matukio hayo ni namna inavyoshughulika na wanachama wake ambao wanaonyesha nia ya kufanya mabadiliko ya kidemokrasia ndani ya hicho.

Ieleweke nia yetu si kutaka Chadema ikubali kuhujumiwa kwa njia ya demokrasia hapana bali kuitaka kuangalia namna ya kushughulikia masuala yake kwa njia zile zile inazohubiri.

Kwa mfano namna Chadema ilivyoshughulika na tukio la sasa la Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kuanguka kwenye nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Pwani imezua maswali.

Hata kama washindani wake walilenga kumchimba Mwenyekiti wake wa sasa, Freeman Mbowe, mazingira ya Sumaye kuanguka katika uchaguzi huo ndiyo yanayozua maswali ambayo yasipojibiwa sawasawa yanaweza kuwa na athari.

Wengi sasa wanaweza kuhisi kwamba ndani ya chama hicho pamoja na kuhubiri demokrasia hakuna demokrasia.

Zaidi wanaweza kuona yale mambo ambayo hawakuyataka ndani ya chama tawala yapo pia upinzani kama hili la siasa za kushughulikiana.

Sisi tunaona pamoja na kwamba Chadema ya Mbowe inaweza kuwa katika mapambano na mawakala wa washindani wao, lakini bado ilipaswa kushughulikia mambo yake kwa namna ambayo chama hicho kitaonekana kinazingatia demokrasia na kujitofautisha kwa maneno na matendo na vyama ambavyo wao wamekuwa wa kwanza kuvinyooshea vidole.
MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here