24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Mkuu ataka wahitimu Chuo cha Mahakama kutumikia jamii

Na Mwandishi wetu

– Lushoto

JAJI Mkuu Profesa Ibrahim Juma, amewataka wahitimu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kutumia silaha ya elimu ya sheria kuitumikia jamii kikamilifu na kuinoa kila wakati ili iwe na nguvu ya kuibadilisha dunia.

Profesa Juma alisema hayo katika mahafali ya 19 ya chuo hicho kwa wahitimu wa Stashahada na Astashahada ya Sheria.

“Katika fani ya sheria, moja ya njia ya kuinoa silaha hiyo ni kujisomea kila wakati kwa sababu sheria na kanuni huwa zinabadilika mara kwa mara. Sio vyeti vyenu vitakavyofanya kazi ya kutoa huduma. Kwa kuhitimu hivi haina maana mtakuwa mmemaliza kujifunza masuala yote ya kisheria.

“Mnapaswa kuendelea kuwa wanafunzi kila wakati ili kujua sheria mpya na kanuni zake pindi zinapobadilika. Mhitimu mzuri ni yule anayeacha milango wazi ya kujifunza kutoka kwa wengine,”alisema Jaji Mkuu.

 Aliwaasa wahitimu hao popote watakapokuwa kujifunza jambo jipya kila siku wasipitwe na wakati ili kutoiaibisha fani yao, hivyo  wajiendeleze hadi kufikia viwango vya juu katika fani hiyo muhimu.

“Jengeni tabia ya kujisomea wenyewe vitabu ili kuendelea kujielimisha. Kamwe usimtegemee mtu mwingine asome kisha akuelekeze.

“Katika kujisomea, hakikisheni mnasoma mambo yasiyo ya kisheria kwa mfano hivi karibuni, Rais mstaafu Benjamin William Mkapa alizindua kitabu chake,” alisisitiza.

Alisema kitabu hicho kitawaongezea ufahamu wa historia ya nchi kupitia miaka 81 ya maisha ya rais huyo mstaafu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa chuo hicho, Jaji Dk. Gerald Ndika, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, alisema mahafali hayo yamefanya jumla ya wahitimu 6,037 katika ngazi ya Stashahada na Astashahada ya Sheria tangu kilipoanzishwa mwaka 2001.

Mkuu wa chuo hicho, Jaji  Dk. Paul Kihwelo akizitaja  takwimu za wahitimu hao kwa mwaka huu kwa upande wa Stashahada ya Sheria, alisema kati ya wahitimu  169 wanaume ni 93 sawa na asilimia 55.03 na wanawake ni 76 sawa na asilimia 44.97 na kwa upande wa Astashahada ya Sheria, kati ya wahitimu 234 wanaume ni 102  sawa na asilimia 43.59 na wanawake ni 132 sawa na asilimia 56.41.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles