24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Vigogo kumpokea Lowassa Monduli

DAR ES SALAAM

WIKI moja baada ya yeye mwenyewe kusema amerudi nyumbani yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, leo anatarajiwa kupokewa rasmi na vigogo wa chama hicho.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa Lowassa atapokewa na viongozi wa juu wa CCM katika ofisi cha chama hicho Wilaya ya Monduli.

Miongoni mwa viongozi wa CCM wanaotajwa kuwamo kwenye hafla ya kumpokea Lowassa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Bashiru Ally na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole.

Akizungumza na gazeti hili, Polepole, alisema Lowassa atapokelewa leo saa tano asubuhi katika ofisi za CCM Wilaya ya Monduli.

Kupokelewa kwa Lowassa CCM baadhi wanaona kunaweza kukafufua upya ajenda zake kuu mbili ambazo amekuwa akiziamini na kuzisimamia kwa muda mrefu.

Ajenda hizo ni pamoja na elimu ambayo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 aliibeba katika majukwaa ya kuomba kura dhidi ya Rais Magufuli.

Lowassa amekuwa akitajwa nyuma ya mafanikio ya uanzishwaji na shule za kata na ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ajenda nyingine ni ajira ambapo amekuwa akisema wazi juu ya tatizo hilo kiasi wakati fulani akajikuta akiingia katika vita ya maneno na baadhi ya viongozi wa Serikali iliyopita.  

Jumamosi iliyopita, Lowassa alitangaza kurudi rasmi CCM akitokea Chadema alikokaa kwa takribani miaka mitatu.

Kabla ya kurudi sasa, Lowassa alihama CCM baada ya jina lake kukatwa kimizengwe katika mchakato wa kupitisha mgombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015 ambapo Rais Dk. John Magufuli, alisimamishwa na kushinda.

Rais Magufuli ndiye aliyeongoza shughuli ya kumpokea Lowassa katika Ofisi Ndogo ya CCM, Makao Makuu, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli ambaye alikuwa sambamba na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula na baadhi ya makada wa chama hicho akiwamo Rostam Aziz, alisema Lowassa amerudi nyumbani.

“Ndugu zangu kama alivyozungumza, Lowassa ametumia maneno mafupi, amerudi nyumbani na nyumbani ni hapa CCM, ndio maana amesimama kwenye jengo la Makao Makuu Ofisi ndogo ya CCM,” alisema Rais Magufuli.

Naye Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru, alipozungumza alisema, Lowassa, ametangaza kurudi nyumbani na wamempokea.

 “Ametangaza kurudi nyumbani na tuko tayari kumpokea,” alisema Dk. Bashiru.

Kurudi kwake CCM kumeonekana kuwashtua wengi na hasa upande wa upinzani ambako alipeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi, (Ukawa) na kutoa upinzani mkali kwa Rais Magufuli.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, akizungumza na gazeti la MTANZANIA Jumapili wiki iliyopita, alikiri mambo kadhaa ikiwamo kesi dhidi ya viongozi wake, tukio la Lissu, hamahama kukipitisha chama hicho katika wakati mgumu.

Mrema ambaye alizungumza mara mbili tofauti na gazeti hilo, alisema ukiachia mbali hoja ya kuvurugwa kwa njia hizo pia zipo hoja nyingine kama za kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara pamoja na vikao vya Bunge kutoonyeshwa mubashara.

Alisema mbinu hizo zililenga kubana mwanya wa hoja za viongozi wa Chadema kuwafikia wananchi.

Aliongeza kwa kusema pamoja na kuvurugwa kiasi kutokana na matukio kadha wa kadha ambayo yamewakumba viongozi, lakini chama hicho kilitambua mapema dalili za kuvurugwa hivyo kikaamua kujipanga kwa kuwa na mbinu mbadala ya kuendelea kukijenga.

Kuhusu kuondoka kwa Lowassa, Mrema alisema: “Mimi binafsi sikuwa na taarifa hizo, nisisemee wenzangu labda alieleza wenzangu, bado hatujakaa tukaulizana isije kuwa alimweleza mmoja wa viongozi.”

Baada tu ya Lowassa kurudi CCM, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, yeye aliandika kupitia akaunti yake ya Twitter  kuwa: “Kama kuna jambo la maana kubwa Lowassa amefanyia Chadema ni kuondoka Chadema kurudi CCM.”

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, naye aliandika kwa kifupi ujumbe kupitia akaunti yake ya Twitter kuwa: “Msiogope”.

Dk. Mashinji naye aliandika: “…mambo mengi huishia kama yalivyoanza…”

Nalo Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), liliandika ujumbe kwa kunukuu mistari kupitia kitabu cha Biblia Takatifu ambao unasomeka:

“Maandiko yanasema 1 Yohana 2:19, Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si wote walio wa kwetu.”

Kwa upande wa CCM hali ilikuwa tofauti katika mitandao ya kijamii, ujumbe wa wengi wakiwamo wale waliokuwa wakimdhihaki wakati alipokuwa Chadema ulikuwa ukisomeka: “Karibu nyumbani”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles