22 C
Dar es Salaam
Sunday, May 28, 2023

Contact us: [email protected]

Uzazi wa mpango Geita Mjini wafikia asilimia 35

Na Yohana Paul, Geita

AFISA Muuguzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani hapa, Rehema Kitoa amesema kuwa matumizi ya huduma za uzazi wa mpango Geita mjini yameongezeka na kufikia asilimia 35 hali inayoonyesha mwelekeo mzuri wa kukua kwa uelewa wa elimu ya afya ya uzazi.

Kitoa alisema hayo juzi wakati wa semina kwa viongozi wa dini, viongozi wa vijiji, kata na halmashauri ya mji wa Geita kulenga kupanua uwigo wa uelewa wa matumizi sahihi ya uzazi wa mpango, kupunguza mimba za utotoni na kutoa huduma rafiki za uzazi kwa vijana.

Alisema ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya hivi karibuni tathimini imeonyesha uwepo wa mabadiliko makubwa ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango hali iliyochangia kwa kiwango kikubwa kupunguza vifo vya kina mama wajawazito.

“Ukichukua takwimu za mwaka jana na mwaka juzi, tunaona kwamba kwa kipindi cha mwaka 2019 utumiaji wa uzazi wa mpango ulikuwa ni asilimia 29 lakini kwa kipindi cha mwaka 2020 tumeweza kufikia asilimia 35.

“Tafiti zinaonyesha kwa asilimia 44 matumizi ya uzazi wa mpango yanapunguza vifo vitokanavyo na uzazi, jamii yetu tunaendelea kuihamasisha kupitia wadau mbalimbali ambao wamekuja na mikakati tofauti wakisaidiana na halmashauri ya mji kwa lengo la kuongeza matumizi ya uzazi wa mpango.

“Kama hivi leo tulivyokusanyika mahala hapa, tunafikisha kauli mbiu ya ‘Tupange Kwa Pamoja’, inamaana kila mwana jamii aliyeko katika halmashauri yetu aweze kujua habari ya uzazi wa mpango na hata vituo viweze kutambulika ni wapi huduma ya uzazi wa mpango inaweza kitolewa.

“Katika mradi huu tumejikita zaidi katika halamshauri za miji na manispaa, kwani ndiyo sehemu zenye mkusanyiko mkubwa wa watu ndiyo maana tunaendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi tukipitia mashuleni pamoja na kushirikiana na viongozi wa kijiji au kata kupata sehemu maalumu na kutoa elimu,” alieleza Kitoa.

Muuguzi Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Caritas Ntambi alisema mradi huo kupitia shirika la Tupange Pamoja unatekelezwa kupitia vituo vua afya 15 ndani ya halmashauri ya mji wa Geita na wamelenga hadi kukamilika miaka mitatu ya mradi kufikia asilimia 50 ya matumizi ya uzazi wa mpango.

Afisa Usitawi wa Jamii Halamshauri ya Mji wa Geita, Carthbert Byabato alisema mradi huo wa Tupange Pamoja umelenga kuwashirikisha kina baba ili mchakato wa kupanga idadi ya watoto ndani ya familia uwe jumuishi na pia utawafikia wanafunzi ili nao waweze kuelewa namna ya kuepuka mimba za utotoni.

Diwani wa Kata ya Kasamwa na Mwenyekiti wa Kata ya Afya, Elimu na Uchumi, Mary Kasanda alisema elimu inayotolewa itasaidia kubadili mitazamo hasi juu ya matumizi ya uzazi wa mpango ikiwemo dhana potofu kwamba matumizi ya uzazi wa mpango yanasababisha kuzaa watoto wenye upungufu wa akili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,167FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles