24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

UTEUZI WA GAVANA MPYA WATIKISA

Profesa Florens Luoga

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amemtangaza Profesa Florens Luoga, kwamba atakuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mara baada ya muda wa Profesa Benno Ndulu, kumalizika Desemba mwaka huu.

Mara baada ya kumtangaza Profesa Luoga, alisema ana imani kuwa, Profesa Ndulu atamkabidhi haraka ofisi Profesa Luoga, ambaye ni mbobezi wa sheria za kodi.

Katika hali ambayo haijazoeleka, Rais Magufuli alitangaza uteuzi huo wakati akizungumza mara baada ya kutoa vyeti vya heshima kwa wajumbe walioshiriki mazungumzo na Kampuni ya Madini ya Barrick na kuibuka na mafanikio lukuki.

Imezoeleka kuwa, mara nyingi Rais hufanya uteuzi kisha, Kurugenzi ya Mawasiliano, kutoa taarifa kwa umma, lakini mtindo wa jana ulionekana kushtua wengi.

Profesa Luoga alikuwa miongoni mwa wajumbe waliotunukiwa cheti cha heshima.

Akizungumza baada ya kutoa vyeti hivyo, Rais Magufuli alisema amemteua gavana kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya mashauriano kuhusu madini kutokana na kuridhishwa na kazi yao.

Kutokana na hilo, aliamua kumtaja Profesa Luoga kuwa ndiye atakuwa gavana mpya wa BoT, huku akisema hakumwambia lakini tayari amemteua.

“Wapo watu wanafungua akaunti katika nchi ambazo hazitozi kodi. Wengine ni kupinga tu kwa sababu wamepewa pesa, tuna sheria ambazo wakati mwingine hatuzitumii mfano ile ya mwaka 1992 inayodili na akaunti za nje tumekuwa hatuzitumii.

“Ndiyo maana nazungumzaga kwamba kwanini BoT haikuzuia haya mambo kwanini wameruhusu?  Ili tujue hizo fedha wanazoziingiza.

“Wengine wakati mwingine ukizungumza watasema unamsema fulani…Profesa Ndulu amefanya kazi nzuri sana anamaliza muda wake Disemba au Januari anatakiwa kumaliza hiyo kazi.

“Imebaki miezi kama miwili awe amekabidhi ofisi kwa yule nitakayemteua… nimeamua kumteua gavana miongoni mwa hawa niliowapa vyeti leo.

Nimemteua Profesa Luoga mara baada ya kumkabidhi cheti, nina uhakika aliyepo (Profesa Ndulu) atafanya haraka haraka kumkabidhi, tulikuwa tuna upungufu pale kwenye taxation law,”alisema Rais Magufuli.

PROFESA LUOGA AFUNGUKA

Akizugumza baada ya uteuzi huo, Gavana mteule wa BoT, Profesa Luoga alisema amepokea kwa heshima kubwa dhamana aliyopewa na Rais Magufuli na kwamba anatambua changamoto za nafasi hiyo.

Profesa Luoga ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) – Taaluma, alisema atatumia wataalamu wa BoT kufanya kazi zake na anahitaji ushirikiano wa kila mtu katika kufanikisha kazi aliyopewa.

“Nimepokea kwa heshima dhamana niliyopewa na Rais Magufuli nikitambua kwamba zipo changamoto.

“Nitakwenda kujifunza zaidi kwa sababu sijawahi kuwa gavana…nitatumia wataalamu waliopo katika kutekeleza majukumu yangu,”alisema Profesa Luoga.

Profesa Ndulu anayemaliza muda wake, amekuwa Gavana wa BoT tangu ateuliwe na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2008.

WACHUMI WATOA MAONI

Mtaalamu wa Uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, alisema Rais Magufuli amefanya uamuzi mzuri kumteua gavana mpya mapema ili aweze kujiandaa.

“Ni kawaida muda wa anayemaliza unafahamika, nafasi ya ugavana ni kubwa ni vizuri ametangazwa mapema ili aweze kujiandaa.

“Wengine wanasema lazima gavana awe mchumi na Profesa Luoga ni mwanasheria lakini si lazima awe mchumi, hakuna mahali sheria imesema lazima awe mchumi.

“Lakini akiwa kama mtendaji mkuu sasa wa BoT na ikizingatiwa shughuli za benki ni masuala ya uchumi, hivyo bodi yake inapaswa kumsaidia sana na sisi wengine wa pembezoni nao tunapaswa kumsaidia,” alisema Profesa Ngowi.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema nafasi aliyopewa Profesa Luoga anaiweza kabisa kwa sababu ana uwezo mkubwa.

“Kuna watu wanasema ni mwanasheria lakini watu hao hawamjui Profesa Luoga, kwa sababu kwenye mafunzo ya sheria mwaka wa kwanza na wa pili, wanafundishwa mambo ya uchumi.

“Hii nafasi anaiweza kabisa yeye ni mtaalamu wa sheria uchumi na ni mtu yuko very humble (mnyenyekevu) na atafanya kazi hiyo kwa kufuata sheria,”alisema Profesa Semboja.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi huo mapema kwa sababu sasa gavana mpya atasaidiwa kupewa taarifa zote na Profesa Ndulu.

Huo ni uteuzi wa pili kwa Profesa Luoga, ambapo  Julai 11 mwaka huu Rais Magufuli alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).

Profesa Luoga alichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye bodi yake ilivunjwa na uteuzi wake kutenguliwa.

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Luoga alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA).

Profesa Luoga ni mtaalamu katika masuala ya sheria za kodi na amefundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu mwaka 1986 kabla ya kupandishwa cheo na kuwa profesa mshiriki (Associate Professor) mwaka 2005.

Ameshika nafasi mbalimbali chuoni hapo ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kamati ya misaada ya kisheria katika kitivo cha sheria mwaka 1993 -1995, mkurugenzi wa masomo ya shahada za awali (2005 – 2009), katibu wa baraza la chuo kikuu (2009 – 2013) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma (2013 hadi sasa).

Profesa Luoga aliyezaliwa mwaka 1958 ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Alihitimu shahada ya kwanza ya sheria UDSM mwaka 1985.

Baadaye alikwenda kusoma Shahada ya Uzamili (LLM) katika chuo cha Queen’s University cha Canada (1988).

Mwaka 1988 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa (MIL) katika Chuo cha Lund University cha Sweden (1991) na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza mwaka 2003.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles