26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAANDISHI WASUSIA POLISI

Na MWANDISHI WETU-GEITA

JESHI la Polisi mkoani Geita limeingia katika mgogoro na waandishi wa habari wanaolituhumu kuwa linawanyanyasa.

Wakati hayo yakijili mkoani Geita, jana Mwandishi wa habari wa Gazeti la Nipashe mkoani Dodoma,  Augusta Njoji alishikiliwa Polisi kwa takribani saa tano kwa madai ya kuandika habari ya kulichafua.

Akitangaza uamuzi wa kuwa na mgogoro na polisi, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita, Daniel Limbe alisema habari zinazolihusu jeshi hilo hazitaandikwa.

Alisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha dharura cha viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Geita, kilichoketi jana kujadili unyanyaswaji unaofanywa na polisi dhidi ya waandishi wa habari.

Alisema uamuzi huo utasitishwa iwapo polisi wataomba radhi na kuwahakikishia waandishi usalama wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Limbe alionya kuwa mwandishi wa habari atakayekiuka uamuzi huo atachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufutwa uanachama.

Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku mbili baada ya polisi kuwatandika bakora waandishi wa habari wanne na kuharibiwa vifaa vyao vya kazi wakiwa wanaripoti tukio la vurugu zilizotokea Shule ya Sekondari Geita (Geseco).

Katika tukio hilo, inadaiwa kuwa wanafunzi walitishia kuichoma moto shule iwapo wenzao watano waliokuwa wanashikiliwa na polisi hawataachiwa.

Waandishi waliotandikwa bakora ni Editha Edward wa Gazeti la Mtanzania, Rehema Matowo wa Mwananchi, Ester Sumira wa Azam Televisheni na Emmanuel Ibrahimu wa Clouds Media.

Wakati huo huo, taarifa kutoka mkoani Dodoma zinaeleza kuwa Mwandishi wa Gazeti la Nipashe, Augusta Njoji jana alishikiliwa polisi kwa takribani saa tano akituhumiwa kuandika habari ya kulichafua.

Njoji aliachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni tano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Dodoma (CPC) Habel Chidawali, polisi wanalalamikia habari iliyochapishwa katika Gazeti la Nipashe, toleo la siku ya  Jumamosi, wiki iliyopita ikilihusisha na kashfa ya utata wa mkataba wa ununuzi wa magari 770 ya maji ya kuwasha, maarufu kama washawasha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles