27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Upigaji chapa ng’ombe ni urasimishaji sekta mifugo

picha-ngombe

Na Lilian Justice, Morogoro 

UTAMBUZI  na Ufuatiliaji Mifugo ni mfumo unaowezesha kuwa na alama na kumbukumbu ya mifugo  kupitia usajili wa mifugo yenyewe, wamiliki wake, mahali ilipo na matukio muhimu kwenye uhai wa mifugo hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani – OIE utambuzi wa mifugo unajumuisha pia usajili wake (OIE Terrestrial Animal Health Code).

Utambuzi wa mnyama unaweza kuwa wa mnyama mmoja mmoja au wa kundi kwa maana ya alama moja kwa kundi la wanyama, mfano hapa Tanzania Utambuzi wa wanyama kwa kundi unafanyika kwa kila kijiji kuwa na alama moja ya chapa ya utambulisho wa kitaifa.

Historia ya Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo Tanzania (TANLITS) inaanzia kwenye Mkutano wa Taifa wa wadau wa mifugo uliofanyika Arusha mwaka 2002 chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Rais wakati huo Mhe Benjamin William Mkapa. Moja ya maazimio ya Mkutano huo ni kuwa na ufugaji wa kibiashara ulio endelevu ifikapo mwaka 2025.

Maazimio ya wadau yalifuatiwa na kutungwa kwa Sera ya Taifa ya Mifugo mwaka 2006 ambayo ibara ya 3.10 ilihusu tamko la kuanzishwa kwa Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo.

Akizungumzia kuhufu madhumuni  ya Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo nchini Daktari wa mifugo Mkuu mfumo wa utambuzi na ufuatailiaji wa mifugo Dr. Stanslaus   Kagaruki anasema kuwa  ni nyenzo muhimu kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kukabili magonjwa ya mlipuko, kuimarisha koo saafu za mifugo, hakikisho la usalama wa chakula, soko la mifugo na mazao yake, bima na mikopo, kusaidia kudhibiti wizi wa mifugo na mengineyo yanayohusiana na haya.

Kagaruki anaeleza  kuwa mfumo  wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo ni nyenzo muhimu kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kukabili magonjwa ya mlipuko, kuimarisha koosaafu za mifugo, hakikisho la usalama wa chakula, soko la mifugo na mazao yake, bima na mikopo, kusaidia kudhibiti wizi wa mifugo na mengineyo yanayohusiana na haya.

Anasema kuwa lengo kuu ni   kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya jamii ya wafugaji na kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla  kupitia kukuza soko la mifugo na mazao yake  na kuongeza usalama wa rasilimali za mifugo.

Aidha anaeleza kuwa kumekuwepo na  changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa mfumo huo  na kufanya upanuzi wa mfumo na utekelezaji kukwama ambapo miongoni mwa changamoto hizo ni upatikaji wa rasilimali fedha  ,utekelezaji katika ngazi ya kijiji ilitarajiwa kuwa kazi hii ingefanywa na mtaalamu wa ugani wa kijiji kama suala la utekelezaji wa kawaida (routine) wakati wa utoaji huduma za ugani.

Hata hivyo imedhihirika baadae kuwa zoezi hili kwa mara ya kwanza (first tagging and branding) linahitaji fedha za kuanzia (kick-start) ili kufanyika kwa njia ya kampeni ya chapa na uwekaji wa hereni/ tufe la tumboni ambapo pia usimamizi ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa pia inahitaji fedha kuwezesha kusafiri, kusambaza vifaa vya utambuzi, mafunzo na ushauri wa kitaalamu.

Aidha anaeleza changamoto  nyingine ni upatikanaji  wa taarifa za msingi kama orodha ya wafugaji, mashamba, vijiji n.k katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) ni changamoto ambayo kwa kiwango kikubwa inatokana na wataalam kuwa na mtazamo wa miradi katika utendaji wao na hivyo kusababisha utekelezaji duni wa mfumo wa TANLITS.’’anasema .

Hata hivyo Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro inatekeleza   agizo hilo la serikali la  kufanya utambuzi , usajili  na ufuatiliaji wa mifugo kwa lengo la kupiga chapa mifugo hiyo.

Akielezea kuhusu zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl.  Mohamed Utaly anasema kuwa  zoezi la  kupiga chapa mifugo lipo kisheria  kutokana  na sheria namba 12 ya mwaka 2010  ambapo anasema kuwa mpango huo ni utekelezaji wa sheria  inayolenga wafugaji kupiga chapa mifugo yao sambamba na kuorodheshwa mifugo yao  katika daftari maalumu  ili  mwisho wa siku iweze kubainika idadi kamili ya mifugo iliyopo katika wilaya nzima.

“Endapo mifugo haitapigwa chapa itachochea  kuendelea kuwepo kwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji na pia kuwa na uwezekano mkubwa wa kuingia mifugo mipya bila taarifa ndani ya wilaya,’’anasema.

Hata hivyo anabainisha kuwa serikali  ina lengo la  kuboresha miundombinu ya wafugaji  hususani majosho , malambo , masoko ya ndani na nje ya nchi   hivyo haina budi kujua idadi kamili ya mifugo iliyopo , nyama inayozalishwa   na hata mfugaji mwenyewe aweze kujulikana .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Florent Kyombo   anabainisha kuwa zoezi hilo  linaendeshwa  kwa wafugaji katika vijiji vyote ndani ya wilaya hiyo na kuwataka  wafugaji kujitokeza  zaidi katika kufanikisha zoezi hilo.

Kyombo anasema kuwa endapo mifugo hiyo itapigwa chapa hususani ng’ombe itapelekea kuwepo kwa mazingira mazuri ya malisho,kupata maji, nyama kuuza katika masoko mazuri sambamba  kuzalisha zaidi mifugo.

Aidha anawataka viongozi wa vijiji , viongozi wawakilishi wa wafugaji ,maafisa mifugo  kuwahamasiaha wafugaji  kujitokeza   katika zoezi hilo  la kupiga chapa mifugo kwani zoezi hilo lina manufaa kwao na ni agizo la serikali.

Hata hivyo anatoa onyo kwa wale watakaokaidi agizo la kupiga chapa mifugo yao watatozwa faini ya kiasi cha shilingi milioni 2 ama kifungo  cha miezi sita  kwani wanakiuka agizo  zuri la serikali.

Naye Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo Daniel Pangani anaeleza kuwa  lengo la kuwepo kwa zoezi hilo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria  inalenga  kudhibiti  magonjwa ya mifugo,kudhibiti wizi wa mifugo.kuboresha  mazao ya mifugo  nyama na mazao na pia kuboresha soko  la mifugo  ndani na nje ya nchi   sambamba na kusimamia  usafirishaji wa mifugo na kusaidia  kuweka majosho na malambo na pia kujua idadi ya mifugo iliyopo.

Pangani anaeleza kuwa  kufanyika kwa zoezi hilo kutasababisha  kupatikana kwa masoko  maalumu kwa ajili ya kuuza  mifugo yao  kwa bei nzuri na hivyo kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

Afisa huyo anasema kuwa katika zoezi hilo sehemu maalumu ya kupiga chapa  ni mguu wa nyuma kulia chini ya paja  ambapo ngombe kuanzia umri wa miezi 6 hadi 12 anaweza kupigwa chapa  bila ya kupata madhara yoyote ama kujali ana umri mdogo ama mkubwa  na pia kuvalisha hereni kwa wale ng’ombe wanaofugwa majumbani.

“Niwaondoe hofu wafugaji kuwa hata ndama mwenye umri huo anaweza kupigwa chapa sawa na wale ng’ombe wenye umri mkubwa bila ya kupata madhara yoyote yale.’’anasema  Pangani.

Hata hivyo Afisa mifugo huyo anasema ifikapo Septemba 30 mwaka huu wafugaji wote ndani ya wilaya wawe wamefanya utambuzi, usajili na kupiga chapa mifugo yao na yeyote atakaebainika kukaidi agizo hilo atatozwa faini ya shilingi milioni mbili ama kifungo .

Hata hivyo anasema  kuwa zoezi hilo halina nia ya kukwamisha shughuli zozote za kimaendeleo ama serikali kuchukua mifugo ya wafugaji kama inavyodaiwa na baadhi ya watu  bali ni kuhakikisha inamwekea mfugaji miundombinu ya kisasa ili aweze kufuga  kwa tija  kama nguzo moja wapo ya kuimarisha uchumi wake na Taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa wafugaji Wilayani Mvomero Ngaye Muganya   anasema kuwa  bado jamiii ya kifugaji haina uelewa mkubwa  kuhusu suala la serikali la kuwataka kupiga chapa  mifugo yao na hivyo kuwaomba viongozi wanaohusika kufika katika maeneo yao ili kuwapa elimu zaidi.

“Bado jamii ya kifugaji haina uelewa   kuhusu zoezi hili hivyo tunaiomba serikali ya wilaya kutupa elimu zaidi  na kutuongezea muda ili kuweza kufanikisha zoezi hili,’’anasema Muganya.

Kwa upande wake mfugaji Ngirimo Sangaine  anaeleza  kuwa  bado jamii ya kifugaji haioni haja ya serikali kuwataka kupiga chapa mifugo yao kwani tayari wameshaweka chapa za asili katika mifugo yao.

“Sisi tunaona  hakuna haja ya kupiga chapa kwani tayari tunazo chapa zetu za asili kwani kupiga chapa ya serikali bado ni gharama.

“Uongozi wa wilaya  wametuambia kuwa gharama za kupiga chapa kila ng’ombe mmoja ni shilingi 1,000/-  bado sisi tunaona ni gharama,’’anafafanua.

Hata hivyo Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ina  jumla ya ngo’mbe  163,000   huku  bado wafugaji wakikabiliwa  na changamoto mbalimbali ikiwemo miundombinu mibovu ya  minada.

Hata  hivyo ili kuleta mapinduzi katika sekta ya mifugo, changamoto hizi na zingine ambazo hazikutajwa hapa, zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi ambapo Wizara kwa kushirikiana na wadau wake wanatakiwa kushirikiana kwa karibu ili kupanga mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto zilizopo.

Pia mauzo ya mifugo minadani yanaendelea kuongezeka  huku  minada mingi iko katika hali isiyo ya kuridhisha na inahitaji kuimarishwa zaidi ili ifanye kazi kwa ufanisi kwani uuzaji wa mifugo nje ya nchi bado ni kidogo sana kwani soko linalotegemewa ni, Comoro na nchi jirani ambazo mahitaji yao yanabadilika mara kwa mara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles