25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 4, 2022

Contact us: [email protected]

Ni muhimu watu kulipa kodi bila shuruti

Miundombinu kama daraja la Kigamboni hujengwa kutokana na kodi za wananchi.
Miundombinu kama daraja la Kigamboni hujengwa kutokana na kodi za wananchi.

Na  Gabriel Mwangosi

Tangu kuumbwa kwa ulimwengu, kodi limekuwa jambo gumu kwa wanajamii wengi kulitekeleza kwa hiari bila kushurutishwa. Kodi inajulikana kwa umarufu wake wa kuwa ni mchango wa lazima ambapo kila mwanajamii anatakiwa kushiriki kikamilifu kulipa kodi inayoendana na kipato chake katika biashara, ajira na uwekezaji wa rasilimali au matumizi ya huduma fulani ambayo manufaa yake yanatakiwa kulipiwa kodi. Kodi inatakiwa kuwa ya haki kwa kulipwa kwa kiwango sahihi na kwa wakati unaotakiwa kisheria.

Sababu muafaka kulipa kodi

Kuna sababu tatu kubwa ambazo zinaifanya kodi iwe jambo la muhimu sana katika maisha ya mwanadamu duniani kote.

Kwanza Kodi ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya mapato ya serikali. Serikali ni taasisi moja kubwa katika nchi ambayo inabeba majukumu yote ya kijamii, kiuchumi na kisiasa na kuhakikisha kuwa kila jambo linaenda vizuri.

Shughuli zote hizi za serikali haziwezi kuenda mbele na kuwa na tija kwa wananchi bila ya kuwepo fedha/mapato ya kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake.

Hivyo basi serikali lazima ikusanye kodi kikamilifu kutoka kwa wahusika wote na kuwa kila mwananchi au mgeni hapa nchini alipe kodi stahili/stahiki.

Mwananchi akilipa kodi anakuwa ametekeleza wajibu wake wa kimsingi, hivyo kupata haki ya kudai huduma bora kutoka serikalini.

Sababu ya pili, kodi inatumika kama nyenzo au chombo cha kurekebisha mwenendo wa uchumi wa nchi kwa kipindi husika. Hii inatokana na ukweli kuwa, uwezo wa kiuchumi miongoni mwa wananchi unatofautiana toka mtu mmoja na mwingine, hivyo kodi hutumika kama njia ya kugawanya utajiri au uwezo wa kiuchumi wa nchi kwenda kwa wananchi wake.

Utaratibu huu unapunguzi nafasi iliyopo kati ya walionacho na wale wasionacho kwa njia ya kodi na mtindo wa utoaji wa huduma ambazo vyanzo vyake vya mapato ni kodi kwani kodi inalipwa na mtu mwenye uwezo wa kuilipa kodi husika.

Njia  za Kukadiria na Kulipa Kodi

Mtindo wa ukadiriaji na ulipaji kodi umejengwa kwenye aina za kodi. Kupitia utaratibu huu, kila mmoja analazimika kushiriki katikaulipaji kodi kupitia aina ya kodi ambayo shughuli zake zinahusiana nae.

Mamlaka ya Kodi (TRA) inasimamia na kukusanya kodi kutoka vyanzo vifuatavyo:-

Kodi ya Mapato Mwaka 2004

Kodi ya mapato; hii ni aina ya kodi ya moja kwa moja ambayo hutozwa kwa mtu mwenye kipato. Kodi hii inasimamiwa na TRA kupitia sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004.

Mlipakodi  anaweza kuwa binadamu au kampuni na kulazimika kulipa kodi ya mapato ya makampuni, watu binafsi, kodi mapato yatokanayo na ajira, gawio la faida ya kampuni, mapato ya pango ya majumba  na nyumba na  Kodi ya uwekezaji wa rasilimali.

Jambo la kuzingatia katika utozaji kodi ya mapato ni kipato au faida. Bila kipato haiwezekani kutoza kodi ya mapato. Ni uvunjaji wa sheria kwa yeyote mwenye kipato kutojitokeza na kulipa kodi inayostahili. Kodi hutozwa viwango vya asilimia thelathini (30%) ya kipato kwa mwaka kwa makampuni na watu binafsi ni kuanzia asilimia tisa (9%) hadi 30% ya kipato kutegemea uwezo wake na kiwango cha kipato alichochuma katika kipindi husika.

Kodi Ongezeko Thamani Ya Mwaka 2004

Kodi ya Ongezeko la Thamani au kifupi VAT ni kodi inayotozwa na kulipwa na mlaji au mtumiaji wa huduma au bidhaa ambazo zinatozwa kodi. Kodi hii inakusanywa na mfanyabiashara aliyesajiliwa na TRA kukusanya kodi na kuipeleka au kuiwasilisha TRA ndani ya siku 20 baada ya mwezi husika. Kodi ya Ongezeko la Thamani inasimamiwa na Sheria ya VAT ya mwaka 2014 ambayo imeanza rasmi kutumika 1 Julai, 2015. Sheria hii imekuja baada ya kufutwa kwa sheria ya mwaka 1997 ya VAT kwa sababu ya sheria hiyo kupoteza maudhui ya kuundwa kwake kutokana na marekebisho na viraka vingi na kuifanya sheria ikose mwelekeo wa kuundwa kwake.

Sheria hii inamtaka kila mwenye kununua bidhaa au huduma inayotozwa VAT kulipa VAT kwenye manunuzi hayo au matumizi. Ili kuhakikisha kuwa kodi imelipwa, ni lazima muuzaji atoe risiti na mnunuzi adai risiti za kielektroniki za EFDs vinginevyo kodi hiyo itapotelea mikononi mwa mfanyabiashara huyo aliyeikusanya kodi hiyo. Mfanyabiashara aliyesajiliwa kutoza VAT anao wajibu mkubwa kuhakikisha kuwa analipa kodi wakati wa manunuzi ya bidhaa au huduma na anatoza kodi wakati wa mauzo ya bidhaa hizo. Mnunuzi wa bidhaa anawajibika na kuhakikisha kuwa anadai risiti katika manunuzi yote anayofanya.

Kodi  Ushuru Wa Forodha na Bidhaa

Kodi ya Ushuru wa Forodha inatozwa katika bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nchi za nje. Kodi hii msingi wake wa utozaji kodi ni kuwa bidhaa hizo zimetoka nje ya nchi hivyo ili ziruhusiwe kuingia nchini, kodi ya ushuru wa forodha lazima itozwe iwapo bidhaa hizo hazijasamehewa kutozwa kodi.

Utozaji wa kodi hii upo chini ya sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Ushuru wa pamoja ya mwaka 2004. Viwango ya utozaji kodi hiyo vimeainishwa ndani ya sheria na vinafuata makubaliano ya kimataifa kuhusu utozaji wa kodi hiyo (World Customs Organization).

Ada na Tozo Mbalimbali

Pamoja na kodi zilizotajwa hapo juu, bado serikali inakusanya ada na tozo mbali mbali kwa nia ile ile ya kuongeza uwezo wa serikali kuweza kuwahudumia wananchi wake katika masuala yote ya kimaendeleo. Tozo hizo ni Ushuru wa stampu, Ada ya leseni za udereva, ada ya leseni ya magari( road license), Ada ya kutumia viwanja vya ndege na bandari.

Matumizi Ya Kodi

Kodi inatumika na serikali katika kugharamia shughuli za kijamii, maendeleo na siasa.

Shughuli za kijamii:

Ni  pamoja na kujenga shule, kufundisha waalimu, kununua vifaa vya shule, mishahara ya waalimu, ulinzi na usalama wa mali na raia wa Tanzania, kununua vifaajeshi kwa ulinzi, afya kukabiliana na maafa n.k.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,544FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles