21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Tuzo TPSF bidhaa bora kuleta ushindani

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya sekta binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye

Na HAMISA MAGANGA,

SHANI yasubiri Oktoba 7 mwaka huu wakati  wafanyabiashara wakubwa na wajasiriamali watapambana kuwania Tuzo ya Chapa Bora za Kitanzania 2016.

Tuzo hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Godfrey Simbeye, anasema kuwa lengo la kuanzisha tuzo hiyo ni kuongeza uzalishaji, ajira na mapato kwa Serikali.

Anasema kuwa TPSF inachofanya ni kuhimiza Watanzania kununua bidhaa bora zinazotengenezwa na viwanda vya ndani ya nchi na kutumia huduma bora za Tanzania.

“Tuzo hii inatokana na kampeni tuliyoipa jina la ‘Fahari ya Tanzania’. Lengo ni kuwazindua na kuwainua Watanzania, lakini pia kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati,” anasema Simbeye.

Anataja wadau walioshiriki kuandaa kampeni hiyo kuwa ni pamoja na  Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTARDE) na Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).

Pia wamo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

Simbeye anasema kuwa wanachokifanya ni kuhakikisha  wanatoa majibu ya ajira, kukuza ulaji/utumiaji wa bidhaa za ndani lakini pia kuleta chachu katika ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji katika bidhaa, huduma na uuzwaji wake nje ya nchi.

Anasema kuwa kampeni hii itaambatana na utoaji wa elimu kwa walaji wa ndani na nje ya nchi, kwamba wanapokuwa wanafanya manunuzi yao wafikirie kununua bidhaa zilizotengenezwa nyumbani kwao.

“Wakifanya hivyo watakuwa wametoa ajira kwa Watanzania wenzao, watatoa soko kwa bidhaa za ndani, watachangia ukuaji wa uchumi na kipato kwa wakulima ambao mazao yao ni malighafi katika uzalishaji wa bidhaa husika,” anasema Simbeye.

Anataja malengo mengine ya kampeni hiyo kuwa ni kuhamasisha uzalishaji unaotumia viwango vya ubora ili kukidhi matakwa ya soko.

“Pia tunahamasisha  utumiaji wa bidhaa za nchini zilizo kidhi ubora na viwango stahiki, kuhamasisha wazalishaji kuongeza thamani ya bidhaa au kuzalisha kwa kutumia malighafi za Kitanzania ‘Local Content’,” anasema na kuongeza kuwa pia wanahamasisha ushindani wa kuuza kwenye masoko ya nje ya nchi.

Anasema kuwa kampeni ya Fahari ya Tanzania inabebwa na maonesho na makongamano ya bidhaa na huduma za ndani, ambapo itakwenda sambamba na Tuzo kwa bidhaa na huduma bora za Kitanzania.

Anasema kuwa pia watatoa Tuzo bora za kutambua michango ya Watanzania mbalimbali na Lebo ya Fahari ya Tanzania.

Simbeye anaongeza kuwa pia wanafanya kampeni za kuhamasisha watu kununua bidhaa za nyumbani.

Akitoa sababu ya kuwashirikisha TBS katika kampeni hii, Simbeye anasema kuwa shirika hilo ndio lenye dhamana ya kuandaa na kudhibiti viwango vya bidhaa ndani ya nchi.

Akizungumzia faida ya Tuzo za Bidhaa Bora 50 Tanzania, anasema kuwa itawasaidia baadhi ya Watanzania kuwatambua wazalishaji wa bidhaa mbalimbali waliopo pembezoni – nje ya Dar es Salaam.

Simbeye anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa wanapata bidhaa 50 bora za Kitanzania, walizingatia vigezo mbalimbali ikiwamo bidhaa kuwa na viwango vilivyothibitishwa na TBS.

“Pia tunaangalia analipaje kodi, kama anatoa ajira kwa Watanzania, pia tunaangalia chapa ya bidhaa husika imeisaidiaje kampuni kuingiza faida,” anasema Simbeye.

Anasema kuwa katika shindano hilo pia zipo baadhi ya kampuni ambazo zimefadhili shindano na wakati huo huo zinashindana katika kinyang’anyiro hicho.

Anasema pamoja na kampuni hizo kushiriki zoezi la kuchagua washindi, wamezingatia vigezo na si kutoa upendeleo.

“Taratibu zetu za mashindano zilikuwa wazi, hakuna uhusiano kati ya kufadhili mashindano na kuwa mshindi wa chapa bora, kwa sababu wanaochagua Chapa Bora ni walaji na si waandaaji,” anasema.

Naye Meneja wa kampeni hiyo, Emmanuel Nnko, anataja bidhaa zinazolengwa katika kampeni hiyo kuwa ni zote zinazotokana na kilimo na zile za viwandani.

Akizungumzia uwazi uliotumika katika kushindanisha wafanyabiashara Nnko anasema; “Ili kushiriki mashindano haya kampuni zilikuwa zinatakiwa kujaza fomu ambazo zilikuwa zikipatikana katika tovuti ya TPSF na TBS au kuchukua fomu kutoka katika ofisi za TPSF na TBS.”

Akinukuu hotuba ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, aliyoitoa Septemba 30 2001; Simbeye alisema utengenezaji wa bidhaa bora na utoaji wa huduma bora, utaiwezesha Tanzania kuondokana na utegemezi kwa kuzalisha kilicho bora na kutoa huduma bora na hivyo bidhaa na huduma zake kushindana kimataifa kwa kuwa na ufanisi mkubwa.

Nnko anasema kuwa tuzo hizo zilishirikisha chapa 150 ambazo zilichujwa na kupatikana 50.

“Chapa hizi zilitokana na maoni ya washiriki zaidi ya 20,000 kutoka sehemu mbalimbali.

“Mikoa iliyoshirikishwa ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Dodoma, Mtwara, Mbeya na Mwanza,” anafafanua Nnko.

Anamtaja mgeni rasmi wakati wa utoaji wa Tuzo hizo kuwa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles