25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 8, 2022

Contact us: [email protected]

Upande wa pili mwanafunzi ‘Panya Road’

3

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

MKUU wa Shule ya Sekondari Lumo, Catherine Urio, amezungumzia tukio la kupigwa kwa mwanafunzi wake, Isack Ernest ambaye anahusishwa na kundi la uhalifu la Panya Road na kusema kuwa maisha yake ya shule hayaendani na anayodaiwa kuyafanya mtaani.

Isack mwenye umri wa miaka 16, anayedaiwa kuwa mwanachama wa kundi la uhalifu la ‘Taifa Jipya’ lililopo Mbagala, Dar es Salaam, Oktoba 15, mwaka huu alitiwa mbaroni na kupigwa na wananchi wenye hasira kali na kupoteza fahamu na kudhaniwa amefariki dunia.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika Shule ya Sekondari Lumo iliyopo Manispaa ya Ilala, Mkuu wa shule hiyo, Catherine, alithibitisha kumfahamu Isack na kusema kuwa ni mmoja wa wanafunzi wenye tabia nzuri na si mkorofi anapokuwa shule.

Kutokana na mkasa uliomkumba Isack, mwalimu Catherine alisema kuwa ameumia akiwa kama mwalimu wake na mzazi.

“Ni kweli Isack ni mwanafunzi wetu anasoma kidato cha tatu D. Ni mwanafunzi ambaye haendani na aina ya tukio analohusishwa nalo kwani amekuwa akihudhuria vizuri shuleni na darasani, hivyo imetushtua walimu na hata wanafunzi wenzake wamesikitika na wengine walikuwa wanalia baada ya kupewa taarifa hiyo.

“Ukiangalia mahudhurio yake tangu Januari mwaka huu, hakuhudhuria mara chache hapa shuleni na mara ya mwisho kabla ya mkasa uliompata alikuja Alhamisi iliyopita na Ijumaa ilikuwa siku ya mapumziko,” alisema huku akionyesha kitabu cha mahudhurio ya darasa analosoma Isack.

Aliongeza kuwa Isack hakuwa na uhusiano mbaya na wanafunzi wenzake kwani si mgomvi.

Alisema mwanafunzi huyo hakuwahi kupata kesi yoyote ya tabia mbaya shuleni hapo licha ya kwamba amekuwa hafanyi vizuri katika masomo.

“Kimasomo yupo nyuma kidogo, mfano mitihani iliyopita ya nusu muhula alifeli kwa kupata alama ‘F’ katika masomo yote na alishika nafasi ya 61 kati ya wanafunzi 77 wa darasani kwao. Lakini tofauti na hilo, hajawahi kupatikana na kosa lolote la tabia mbaya,” alisema mwalimu Catherine.

Alisema anafikiri alichoeleza Isack katika vyombo vya habari kuwa alifuatana na rafiki zake bila kujua madhumuni yao ni ukweli kwa kuwa tabia yake kwa ujumla si mbaya.

Kutokana na tukio hilo, mkuu huyo wa shule alitoa wito kwa wazazi kuwalea vizuri watoto wao wanapokuwa nyumbani na kushirikiana na walimu pale wanapoona kuna tatizo.

Alisema kinachoendela sasa ni kusubiri hatua zitakazochukuliwa na vyombo husika vya Serikali kwani suala hilo linawahusu wazazi zaidi.

Baba mzazi wa kijana huyo, Ernest Chalo, alinukuliwa na vyombo vya habari juzi akisema kuwa mtoto wake alimuaga anakwenda kuangalia mpira Mbagala huku yeye akiwa anafuatilia kwa njia ya runinga mchezo wa timu ya Simba na Kagera Sugar uliochezwa siku hiyo.

Isack alinukuliwa akidai kuwa wenzake walimfuata nyumbani kumtaka waende kwenye Tamasha la Singeli Mbagala na baada ya kumalizika, alifuatana nao.

Alisema kuwa wakiwa njiani, wenzake wakaanza kupora watu yeye akiwa hajui kilichokuwa kinaendelea kwani walimweleza walikuwa wanaenda kula.

Kutokana na tukio hilo, Isack aliwataja wenzake 10 ambao wameshikiliwa na Jeshi la Polisi pamoja na wazazi wao.

Jeshi hilo limesema kuwa litawafikisha mahakamani wazazi hao kwa kukiuka sheria ya mtoto ya mwaka 2009 kwa kushindwa kuwasimamia vyema watoto wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,682FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles